MKWAMO WA KISIASA ZANZIBAR

MFUMO WA VYAMA VINGI

Nchini UK (United Kingdom) katika uchaguzi wa mwaka 2010 hakuna chama cha siasa kilichoshinda uchaguzi, chama kimoja tu (Conservative) ndicho chama kilichopata kura nyingi kuliko vyama vingine lakini idadi ya kura zao hazikuwawezesha kufikia idadi inayotakiwa ya kuunda serikali, lakini wakawa na fursa ya kuunda serikali ya vyama viwili ambayo ni serikali yenye mfumo unaojulikana kwa lugha ya Kiingereza kama “Coalition”. Baada ya uchaguzi kwisha kukawa na mvutano wa siku-nenda siku-rudi mwishowe wakaja kuunda serikali na chama cha Liberal Democrats au Liberal Democrats wakaunda serikali ya pamoja na chama cha Conservative kuondoa kiwingu kilicho tanda baada ya masiku ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2010 kwisha. Kawaida katika mfumo huu wa muungano wa vyama ambavyo kila chama kina sera zake mwenyewe mbali na chama kingine lazima kutakuwa na migongano ya hapa na pale ambayo migongano hii mara nyingi hupelekea kujenga taifa na si ya kurudisha nyuma taifa na watu wake, na kila chama kilikubali na kuridhia kuondoa baadhi ya sera zake ili kupisha sera za chama kingine ambazo wote waliziona ni sera zenye makubaliano ya kujenga nchi na kuwaletea wananchi maisha mema na mafanikio.

Tanzania bara na visiwani, bila ya shaka vyama vyote vya siasa vina nia nzuri kwa walengwa wananchi wote wa Tanzania bara na visiwani katika kuleta maendeleo ya wananchi kuishi maisha mazuri na kuishi kwa amani, usalama na utulivu (na sina shaka na hili kwasababu vyama vyote vina nia nzuri katika kuleta maendeleo ya wananchi kwa bara na visiwani). Ukiangalia katika mkwamo na mvutano wa kisiasa Zanzibar ulipofikia kwa vyama vyote, ningependa kutoa nasaha yangu na ningeomba ichukuliwe kama ni ushauri tu kama ndugu yenu Mtanzania na Mzawa mwenzenu.

HALI YA KISIASA ZANZIBAR

Sababu kubwa ya kunipelekea kuandika makala hii, ni kuona kuna ishara zinaanza kujitokeza za ukosefu wa amani, ukosefu wa utulivu na ukosefu wa usalama kwa ndugu zetu wa Zanzibar ambayo ishara hiyo inaweza kusababisha kuwa ndiyo sababu ya kukosa amani nchi nzima (Mungu atulinde na hilo). Ukiangalia baada ya uchaguzi wa tarehe 25 Oktoba 2015, kuna vitu ambavyo vimejitokeza ambavyo mvutano wake unaweza kuleta athari kubwa sana kwa wananchi wapendao amani na utulivu Zanzibar. Na athari zake ni kuwa badala ya kuleta maendeleo ambayo wananchi wanatarajia katika miaka mitano na miaka kumi ijayo badala yake nchi itarudishwa nyuma miaka khamsini kimaendeleo kwasababu sote tunajua nini athari ya nchi iliyokosa amani na mifano ipo iliyotokea katika historia ya uhai wetu katika baadhi ya nchi za bara letu la Afrika nchi za jirani na nchi za mbali. Hali halisi iliyopo Zanzibar na si ya kutoka kwenye kinywa changu ni hali ambayo imeshajitokeza muhimu ni kuangalia nini la kufanyika kuanzia hapa. Hali iliyopo hivi sasa yenye kuleta mkwamo wa kisiasa wa Zanzibar ni kuna mambo madogo madogo ambayo yanajitokeza kila siku, lakini mambo makuu matatu nayo ni, (1) kuna kundi kubwa la watu wanaosema kuwa uchaguzi wa Zanzibar umefutwa, kundi hili ni kuanzia viongozi mpaka baadhi ya wananchi wamegawanyika, (2) na kila kundi kuanzia viongozi mpaka kuna baadhi ya wananchi wanaosema kuwa chama chao kimeshinda uchaguzi, (3) na vilevile kuna kundi kubwa la watu kuanzia viongozi mpaka baadhi wananchi wanaosema kuwa uchaguzi urudiwe. Hii ndiyo hali halisi iliyokuwepo hivi sasa nje nje katika vyombo vyote vya khabari, na ukiangalia haya makundi yanazidi kujigawa na yanazidi kuwa makubwa, je, kuna usalama au usalama utapatikana? Na’am.

Ukiangalia mambo hayo matatu yanayovutana mpaka hivi sasa kupelekea kutokufikia uamuzi wa mwisho wa wote kukubaliana na kuangalia mustaqbali wa Wazanzibar ni mfano wa ile inayoitwa “Bermuda Triangle Conspiracy” simaanishi kuwa hali ya kisiasa ya Zanzibar kwa tafsiri ya “Bermuda Triangle” yenyewe, lakini kwa tafsiri ya “Conspiracy” ya mambo hayo matatu yaliyofungamana katika hali ya mkwamo wa kisiasa ya Zanzibar, hali ya kuwa kila mmoja anaona kivyake ni sawa, pengine kumbe kweli inaweza kuwa ni sawa au pengine kumbe inaweza kuwa si sawa, na hali ya kuwa hali inaendelea kuwa vilevile bila ya mabadiliko, na itakuwa ni msiba mkubwa huu kwa ndugu zetu wa Zanzibar tusipoangalia vizuri marefu yake na mapana yake. Allah atulinde. Amin.

Alhamdulillah, nikiangalia Zanzibar vyama vyote vikubwa vya Zanzibar viongozi wao ni Waislam, na Mungu aijaaliye iendelee kuwa hivyo hivyo ikiwa Zanzibar tunaiombea utulivu, amani na usalama katika visiwa hivi vya Tanzania, kwasababu wazungu wana msemo unaosema “Horses for courses”. Tumeona mfano mzuri wa viongozi wetu, mashujaa wetu wa vyama vyote viwili, Dokta Ali Mohamed Shein (CCM), na Maalim Seif Sharif Hamad (CUF) na majopo ya vyama vyao pamoja na wanachama wao kwa ujumla katika uamuzi uliofikia kikomo wa mwaka 2010 kuunda serikali moja na Alhamdulillah miaka mitano imepita kwa salama bila ya kumwagika kwa damu. Hii ni subra kubwa ambayo imefanya miaka mitano imepita ukiangalia ni kama kufunga na kufungua jicho tu, siku zote ukifuata subra kawaida matokeo yake ni faraja. Nikiwa kama Mtanzania mwenzenu, nikiwa kama ndugu yenu, suala ambalo linanikera mpaka sasa ambalo ningeomba kutoa ushauri wangu kwa ndugu zangu wapendwa viongozi wote wa vyama hivi viwili ni kwamba, mambo yoote yenye sera za kuleta manufaa kwenye mambo ya kimsingi kwa Wananchi wa Zanzibar kwa mfano Afya, Ustawi wa jamii, Elimu, Utamaduni, Miundo-mbinu ya barabara na ujenzi wa majumba na makazi mazuri kwa wananchi, na kadhaa wa kadhaa… kwanini hayajafanyika miaka hii mitano iliyopita ikiwa viongozi wote wawili walikuwepo madarakani na kwanini tutarajie miaka mitano au kumi inayokuja basi akija kiongozi fulani kutakuwa na mabadiliko ya kimaendeleo Zanzibar, uzito na ugumu uko wapi? Hili suala ni la kuangaliwa kwa viongozi wote na nini linaweza kufanyika kuanzia hapa tulipo na kwenda kufikia malengo tarajiwa ya maendeleo ya Zanzibar na watu wake na maendeleo kwa Tanzania nzima chini ya Rais wetu muadilifu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dokta John Pombe Magufuli ambaye ndiye ufunguo wa maendeleo katika miaka mitano na miaka kumi ijayo katika nchi yetu hii ya TANZANIA (Mwenyezi Mungu amhifadhi) na ni Rais ambaye asiyeangalia itikadi ya kichama, ukabila, dini, rangi, kama alivyosema mwenyewe katika ziara yake mjini Arusha wiki hii, “…Na nataka niwaahidi mabadiliko yale niliyokuwa nayaahidi katika mpango wangu wakati nafanya kampeni, nitayatekeleza bila uwoga kwa nguvu zote na namuomba Mungu anisaidie. Nataka niwahakikishie, kuzaliwa kwa Tanzania mpya kunakuja… na mimi nitawatumikia Watanzania wote, uwe CHADEMA wewe ni wangu, uwe CUF wewe ni wangu, uwe CCM wewe ni wangu…”

Bila ya shaka hakuna katika viongozi atakayepinga haya maendeleo ya kimsingi kuyafikia wananchi wa Zanzibar hususan viongozi wenyewe wa vyama vyote vya Zanzibar, kwani haya niliyoyataja hapo juu ni mambo ya kimsingi kwa mwanadamu, na mambo mengineyo niliyoyataja hapo juu ni mambo ya kimsingi kwa nchi yenyewe, ili kuwaletea maendeleo wanaadamu wote wa Tanzania bara na visiwani. Nimetumia neno “wanaadamu” badala ya neno “wananchi” nikiwa na maana yote moja lakini nimetumia neno Wanaadamu ni kulingania kuwa ndiyo hali halisi ya Tanzania ilivyo kuwa kuna watu wa rangi tofauti, kuna watu wa dini tofauti, na kuna watu wa makabila tofauti na wote ni Wanaadamu. Sababu kubwa ya kuchanganua huko ni kwasababu baadhi ya nchi nyingi zilizo kosa maendeleo au zilizopo kwenye maendeleo barani Afrika na baadhi ya mabara mengine, vitu hivi vya ukabila, udini na rangi viliwapelekea au vinawapelekea au hata naweza kusema vinaweza kuwapelekea kwenye machafuko kama nilivyosema hapo awali kuwa hata na mifano hai tunayo na tumeiona katika uhai wetu. Lakini Tanzania tumebarikiwa na amani na utulivu sote tunaishi pamoja na watu wa rangi tofauti, dini tofauti, na watu wa makabila na itikadi tofauti, hii ni neema ambayo pengine hata nchi nyingine wangetamani kuwa nayo lakini hawana na hata kama walikuwa nayo ni vigumu na itachukua muda kuipata tena neema kama hii. Neema hii ya Amani siyo kuwa sisi ni mashujaa sana wa kulinda amani ingawa tunajitahidi qadri tuwezavyo, neema hii siyo kuwa sisi ni waadilifu sana wa kulinda utulivu ingawa tunajitahidi qadri tuwezavyo, na neema hii siyo kuwa sisi ni kuwa tumesalimika sana kwa uhodari wetu, La! Sivyo hivyo, hii ni zawadi tu, kwa Mungu ambayo ametutunuku kutokana na misingi iliyowekwa katika nchi hii na wazee wetu na sisi (nakusudia wananchi wote bila ya itikadi yoyote) ni kama warithi wa amana hii ya Amani, Utulivu na Usalama wa nchi yetu hii tunapaswa kuitunza na kuilinda kutokana na misingi ile ile. Tanzania bara na visiwani tumeshapita huko kwenye machafuko na wazee wetu they have paid the price, enough is enough, damu zimemwagika na chuki za kijamii zimeshapitwa na wakati katika karne hizi za kimaendeleo katika nchi zilizobahatika kuwa na usalama, utulivu na amani, ingawa kwikwi za moshi zinaweza kujitokeza za hapa na pale, na leo na kesho, na moto ukazimwa mara moja na kusahaulika kuliko kuupalilia moto mdogo mdogo kama huo ambao unaweza kusababisha moto mkubwa zaidi ikiwa hautowahiwa kuzimwa mapema. Muhimu ni kuangalia nini tufanye kuilinda hii amani na kuleta maendeleo kwa wananchi wote kuanzia hapa tulipofikia na kwenda mbele. Basi ikiwa amana hii tuliyokuwa nayo mikononi mwetu tukaichezea kwa kuona kuwa tupo salama tu, na tupo na amani tu kwa lolote lile basi kama nilivyosema mifano hai ipo haina hata haja ya kutajwa ambayo imetokea katika uhai wetu katika nchi mbalimbali za jirani za Afrika na nje ya Afrika na tunaomba tusifikie huko. Kwahivyo ni muhimu tumshukuru Mwenyezi Mungu aendelee kutupa Amani katika nchi yetu na njia mojawapo ya kuishukuru amana ya urithi huu wa amani yetu ni kwa kuilinda sisi wenyewe kwani amana ni ya kwetu sote viongozi na wananchi.

Kwa kukamilisha maana yangu kama nilivyosema awali kwanini nimetumia neno “Mwanadamu” badala ya neno “Mwananchi” katika kuleta maendeleo ya Watanzania wote wa bara na visiwani ni kuwa Mwenyezi Mungu katuneemesha wote viumbe vyake kama anavyosema mwenyewe kwenye Qur’an tukufu katika Suratul Israa aya ya 70 anasema:

وَلَقَدْ كَرَّمْنَا بَنِي آدَمَ وَحَمَلْنَاهُمْ فِي الْبَرِّ وَالْبَحْرِ وَرَزَقْنَاهُم مِّنَ الطَّيِّبَاتِ وَفَضَّلْنَاهُمْ عَلَىٰ كَثِيرٍ مِّمَّنْ خَلَقْنَا تَفْضِيلًا

(Na hakika tumewatukuza wanaadamu, na tumewapa vya kupanda nchi kavu na baharini, na tumewaruzuku vitu vizuri vizuri, na tumewafadhilisha kwa fadhila kubwa kuliko wengi miongoni mwa tulio waumba)

Allah kawataja Wanadamu wote hapa, hakuweka jinsia wala hakuweka rangi, dini wala kabila, na ikiwa neema na fadhila hizi tulizopewa na mwenyewe Mwenyezi Mungu tusizishukuru na kuzitukuza, basi sote tunajua nini natija yake. Ikiwa Tanzania italeta maisha mazuri kwa wananchi wake kwa Watanzania wote wa bara na visiwani nchi yetu itazidi kunawiri, na utulivu na amani utaendelea kudumu. Kwani Mwanadamu neema na fadhila alizokupa wewe Mwenyezi Mungu sababu ni kuwa uwe mfadhili na mwenye kutoa ili kuwaneemesha wanaadamu wenzako. Hakuna kitu kinachonikera kama kusikia baadhi ya watu wachache katika viongozi na baadhi ya watu wachache katika jamii eti kuwa sisi kwasababu tuna hichi na kile basi hatutaki kuwapa wenzetu hiki na kile, ni kichefuchefu! hasa ukiangalia mtu huyo huyo ndiyo anayetetea haki za wanaadamu wenzake, na ukiangalia Tanzania hivi sasa yote moja na tumeunganisha undugu wetu katika pembe zote nne katika taifa hili adhim.

Ndugu zangu wapendwa, khiyari ni yetu tuijenge nchi yetu miaka mitano na miaka kumi ijayo kama zilivyo nchi nyingine za nje zilivyoendelea, au tuivunje nchi yetu katika karne za utandawazi ni karne ambazo mara tu nchi zinapochafuka kisiasa huchukua si chini ya miaka 20 na nyingine huweza kuchukuwa hata miaka 50 (nusu karne) kuijenga tena nchi iliyochafuka, inategemea na kitu gani kilichoipelekea nchi hiyo kufikia hayo machafuko kutokana na wepesi wake au uzito wake wa machafuko hayo na mazito zaidi ni udini na ukabila uliochanganyika na siasa au uliochanganyika ndani ya siasa. Ukiangalia miaka yote hii iliyopita nchi yetu ipo katika amani na utulivu tangu, ila katika kipindi cha mvutano wa kisiasa tu! Na hapa isifikiriwe vibaya, Siasa siku zote itakuwepo hilo ni wazi na tunalijua na wanasiasa wana majukumu makubwa juu ya usalama na amani ya watu wao ili watu wao waweze kufanya ibada zao kwa utulivu, kuendesha mambo yao ya kifamilia na kijamii kwa utulivu na kuendesha mambo yao ya kimaendeleo ya maisha yao kwa utulivu. Lakini vilevile ingawa viongozi wana majukumu hayo, wananchi nao wana majukumu kwa wananchi wenzao kuwaletea usalama, amani na utulivu ili kuepukana na umwagaji wa damu kama ishara zote tarajiwa sasa zishaanza kujitokeza na wewe kama ni mwananchi una majukumu na wananchi wenzako kama Qur’an tukufu inavyotuambia katika Suratul Maaida aya ya 32:

مِنْ أَجْلِ ذَٰلِكَ كَتَبْنَا عَلَىٰ بَنِي إِسْرَائِيلَ أَنَّهُ مَن قَتَلَ نَفْسًا بِغَيْرِ نَفْسٍ أَوْ فَسَادٍ فِي الْأَرْضِ فَكَأَنَّمَا قَتَلَ النَّاسَ جَمِيعًا وَمَنْ أَحْيَاهَا فَكَأَنَّمَا أَحْيَا النَّاسَ جَمِيعًا ۚ وَلَقَدْ جَاءَتْهُمْ رُسُلُنَا بِالْبَيِّنَاتِ ثُمَّ إِنَّ كَثِيرًا مِّنْهُم بَعْدَ ذَٰلِكَ فِي الْأَرْضِ لَمُسْرِفُونَ

(…aliyemuuwa mtu bila ya yeye kuuwa, au kufanya uchafuzi katika nchi, basi ni kama amewauwa watu wote…)

Na Mwenyezi Mungu atulinde na hilo. Amin.

Nawapa hongera kubwa kwa ndugu zangu na vijana wote wa Zanzibar wanaoishi visiwani na bara na wanaoishi ndani na nje ya nchi bila ya kuangalia rangi zao, dini zao au kabila lao kwa kuwa werevu na kuwa na subra tangu uchaguzi kwisha kwa kuendeleza amani, utulivu na usalama kwa watu wao. Natoa ushauri wangu kuwa kwa lolote lile lililo shawishi na kuleta subra kwenu katika kipindi hichi kilichopita kwa kuendeleza amani, utulivu na usalama wa nchi na kwa wananchi wenu na ndugu zenu wote, basi mjue ndiyo hilo hilo litakaloleta shawishi litakaloleta machafuko ya amani, utulivu na usalama wa nchi na kwa wananchi wote, tuweni makini!

MWANZO WA MWISHO

Najua uamuzi wa kisiasa mara nyingine unaweza kuwa mgumu na hasa pale dunia nzima inapowaangalia msimamo wenu ni nini? Tumeona katika makundi matatu niliyoyazungumzia hapo juu baada ya mazungumzo marefu na mpaka hivi sasa hali halisi ilipofikia Zanzibar joto la tanuru linaanza kuwa kubwa (Allah awahifadhi, na tusifike pabaya) Amin. Na ukiangalia pande zote mbili kila mmoja anasema yeye upande wake ndiyo halali na kwa kukubali la upande mwingine ni kama kuhalalisha haramu. Ningependa kutoa nasaha yangu kuwa hivyo sivyo kutokana na hali halisi ilipofikia Zanzibar ikiwa halali na haramu hiyo iliyokusudiwa ni kidini, basi dini yetu ya Kiislam ni dini nyepesi sana na isiyokalfisha na ina suluhisho la kila hali na kila jambo. Pale hali inapofika kuwa hakuna budi na hakuna suluhu na mambo yote yamejifunga, basi ikiwa chama kimoja chochote kile ikiwa kitakuwa mahiri na kuwa shujaa na kuwa na subra na kwa kuliangalia hili jambo kwa mapana yake na kwa marefu yake na madhara ya matokeo yake kutokana na maamuzi yake aidha yake yeye kiongozi binafsi au kwa wafuasi wake ili kuiokoa nchi yake na watu wake kuingia katika kiza kinene cha moto unaopaliliwa, basi hapa inatakiwa ipite Hikma na kulihalalisha jambo linaloonekana kuwa lisilofaa la chama kimoja cha kisiasa kwa chama kingine chochote kile si dhambi ili kuokoa maisha ya Waislam na Wanaadam kwa ujumla na si haramu (muhimu tu hujamshirikisha Allah katika hilo) kama anavyosema mwenyewe Mwenyezi Mungu kwenye Qur’an yake tukufu katika suratul Baqara aya ya 173:

إِنَّمَا حَرَّمَ عَلَيْكُمُ الْمَيْتَةَ وَالدَّمَ وَلَحْمَ الْخِنزِيرِ وَمَا أُهِلَّ بِهِ لِغَيْرِ اللَّـهِ ۖ فَمَنِ اضْطُرَّ غَيْرَ بَاغٍ وَلَا عَادٍ فَلَا إِثْمَ عَلَيْهِ ۚ إِنَّ اللَّـهَ غَفُورٌ رَّحِيمٌ

(…Lakini aliye fikiwa na dharura bila ya kutamani wala kupita kiasi, yeye hana dhambi. Hakika Mwenyezi Mungu ni mwenye kusamehe, mwenye kurehemu)

Muhimu usimshirikishe Mwenyezi Mungu tu! Lakini pasipo na budi kutokana na hali ilivyo unaruhusiwa na utasamehewa, hakika yeye Allah ni mwingi wa kusamehe. Muhimu ni kuwa na subra na Imani ya chama chako bado unayo moyoni na imani ya sera za chama chako zipo palepale moyoni mwako basi Mwenyezi Mungu hukuletea maghfira kama unahisi ulilofanya si sawa lakini kwasababu ya nia nzuri ya watu wako na nchi yako, na sote tunajua faida za maghfira ni Rizq, Ustawi wa watoto na jamii, Barka na mengineyo mengi. Mifano ya mwanadamu anayotakiwa awe na subra na kuhusiana mema katika mambo mazito ya Zama au ya Nyakati kama hizi, mifano hiyo ni kama anavyoielezea Sheikh Abdullah Saleh Al-Farsy (Allah amghufirie madhambi yake na ampe Jannat Firdous) katika maelezo ya tafsiri ya Kiswahili ya Suratul A’sr katika Qur’an tukufu, anaelezea kwa kusema, “Subira ni namna nne: (a) Kustahamili katika kufanya mambo mema ambayo ni mazito kwa mtu kudumu nayo, na (b) Kustahamili katika kuacha mambo maovu ambayo ni mazito kwake kuyawacha, na (c) Kustahamiliana na viumbe wenziwe, awachukulie mabaya yao wala asiwafanyie mabaya yake, na (d) Kustahamili misukosuko ya ulimwengu.” Hivi ndivyo Sheikh Abdullah Saleh Al-Farsy alivyoielezea “Subra”. Na sote tunajua hasara za kutokuwa na subra na jambo hasara zake ni kubwa. Lakini nina Imani na viongozi wetu wa bara na visiwani na ndugu zangu vijana werevu wa bara na visiwani wataliangalia hili kwani kulinganiana haki na subra ni hutokana na vikao vyenu, mikutano yenu mnapokutana na kwenye mabaraza yenu ili matokeo yawe ni ya kuleta maendeleo tarajiwa Zanzibar na Tanzania yote kwa ujumla. Wallahu a’alam.

Huu ni mchango wangu tu katika mkwamo wa kisiasa wa Zanzibar hapa lilipofikia nikiwa kama ndugu yenu na si lazima mchango huu ufuatwe lakini ni rai au ushauri ambao nami nimejitolea kuuweka mezani na samahani kama nimekosea. Nawatakia kila kheri. Amin.

 

Ndugu yenu,

 

Saleh Jaber

24/01/2016