MPANGO WA MTAA MMOJA KUWA BAA JIJINI DAR ES SALAAM

KIONGOZI MCHAPAKAZI

Tukiwa katika gurupu la whatsapp na wanagurupu katika kuburudishana, kuelimishana na kupatiana habari mbalimbali, ghafla hivi iliingia habari ya mmoja wa viongozi wachapa kazi iliyoonesha jinsi ya kiongozi huyo anavyopambana na uzembe wa kazi unaozorotesha maendeleo ya kasi kwa wananchi, habari hiyo iliingia kwenye gurupu kwa njia ya picha zikiambatana na maelezo yake na baadae kufuatiwa na video clip ya habari ya tukio hilo hilo ikiambatana na maelezo yake jinsi mheshimiwa huyo anavyopambana na uzembe kazini. Habari hiyo ilikuwa inahusu mkutano uliopangwa mwishoni mwezi Novemba mwaka jana (2015) baina ya wakazi, maafisa ardhi na aliyekuwa mkuu wa wilaya ya Kinondoni, kwa kutatua na kutafuta ufumbuzi wa mgogoro wa ardhi baina ya Wanashamba na Wakazi wa wilaya ya Kinondoni jijini Dar es Salaam. Kiongozi huyo siyo mwingine ila ni Mheshimiwa Paul Makonda, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam.

Baada ya habari hiyo kutuwa kwenye gurupu mada hiyo ilianza kuchangiwa kwa maoni mbalimbali ambayo maoni hayo yalikuwa na mchango wenye nia nzuri juu ya suala zima la mada hiyo kwa pande zote za waliohusishwa ambao wametajwa hapo juu ambao waliohusiana na mkutano wa mgogoro huo. Mjadala ulikuwa baada ya hatua iliyochukuliwa na mheshimiwa Paul Makonda dhidi ya maafisa ardhi husika, na sababu zilizompelekea aliyekuwa mkuu wa wilaya kuchukua hatua alizozichukua. Katika mchango wangu wa mada hiyo nilichangia kimantiki hatua iliyochukuliwa na aliyekuwa mkuu wa wilaya, na mmoja kati ya wanagurupu wenzangu (jina limehifadhiwa) aliniuliza nalionaje suala hili la hatua iliyochukuliwa na aliyekuwa mkuu wa wilaya, na jibu langu lilikuwa (bila ya kunukuu), hatua hiyo ionekane kama ni ‘disciplinary action’ au ‘adhabu ya utovu wa nidhamu’ kazini, na isionekane vingine. Ingawa kulikuwa kuna mvutano wa kimaoni, niliendelea kuchangia maoni kwa kusema (bila ya kunukuu), kutokana na nchi yetu imeachwa nyuma sana kimaendeleo, inafikia wakati inakubidi uchukue hatua fulani fulani ili tuweze kufikia malengo tarajiwa ya kimaendeleo. Baada ya kusema hayo lilifuatiwa na suali la nyongeza mwanagurupu mwenzangu kuniuliza, je, hatua aliyoichukuwa mheshimiwa ya kuwatia ndani maafisa ardhi ni sawa? Jibu langu lilikuwa (bila ya kunukuu), suala hilo ni bora kamuulize mwenyewe DC (mkuu wa wilaya) lakini hapa tulipo kwa hivi sasa nchi yetu tunahitaji kwenda mwendo wa kasi kufikia malengo tarajiwa, na mchango wa kila Mtanzania kwenye ngazi zote kuanzia shina mpaka kitaifa mchango wake unahitajika kuchangia kwenye kasi hii ya kufikia malengo ya maendeleo tarajiwa kwa faida ya raia wa Tanzania wote na vizazi vijavyo. Hususan ukiangalia mgogoro huo wa wakazi wa wilaya ya Kinondoni ulifungamana na sababu ya watu (Watanzania) kupoteza maisha yao kutokana na mgogoro huo huo! Mada hiyo iliishia hapo kama ninavyokumbuka.

Mara nyingi katika nyakati za kisasa, wakati mwingine habari hutufikia mapema kwa njia ya whatsapp kwa kupitia simu za mikononi kuliko njia za kawaida zilizozoeleka au (conventional means). Mwanzoni mwezi Machi 2016, iliingia habari nyingine mpya ya aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, mchapa kazi mheshimiwa Paul Makonda kwa nia yake nzuri ya mpango wa kuleta maendeleo ya mipango ya wilaya yake ya Kinondoni kwa kuanzisha mtaa maalum utakaokuwa ukihusika na sehemu za starehe ya biashara ya uuzaji wa vinywaji vikali na baridi ijulikanayo kwa jina lingine kama ni baa (bar), na kwa sababu hiyo, imenipelekea kuchukua fursa hii kuandika makala hii kwa ufupi ikiwa kama mchango wangu kifikra.

Sina shaka kuwa nia ya aliyekuwa mkuu wa wilaya ya Kinondoni mheshimiwa Paul Makonda ni nia nzuri baada ya kunukuliwa akisema, “Kinondoni nina mpango wa kutengeneza mtaa mmoja maalum wenye baa tu ili watu wakitaka kwenda kunywa pombe waende mtaa huo bila kubughudhiwa. Nasubiri muda tu ufike kwa sababu haiwezekani kila eneo liwe na baa mpaka nyuma ya misikiti na nyuma ya makanisa,” Kutokana na nukuu hiyo, inaonesha wazi kuwa mheshimiwa Paul Makonda ameliona suala hili kuwa bughudha zipo pande mbili, bughudha kwa watu wanaotaka kwenda kwenye pombe na bughudha kwa sehemu za ibada.

Huu ni mtazamo mzuri wa uongozi, lakini kabla ya kuanza mipango ya mpango huu na kama mpango wake ukiwa umeshaanza basi naomba kutoa mchango wangu mheshimiwa Paul Makonda na serikali husika kuliangalia hili suala kwa kina kabla ya kuingia kwenye mpango huu kama ifuatavyo.

 

UTAFITI WA MIPANGO MJI

Wakati leseni zilivyokuwa zinatolewa na mpaka hivi sasa na serikali husika kwa sehemu za starehe za biashara ya uuzaji wa vinywaji vikali na baridi ijulikanayo kwa jina lingine kama ni baa, tukumbuke kuwa serikali haikuwapa watu hawa leseni kwa mazingatio ya maeneo yao bali ni kwa kutoa leseni kwa mazingatio kuwa waomba leseni ni kama wafanyabiashara. Nia ya wafanyabiashara hawa ni ile dhana ya kupata mapato kwa kutumia njia hiyo wanayoiona kwao ndiyo njia ya kuwasukuma kimaisha na kuwafaidisha katika maendeleo ya maisha yao binafsi, na kwa dhana ya kuwanufaisha watumiaji ulevi kwa dhana ya watumiaji ulevi kunufaika kwa njia moja au nyingine na pengine sababu hizo zimepelekea mfanyabiashara huyo kuichukulia biashara hiyo kuiona kama ni biashara nyingine kimapato.

Sababu kubwa ya kuyasema niliyoyasema hapo juu, ni kuwa wakati serikali inatoa leseni hizi serikali haikufanya utafiti wa sehemu za wafanyabiashara hao pale wanapoenda kufanyia biashara hizo, kwa hiyo serikali ilikuwa inatoa leseni ya biashara tu bila ya kuingiza pua na mguu wake na bila ya kufanyia utafiti wa kimazingira wa maeneo hayo ya starehe. Sasa basi, ikiwa sasa serikali itaamua kuwatengezea mtaa mmoja wa baa ili wafanyabiashara wa starehe hizo waondoke sehemu walizo kuwepo hivi sasa, itakuwa serikali imeshaingiza mguu wake kwenye jambo hili na itabidi lijikite kwenye kufanya utafiti wa kina kwenye mambo yafuatayo.

Sehemu zitakazohamwa na wafanyabiashara hao ambao wengine pengine wanakodi au wanamiliki sehemu hizo, zitafanyiwa matumizi gani mubadala na wenye kumiliki sehemu hizo?

Sehemu mpya itakayohamiwa itakuwa na umbali gani kutoka kwenye misikiti, makanisa na wakazi wa maeneo hayo kwa wafanyabiashara za sehemu za starehe wenye vipaza sauti vya nje vinavyosikika kutoka mbali?

Sehemu mpya itakayohamiwa itakuwa na umbali gani kutoka kwenye misikiti, makanisa na wakazi wa maeneo hayo kwa wafanyabiashara za sehemu za starehe wenye vipaza sauti vya ndani?

Serikali itachukua hatua gani na ina mipango gani ya kuwawekea usalama watakaoenda kwenye maeneo hayo kwa wakati wote maeneo hayo yanapokuwa wazi, ili wanaoenda kwa ajili ya starehe hizo wafanye starehe zao kwa usalama na usalama wa jamii ziliyopo karibu na sehemu hizo za starehe?

Serikali itachukua hatua gani na ina mipango gani ya kuwawekea usalama wananchi na wageni watakaoenda kwenye maeneo hayo kuhakikisha kuwa ikitokea madhara yoyote madogo na makubwa yakiwa kama ni matokeo yaliyotokana na sehemu hizo za starehe, kwa mfano, kuwa na Asafu au Ambulensi wakati wote iwe hapo (stand-by) ili yakitokea maafa yoyote yale iweze kusaidia wananchi na wageni kufikishwa hospitali mara moja, na angalau gari moja au mbili za Polisi kuwepo pande zote za mtaa huo, inategemea na urefu na ukubwa wa mtaa huo au sehemu hiyo?

Serikali iangalie mara tu itakapoamua kutia mguu wake kwenye suala hili, imejipanga kivipi kifedha katika utoaji huduma za kulinda afya ya mwananchi atakayeathirika kiafya kwa ulevi. Hatuwezi kusema tumlinde mwananchi kwenye uhalifu tu na tudharau sehemu zingine muhimu kama afya yake mwananchi. Na hapa isieleweke vibaya kwa wafanyabiashara wenye dhana ya kujipatia mapato ya kimaisha kwenye sehemu hizi za starehe, lakini nina msemo wangu usemao ukitunzacho ndicho kikufaacho

Yote hayo niliyoyataja hapo juu ni mambo ambayo ya kuzingatiwa katika mpango huu na kufanyia utafiti wa sehemu za starehe tarajiwa, athari za ulevi katika uchumi wa serikali, utafiti wa kuwawekea mazingira mazuri kwa wanaokwenda sehemu hizo za starehe na mazingira mazuri kwa wale wakazi wanaoishi karibu na sehemu hizo za starehe kama ilivyo nia iliyokusudiwa. Serikali ifanye utafiti wa kina vipi inaweza kubeba suala hili kwa ujumla kabla ya utekelezaji, na itabidi serikali itekeleze hayo kwa manufaa ya wananchi kwasababu sasa imeamua kutia mguu wake kwenye jambo hili na si kama ilivyokuwa hapo awali kwa kutoa leseni tu.

 

ATHARI ZA ULEVI

Pengine sote tunaweza kuwa tunajuwa kwa mwenye kutumia ulevi nini athari zake kiafya, kikazi, athari za umaskini, kifamilia na kijamii, lakini vilevile tuangalie athari zake kwa serikali kiuchumi.

 

KIAFYA

Ulevi, mbali na uvutaji wa sigara, shisha, bangi na vilevi vingine, ulevi ni moja ya sababu kubwa ya magonjwa makubwa ambayo mwanadamu huwa na nafasi ndogo sana ya kupona katika maisha yake na matokeo yake ni kupoteza maisha yake na kuacha familia yake na watu wake awapendao. Magonjwa makuu ambayo mpaka sasa yajulikanayo kiulimwengu ni Ugonjwa wa moyo (Heart disease), Ugonjwa wa kiharusi (Stroke), Ugonjwa wa shinikizo la damu (Blood pressure), Ugonjwa wa saratani (Cancer), Ugonjwa wa maini (Liver disease), na magonjwa mengineyo ambayo bado hayajajulikana.

Mwenye kunywa ulevi hujiongezea nafasi ya kupata shinikizo la damu kwa mara nne zaidi kuliko mtu asiyekunywa ulevi, kiharusi kwa mara mbili zaidi, saratani kwa mara mbiili zaidi, maini kwa mara kumi-na-tatu zaidi. Vilevile, mwenye kunywa ulevi hujipandikizia sumu kwenye ubongo na kwenye mwili na hupelekea ubongo na mwili wake kubadilika kikemia na kusababisha mwenye kutumia ulevi kutokuacha kutumia ulevi na mpaka kilevi hicho kufikia kiwango cha kuwa kilevi-tegemezi ambacho mnywaji hushindwa tena kuacha ulevi kwasababu ya mabadiliko hayo ya kikemia ndani ya ubongo na mwili wake.

Kwa wakati wowote ule, madhara haya yanawapata wanaume na wanawake kwa ujumla kwa viwango vyao. Moja ya madhara kwa wanaume mbali na ya hapo juu ni kusababisha kutosimika katika ngono, na kwa wanawake madhara yake huzidi hasa wakiwepo kwenye hali ya mimba, ulevi huuwa kiumbe au kizazi kilichopo tumboni kwa njia mbalimbali ikiwemo kuharibika kwa mimba, kusababisha mtoto kuzaliwa akiwa na uzito mdogo, na kusababisha maradhi mengine ambayo mtoto anakuwa nayo baada ya kuzaliwa ikiwa kama kizazi hicho hakijafia tumboni kwa madhara ya matumizi ya ulevi. Vilevile, madhara hayo hupelekea mtoto kuwa na maisha siyo ya kawaida kama ya watoto wenzie na matokeo yake hupelekea wazazi kuwa na majukumu makubwa ya kumuangalia mtoto huyo kwasababu hali yake inakuwa siyo sawa na watoto wengine wa kawaida. Nimeweka kiungo kifuatacho kwa kusoma kiufupi tu madhara ya magonjwa ya watoto yanayosababishwa na ulevi kwa kina mama kama mfano ugonjwa wa FAS (Fetal Alcohol Syndrome) http://kidshealth.org/en/parents/fas.html

 

KIKAZI

Ulevi una athari kubwa sana katika sehemu za kazi kwa Mfanyakazi, lakini na athari za Muajiri ni kubwa sana na zaidi kama utaangalia upeo na upana wa athari zake. Mifano ya athari hizo kwa mfanyakazi ni mfanyakazi kutokuwa na fahamu yakini anapokuwa kazini na hupelekea kuduwaa duwaa na mara nyingine kucheka cheka ovyo au kuongea vitu ambavyo wenziye hawamfahamu nini anaongea. Na mifano ya athari za muajiri ni kama pale mfanyakazi kutokuwepo au kutokuhudhuria kazini wakati wa kazi pengine kutokana na mfanyakazi huyo kile kilevi bado hakijamtoka mwilini na kushindwa kuwakilisha kazi yake kazini, au kutokuhudhuria kazini kwasababu ya kupata ajali ndogo au kubwa iliyotokana na kutumia ulevi, pia husababisha tija ya kazi (productivity) kazini kupungua na kusababisha baadhi ya kazi za muajiri kucheleweshwa au kazi kusimama kabisa na kupelekea muajiri kupata gharama zisizo na faida na vilevile kupelekea kuathiri mifuko ya jamii kwa ujumla kama vile NSSF, PPF na LAPF. Hasa ukizingatia serikali ina dira ya kuifanya nchi yetu iwe nchi ya viwanda na kuwatoa wananchi kwenye umaskini na kufikia kiwango cha kati kimaisha, kwahivyo bila ya kudhibiti ulevi kwenye kila pembe za kijamii kimpango bila ya kuathiri wenye dhana ya uchumi wa ulevi ulioruhusiwa kiserikali, nchi yetu itashindwa kufikia malengo yake tarajiwa kwasababu jamii ndiyo watu na watu ndiyo wanaojenga nchi.

 

UMASKINI

Mfanyakazi anaposhindwa kutimiza wajibu wake kazini kwenye mahudhurio ya kazi, au anaposhindwa kutimiza wajibu wa tija ya kazi (productivity), au anaposhindwa kuwakilisha kazi aliyopewa kwa sababu za kutokana na ulevi, mfanyakazi humpelekea mwisho kuachishwa kazi na muajiri na kuachishwa kazi inaweza kumfanya mfanyakazi huyo aliyekosa kazi akazidisha ulevi wa bila ya kuwa na mapato na kusababisha familia yake kukosa matumizi ya msingi na matumizi endelevu ya kimaisha ya ndani ya familia na hupelekea kuathirika kwa familia na jamii kwa ujumla. Aidha, mlevi awe na kazi au awe hana kazi, awe na familia au awe hana familia, athari za kifamilia na za kijamii kwa ujumla ni sawa.

 

KIFAMILIA

Nyuzi za mkeka wa taifa ni Familia. Kama vile mkeka unavyoachia pale nyuzi zinapoachana kwasababu ya kasoro fulani fulani, basi ni hivyo hivyo ulevi una athari kubwa sana katika familia. Kilevi au ulevi wa aina yoyote ule unaweza ukamfanya mzazi kumtatiza na kumpunguzia uwezo wa kuiangalia familia yake na kusababisha athari kubwa kwa watoto kisaikolojia, na mtazamo wa watoto wenzao wanavyowaangalia katika jamii unakuwa ni vingine na kusababisha watoto kutokuwa na furaha na nafasi nzuri kwa watoto wenzao kwenye jamii kwa ujumla na kupelekea kuwepo kwa huzuni, hofu na wasiwasi wa maisha ya baadae kwa watoto hao na wanafamilia wengine wa karibu yao.

Ukiangalia athari nyingine ya kifamilia ni pale mzazi anapoamua kwenda kulewa nje kwa dhana ya kuwa nyumbani si sehemu ya kulewea, hii husababisha mzazi kuwa mbali na familia yake kwa muda mrefu. Athari ya gharama za matibabu ya ulevi ni kubwa ambazo familia nzima husababika kuathirika nazo kutokana na ulevi wa mzazi huyo. Vilevile gharama za kununua vilevi huchangia kupunguza matumizi muhimu ya msingi na matumizi endelevu ya nyumbani kwasababu mshahara unakuwa hautoshelezi kukidhi haja za matumizi ya ulevi sambamba na matumizi ya nyumbani kwa wakati mmoja na wakati mwingine hufikia mzazi au mlezi huyo mpaka kutumia zaidi kwenye ulevi kuliko kwenye mahitaji ya kifamilia, na mpaka mara nyingine hupelekea kuathiri hata wanafamilia wengine wa karibu kusababisha kuiendesha familia hiyo ambayo kwa upande mwingine unaweza kusema siyo wajibu wao kutokana na mantiki hiyo. Kwahivyo, ulevi una athari kubwa katika familia.

 

KIJAMII

Jamii ndiyo kioo cha taifa. Kama nilivyosema hapo awali, kwa maana nyingine ya kuwa mtu ndiye anayejenga familia, na familia ndiyo hujenga jamii na jamii ndiyo hujenga taifa. Bila ya serikali kushuka chini katika ngazi ya jamii kwa kuziangalia jamii (kishina, kitawi, kikata, kiwilaya au kimkoa) kwa kuziangalia bila ya kuangalia tofauti zao za kidini au za kikabila au za kiitikadi yoyote ile, basi taifa litakuwa katika hasara kubwa. Naomba radhi nitatoka nje ya mada hapa kidogo.

Serikali ina majukumu ya kuangalia maslahi ya raia wake popote pale walipo iwe ndani ya nchi au nje ya nchi bila ya kuangalia dini zao au kabila zao au itikadi zao. Kutokuwaangalia na kutokuwatunza raia kwa kuwafaidisha wote kwa ujumla bila ya kuangalia tofauti zao katika mambo ya Elimu, Afya na Uchumi hususan waliopo nchini Tanzania ili wawe wazalendo bora wenye kujitawala na wawe wenye kuiendesha nchi yao kwa pamoja kama mkeka mmoja wa taifa ili kufikia dira yetu ya taifa tunayoitaka ifikie malengo yake, basi kutokufanya hivyo tutakuja kutawaliwa na kuendeshwa na watu wa kutoka nje ya nchi.

Unavuna kile ulichokipanda, na kama mbegu zinazopandwa au zilizopandwa awali zimezaliana na magugu, basi tuyakate magugu na tupandikize mbegu mpya ili nchi yetu ipendeze iwe na umoja na iwe nchi yenye kujenga ari ya uzalendo kwa kila raia ili tufikie malengo ya huko tunapoelekea. Nakumbuka nilipokuwa nasoma shule ya vidudu, Independence Nursery School, jijini Dar es Salaam iliyopo mtaa wa Independence Avenue, (sasa unaitwa mtaa wa Samora Avenue), tulikuwa wote tukiimba, “Maua mazuri yapendeza, ukiyatazama utachekelea, hakuna umoja usiopendeza…”

Turudi kwenye mada yetu, jamii ndiyo kioo cha taifa na utakapoilinda jamii katika njia zote za kimsingi ndiyo taifa litaimarika na litashamiri. Nimefurahi kuona mheshimiwa Paul Makonda kwa kuchukua hatua hii ya kufikiria jamii ya wakazi na wafanyabiashara wa maeneo ya Kinondoni na sehemu za ibada (misikiti na makanisa) kwa nia nzuri aliyonayo na madamu hivi sasa kafikia wadhfa wa Mkuu wa Mkoa nataraji hatua hii sasa ataiangalia kwa upeo mkubwa zaidi wa kuondoa bughudha hizi kwa wilaya zote za jiji la Dar es Salaam na kuwa ni mfano mkubwa wa kuigwa kwa mikoa mingine nchini mwetu kwa manufaa ya watu wote, kwani Kizuri chenye tija, ndicho cha kuigwa.

 

ATHARI YA ULEVI KATIKA SERIKALI KIUCHUMI

Serikali zote duniani zinaathirika kwa njia moja au nyingine kwa gharama zinazopotezea kwenye kusimamia athari za ulevi. Kwasababu sina takwimu za haraka haraka za athari za ulevi nchini Tanzania, ningependa kuchukulia mfano wa takwimu za nchi nyingine duniani mfano nchi za ulaya, asia au marekani, kwani watu wa ulaya, asia au marekani kimaumbile hawana tofauti na watu wa afrika kwa hivyo matokeo ya madhara kwa wote ni sawa.

Serikali hupata gharama za moja kwa moja na gharama zingine zisizo za moja kwa moja katika kusimamia athari za ulevi. Mfano wa gharama za moja kwa moja ni serikali kubeba gharama za matangazo ya athari za ulevi kwa kuwaonya wananchi (alcohol awareness), na vifaa na vyombo vyote husika vinavyohusu kuwasilisha ujumbe wa athari za ulevi. Mfano wa gharama zisizo za moja kwa moja katika kusimamia athari ya ulevi ambazo serikali zinabeba ni pale mtu anapozidiwa kutokana na ulevi wake mwenyewe inabidi itoke asafu au ambulensi ya kumchukua na kumhudumia, au pale panapotokea vurugu au fujo zilizosababishwa na ulevi inabidi vyombo vya serikali viwasili kutuliza vurugu au fujo. Vilevile kama nilivyosema huko nyuma, pale mfanyakazi au wafanyakazi wasipohudhuria kazini au kushindwa kuwasilisha kazi kutokana na ulevi, serikali inaathirika kwenye mapato na kwenye mifuko ya jamii kama NSSF, PPF na LAPF na kusababisha kurudisha nyuma maendeleo na uchumi wa taifa.

Katika baadhi ya nchi zilizoendelea, hasa tukichukulia kwenye sekta ya viwanda (Industrialised countries), majumuisho ya gharama zinazotumika katika kusimamia athari za ulevi katika uchumi wa taifa au GDP (Gross Domestic Product) ni kubwa sana, kwa mfano Canada inagharamika 1.1% katika uchumi wake wa taifa, Italy 5.6% katika uchumi wake wa taifa na nchi nyingine nyingi tu. Nchini United Kingdom, gharama za huduma zinazotolewa kutokana na athari za ulevi ambazo huduma hizo zinatolewa moja kwa moja na huduma ya taifa ya afya (NHS) mahospitalini ni £3bn (Pauni bilioni tatu za Kiingereza) kwa mwaka kwenye mahospitali tu, na inakadiriwa kutokana na utafiti wa wanaharakati kuwa gharama zinazoathiri uchumi wa taifa kwa mwaka kutokana na sababu za ulevi kama mfano wafanyakazi kutohudhuria kazini, walioachishwa kazi kwasababu ya ulevi, vifo vilivyosababishwa na ulevi, ajali za barabarani na uhalifu zinafikia £6bn jumla (Pauni bilioni sita za Kiingereza) ambazo ni takriban na shilingi za Tanzania 19,216,029,782,108.90 (Trilioni kumi na tisa nukta mbili za shilingi ya Tanzania) kwa mwaka, kutokana na chenji ya XE currency converter ya leo tarehe 28 May 2016.

Juzi nilikuwa napitia pitia mitandaoni, nikaona jinsi gani serikali ya Oman imechukuwa hatua kuondoa kero za wananchi katika jamii juu ya vilevi, na mfano wake hautofautiani sana na mada tunayoizungumzia kuhusu uhamisho wa sehemu za baa, bonyeza hapa kwa maelezo zaidi.

Juzi hiyo hiyo nikaona jinsi gani serikali ya UK imechukuwa hatua ya kusimamisha uuzwaji wa vilevi tegemezi, bonyeza hapa kwa maelezo zaidi. Ingawa vilevi hivi hatuwezi kufananisha na vilevi vilivyo kwenye mada yetu, lakini baadhi ya athari zake kwa upande mmoja au mwingine zinalingana na nimejaribu kuweka viungo hivi ili tuweze kuona jinsi gani serikali zinachukua hatua mbalimbali za kupunguza madhara kwa wananchi na kupunguza gharama kwa serikali kiuchumi bila ya kuwadhuru wafanyabiashara walioruhusiwa kufanya biashara hiyo kiserikali.

 

MWISHO

Mifano yote hii niliyoitoa hapo juu ni kwa nia nzuri kutokana na mtazamo wangu na ichukuliwe kama ni rai tu ikiwa serikali itaamua kuingiza mguu wake kwenye suala hili katika kutafuta maeneo pekee yatakayowekwa baa kwa wenye dhana ya kufanya biashara hiyo na serikali iangalie athari zote hizi kufanyia utafiti kwa upana zaidi ili pande zote ziwe zenye kunufaika, hususan jamii. Hongera mheshimiwa Paul Makonda kwa juhudi zako na fikra zako za kikazi kwa manufaa ya wakazi wa jiji la Dar es Salaam chini ya rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa, Dokta John Pombe Magufuli, kaza buti kaka!

 

Samahani kama nimekosea popote.

 

Ndugu yenu,

 

Saleh Jaber

28/05/2016

Advertisements