Serikali Ya Mwendo Kasi Ukingoni Mwa Kufikisha Mwaka Mmoja Tangu Kuwemo Madarakani

Ningependa kuchukua fursa hii kumpongeza Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dokta John Pombe Magufuli kwa kazi kubwa anayoifanya kwa kuleta kimbunga cha mabadiliko ambacho hakijawahi kutokea kwenye historia ya Tanzania tangu tupate Uhuru.

Sote tunajua maendeleo ya kila sekta ya nyanja zote za taifa hayaji kwa usiku mmoja kama nilivyosema kwenye makala yangu iliyopita kwa kumaanisha kuwa awamu moja peke yake haiwezi kuleta maendeleo tarajiwa ya kila sekta na kufikia ngazi ya kimataifa, hii huchukuwa muda na subra, lakini Mabadiliko yanaweza kutokea kwenye msimu mmoja au awamu moja kwa maana ya kuwa, inawezekana kwenye awamu moja kutokea mabadiliko ya Mfumo wa kuleta maendeleo ya kila sekta ya nyanja zote za taifa na kuwa kama ndiyo kitako au msingi wa maendeleo wa taifa zima kwa siku za usoni zijazo. Nimetumia neno kimbunga ni kutokana na kasi ya mabadiliko haya ya mfumo wa utendaji kazi unaotokea nchini kwetu hivi sasa kwenye sekta mbalimbali ambayo yanayosaidia kuichonga ile dira ya taifa ya mwaka 2025 na zaidi, kwa kutokomeza umaskini na kuwapa huduma bora za msingi na huduma stahiki kwa raia wa hali ya chini na raia wote kwa ujumla katika taifa letu adhim.

Rais wetu mheshimiwa John Pombe Magufuli ameamua kujikita kuleta maendeleo kwa kuleta Mapinduzi ya Viwanda ambayo mchakamchaka wake unastahili mapongezi kwake na majopo yake, na unastahili mapongezi kwa mawaziri wa sekta zote akiwamo Waziri Mkuu Kassim Majaaliwa kwa kazi kubwa wanayoifanya kwenye kila kona ya nchi na kushuka kwenye ngazi za chini kabisa kuhakikisha kuwa hakuna jiwe linaloachwa bila ya kupinduliwa-pinduliwa kuangaliwa wapi linaweza kuchongwa na wapi lifanyiwe marekebisho ya kwenda sambamba na maendeleo tarajiwa aliyoyadhamiria mheshimiwa rais ya miaka mitano, kumi na zaidi ijayo.

KUHAMA KWA MAKAO MAKUU

Nia ya serikali kuhamisha Makao Makuu yake Dodoma yalianza tangu miaka ya mwanzo ya sabini (1970’s), sote tulikuwa tunatarajia kuhama kwa makao makuu kutatokea ila ilibaki kuwa ni lini itatokea. Na tendo hili linaweza kuwa limewashtua baadhi ya watu likiwa kama ni jambo jipya kwao, lakini mahamisho ya makao makuu ya serikali si jambo geni, baadhi ya nchi za Afrika na nje ya Afrika zimehamisha makao makuu ya serikali zao kutoka mji mmoja kwenda mji mwingine kwasababu mbalimbali. Hongera mheshimiwa rais kwa kuchukuwa hatua ya kijasiri chini ya mwaka mmoja tangu kuanza kwa madaraka ya kuwa rais na kuhamisha makao makuu kwenda Dodoma. Baadhi ya watu wanaweza kuuliza nia na hoja ya kuhamia kwa ghafla na kwa haraka hivyo kwa kipindi cha miezi miwili tu tangu itangazwe nia rasmi ya kuhama kikamilifu kivitendo, lakini tunaamini kuwa kila penye nia pana njia na tunaomba kila la kheri, Mwenyezi Mungu haangalii matendo bali anaangalia nia.

FAIDA ZA KUHAMISHA MAKAO MAKUU

Tendo la serikali kuhamisha makao makuu Dodoma kimatendo, litapunguza gharama za kiutendaji kazi zaidi kuliko kama ilivyokuwa hivi sasa serikali ipo jijini Dar es Salaam lakini bunge lipo Dodoma, hivyo serikali kuhamisha makao makuu yote Dodoma, itasaidia kubana baadhi ya matumizi mengi ya kipesa, kiharakati na kimawasiliano.

Mji wa Dodoma upo katikati ya nchi ambapo ni rahisi wanaharakati, wabunge, mawaziri, wananchi na watendaji wengine wa serikali na wasio wa kiserikali kwa ujumla kufanya harakati zao na kuwasilisha kazi zao bila ya kusafiri mbali kama ilivyo hivi sasa, kwahiyo itakuwa nafuu kwa mtu anayetoka mfano kaskazini, kusini au magharibi mwa nchi kwenda Dodoma kuliko kuja Dar es Salaam, na watendaji kazi wa kiserikali wanaotoka Dodoma kufikia maeneo mengine ya nchi, ni rahisi na ni nafuu kwao kufika haraka miji mingine kutokana na Dodoma kuwa ipo katikati ya nchi yetu ya Tanzania.

Vilevile itasaidia kupunguza msongamano wa watu jijini Dar es Salaam kwa kiasi fulani, na hili ni jambo serikali la kuliangalia kwa siku za usoni kuwa kila mji wa Tanzania uwe na huduma zote za kutosheleza za kiserikali, na kila mji uwe na vivutio vya wananchi kupata kazi katika miji yao bila ya kuhamia mji mwingine eti kwasababu mji au miji yao haina fursa za kutosha. Hii ni kazi ya serikali kujipanga na kuwapelekea fursa hizo wananchi hasa kwa sasa ni wakati muwafaka wa mapinduzi ya viwanda kwa kuvitawanya viwanda kwenye miji mbalimbali (kwa kufuata miundo mbinu ya kisasa) na vilevile kuwashajiisha wananchi kuwa wajasiriamali katika miji yao ili waweze kuishi na kufanya kazi kwenye miji waliyokulia nayo, na hii isichukuliwe vibaya, kwa kuchukua hatua hizi ni bila ya kukiukwa katiba yetu ya nchi ambayo inampa mwananchi uhuru wa kuishi na kufanya kazi popote pale anapotaka kwa kuleta maendeleo yake yeye binafsi na maendeleo ya familia yake na jamii iliyomzunguka.

HASARA ZA KUHAMISHA MAKAO MAKUU BILA YA KUWA MAKINI

Sina shaka kuwa hatua ya rais kuhamishia makao makuu Dodoma ni ya kutimiza ndoto ya serikali ya kuhamia Dodoma tangu nia hiyo ilipotangazwa rasmi miaka ya mwanzo ya sabini (1970’s) na hongera sana kwa hilo na sina shaka kuwa serikali ipo makini kwa kuchukua hatua hiyo.

Pamoja na kutimiza ndoto ya kuhamishia makao makuu Dodoma, serikali isije ikajisahau na kuipa mgongo Chachu iliyotolewa na mpaka hivi sasa inayoendelea kutolewa na jiji la Dar es Salaam kwa kuleta maendeleo ya taifa hili na kufikia hapa lilipo. Dar es Salaam ndiyo mtoto, ndiyo mama, ndiyo baba na ndiyo mlezi, na maendeleo mengi yaliyopatikana katika nchi yetu yametokana na mkono na kinywa cha jiji la Dar es Salaam, kwa maana nyingine Dodoma itakuwa sasa ni bongo la taifa na Dar es Salaam itabaki na itaendelea kuwa ndiyo moyo wa taifa.

Serikali isije ikajisahau moja kwa moja kuacha kuendelea kuleta maendeleo ya jiji la Dar es Salaam na miji mingine kwa kulimbikiza mapato yote sehemu moja na kusahau sehemu nyingine, huku kunaweza kuleta mtikisiko wa kiuchumi nchini. Kwa kusema hivi, ni muhimu serikali iendelee kuleta maendeleo ya kisasa ya miundombinu na maendeleo mengine katika jiji la Dar es Salaam na miji mingine nchini ili kuleta maendeleo tarajiwa kwa wananchi kwa kutegemea ujasiriamali, viwanda na fursa mbalimbali nyinginezo. Kwa kufanya hivi kutasaidia nchi na miji ijitegemee yenyewe kiuchumi bila ya kutegemea sana maliasili za nchi, na hapa kunanipelekea kuzungumzia kuhusu Maliasili na Rasilimali za nchi yetu.

MALIASILI NA RASILIMALI ZA TAIFA

Kama mfano ilivyo nchi za wenzetu, mfano nchi ya Falme za Kiarabu (U.A.E.), ambayo makao makuu yake ni Abu Dhabi, lakini jiji la Dubai ndiyo inayojulikana duniani kote kwasababu imeshinda kwenye kujitegemea kiuchumi yenyewe kijasiriamali na kibiashara bila ya kutegemea sana maliasili za nchi kama mafuta (oil), gesi (gas), na kadhalika.

Sote tunajua sasa Mwenyezi Mungu katubariki na kaleta neema kubwa katika nchi yetu kwa kuwa na utajiri wa maliasili zikiwemo gesi, madini na maliasili nyingine mbalimbali ambazo nyingine zikiendelea kugunduliwa kila siku. Ikiwa tutakuwa tuna ubinafsi, si maanishi ubinafsi wa kujibinafsisha mtu mmoja, hapana, nazungumzia ubinafsi wa kizazi chetu kilichopo sasa hivi kwa kutumia vibaya maliasili hizi na kuanza kuchimba na kuchimbua kila tunapoona maliasili mpya zinapojitokeza na kuanza kuzitumia bila ya kujua kuwa hakuna kitu kisichokuwa na mwisho basi itakuwa tunawadhulumu vizazi vitakavyokuja miaka mia tano (500) na zaidi ijayo kuanzia hivi sasa, kwani wazee wetu wamesema, “Bandubandu humaliza gogo”. Kwa mfano, lazima tujue kuwa kila ujazo wa gesi iliyopo chini ya ardhi hata kama ikiwa ni trilioni ngapi, basi ipo siku itafikia mwisho wake, na maliasili za chini ya ardhi si kama miti ya kusema kuwa utakata mti leo utapanda mwingine kesho, ingekuwa hivyo basi kila nchi duniani ingekuwa na mafuta na gesi ya kutosha bila ya kutegemea mafuta au gesi ya mwenzie, na hata kama kutakuwa na teknolojia ya kutengenezea au kunakili gesi au mafuta, basi haitokuwa yenye kiwango cha asilia na gharama zake zitakuwa kubwa sana na za kupindukia. Si vibaya kuendelea kufanya utafiti wa maliasili na si vibaya kusimama kwa sasa, lakini siyo kila tunapoiona maliasili ya nchi tunaichimba na kuichimbua kwa manufaa ya kizazi cha sasa tu, hivyo itakuwa hatujatenda uadilifu kwa neema na zawadi hii tuliyopewa na Mwenyezi Mungu kwetu sisi na vizazi vyetu vijavyo.

Vilevile rasilimali za taifa, serikali ijitahidi kuzihodhi hizi rasilimali bila ya kuzibinafsisha ili ziweze kukidhi haja zake za kihuduma kwa raia wa Tanzania na huku ikiendelea kutengeneza rasilimali mpya mbalimbali kwa malengo mbalimbali na kuwapa fursa ya wawekezaji kujijengea rasilimali zao wenyewe binafsi zenye kunufaisha raia wa Tanzania; ningependa kusema “ni bora kukodisha kuliko kubinafsisha.” Vilevile hongera kwa kupigia breki mradi wa Chole, Mafia na kuuangalia kwa kina nini mustakbali wake kwa wakazi wa kijiji hicho Kiuchumi, Kiutamaduni na Kihistoria.

Huu ni ushauri wangu na samahani kama nimekosea popote. Tunamuombea Rais wetu John Pombe Magufuli, Mwenyezi Mungu amlinde, amzidishie afya, hikma na utawala bora. Amin.

 

Ndugu yenu,

 

Saleh Jaber

07/08/2016

Advertisements