MHESHIMIWA (IGP) SIMON SIRRO AONGEA NA WAANDISHI WA HABARI, ASEMA WALIOFANYA UHALIFU MKOA WA PWANI WATALIPWA KWA UHALIFU WAO, AWAHAKIKISHIA RAIA WEMA WAPO VIZURI, AWAOMBA USHIRIKIANO WAO

 • Kwa mara ya kwanza, Mkuu wa Jeshi la Polisi Tanzania (IGP), Mheshimiwa Simon Sirro aongea rasmi na waandishi wa habari na kuzungumzia vipaumbele vyake. Amewashukuru waandishi wa habari kwa kutoa ushirikiano mkubwa na vyombo vya dola, na amewaomba waendelee kutoa ushirikiano huo kama kawaida

 • Amshukuru Mwenyezi Mungu na amshukuru sana Mheshimiwa Rais John Pombe Magufuli kwa kumteua kuwa Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini Tanzania (IGP). Amewaelezea waandishi wa habari kwamba nchi yetu ni shwari, ila changamoto iliyojitokeza hivi karibuni ya ukatili unaoendelea ya wahalifu wachache waliojitokeza maeneo ya Mkuranga, Kibiti, Ikwiriri na Rufiji kwa kuwauwa raia wema na kusababisha Mkoa wa Pwani kukosa amani na utulivu

 • Mheshimiwa Sirro amesema, matukio ya mauaji yaliyojitokeza maeneo ya Ikwiriri na Rufiji, Mkoa wa Pwani, ni matukio ambayo lazima yashughulikiwe kwasababu mauaji yaliyotokea wananchi wanataka majibu kwa kuwaadhibisha wahalifu wachache waliofanya ubaya huu; na ubaya wa ukatili walioufanya utalipwa kwa ubaya kwa mujibu wa sheria kutokana na ukatili wao

 • Lingine katika vipaumbele vyake, Mheshimiwa Sirro amewaonya wana bodaboda ambao wanajihusisha na matukio ya uhalifu, wanaopita kwenye taa nyekundu, wasiovaa helmet wakiwa wanaendesha bodaboda zao na kubeba watu zaidi ya inavyotakiwa (mshikaki), amewataka waache mara moja na badala yake watii sheria bila ya shuruti

 • Amegusia kwa wale wanaojihusisha na madawa ya kulevya waachane na kazi hiyo na watafute kazi mbadala ya kujipatia rizki halali

 • Pamoja na changamoto hizo, amewaonya raia wa kawaida wanaojichukulia sheria mkononi kwa kupiga wezi ambao wengine imepelekea mara nyingine mpaka kuuwawa kwa mtu kwasababu tu ya kuiba kuku. Amesisitiza kwamba raia wa kawaida wasijichukulie sheria mkononi na iwapo watafanya hivyo watakuwa wapo makosani, lakini badala yake wafuate mkondo wa sheria

 • Ametoa onyo kali kwenye vyombo vitakatifu kama chombo cha Polisi kwamba kupokea rushwa ni adui wa haki na yeyote atakayechukua rushwa atachukuliwa hatua yeye na mtoa rushwa. Na hivyo, amewaomba Watanzania wasiwashawishi maaskari kupokea rushwa

 • Amekumbushia maagizo ya RPC wa Mkoa wa Pwani baada ya kutoa listi ya watuhumiwa wa uhalifu wanaotafutwa na Polisi kwamba itahitaji ushirikiano wa wananchi wazalendo kuwafichua wahalifu hao kwa kutoa habari za uhakika kwenye vyombo vya dola. Kwa kurejesha shukrani, Polisi itatoa zawadi ya shilingi milioni kumi kwa yule mwenye habari za uhakika za wahalifu hao badala ya milioni tano iliyotangazwa hapo awali

 • Mwisho, Mheshimiwa Sirro amewaomba waandishi wa habari kuendeleza ushirikiano na vyombo vya dola kuhakikisha Watanzania wanaishi kwa amani na utulivu, na amewaombea Waislamu wote mfungo mwema wa mwezi mtukufu wa Ramadhan

WAKAZI WA MKURANGA WALONGA HALI HALISI YA UNYANYASAJI NA KERO KWA WAKAZI WA MKOA WA PWANI

Baadhi ya wakazi wa Mkuranga wahojiwa na kutoa muono wao wa hali halisi inayoendelea Mkoa wa Pwani na kila mmoja wao ameelezea kwamba Polisi wanawanyanyasa na wanawasumbuwa kufanya kazi zao kwa utulivu na kwa hivyo wamekosa amani. Haya ni maneno ya wakazi na raia wema wenyewe ambao hawafanyi uhalifu wowote. Kwa muda gani wamekuwa wakinyanyaswa, haijulikani.

Ushauri wangu kwa Mheshimiwa Rais ni kuliangalia hili suala kwa ukaribu zaidi kwa amani ya watu wa mkoa wa Pwani. Wakazi wazawa wa maeneo hayo wapewe uhuru wao wa kufanya kazi zao kwa utulivu na amani na bila ya kusumbuliwa kwa kuhamishwa hamishwa na mpaka kufikia hali ya kukosa amani na sehemu zao wenyewe.

Kwa hali hiyo iliyojitokeza kwenye hii video ya Global TV (2017), naishauri serikali kwanza isitumie nguvu ya dola na kusababisha hatari kubwa zaidi. Badala yake, Polisi na uongozi wa CCM wa maeneo hayo wawape amani wakazi wa maeneo hayo kwa kuwaacha na maeneo yao ya makazi na sehemu zao za kujitafutia riziki kwa amani na utulivu na kutafuta njia za kuzungumza na wakazi wa mitaa ya hapo na vijiji vya hapo kwa kuwatatulia changamoto zao na kuwawekea mazingira mazuri, bila ya vitisho; na nina imani kubwa na Rais Magufuli kuwa ni rais msikivu na mwenye kuwatakia watu wake umoja, upendo na amani.

Kuna kitu wazungu wanakiita ‘Gentrification’. Gentrification ni neno ambalo asili yake lilifafanuliwa na bibi mmoja nchini Uingereza anaitwa Ruth Glass (1964) alifafanua, Gentrification ni hali ya kuifanya sehemu moja ya hali ya watu wa chini kuigeuza kuwa ni sehemu ya hali ya juu kwa kuwatoa na kuwafukuza watu wa hali ya chini maskini na kuwapa watu matajiri kujenga nyumba za ghali, halafu kuwasukuma watu maskini mbali na maeneo yao waliyozaliwa nayo na waliyokulia nayo na kuwafanya washindwe kuishi maisha ya hapo walipozaliwa. Kwa lugha nyingine ya kigeni (Social cleansing). Hii ni hali ya hatari nchini kwetu.

Nchi yetu ni nchi ya kijamaa na ndiyo misingi aliyotuwekea baba wa taifa Mwalimu Nyerere. Badala ya kuwafukuza watu maeneo yao tulikuwa tunatakiwa wakazi wa maeneo fulani (popote nchini) waachwe kwa amani katika maeneo yao na badala yake kuwaboreshea maeneo yao ili waendelee kutunza utamaduni wao (ambao ni utamaduni wa Kitanzania) na unatakiwa kulindwa kama ilivyo tamaduni zingine nchini mwetu.

Bi Ruth Glass (1964) alisema, kawaida ya Gentrification inapoanza sehemu moja haiishii hapo itaenda sehemu nyingine ya karibu yake inayofuata, halafu itaendelea kuwa hivyo hivyo na hatimaye watu wa hali ya chini wataendelea kuwa na hali ya chini na watu wa hali ya juu wachache ndiyo watakaofaidika na utamaduni wa watu utapotea.

Mheshimiwa Rais Magufuli nampongeza kwa kuonesha mfano wa kusimamia msingi wa nchi yetu ya Kijamaa kama inavyoainishwa kwenye katiba yetu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na katiba ya chama tawala cha CCM, kwa kuonesha mfano hivi karibuni kwa kuwatetea Watanzania wanyonge wa Magomeni Kota kwa kuchukua sehemu yao ambayo ni ya ghali kwa thamani, na badala yake kuwarudishia sehemu hiyo hiyo wale masikini wanyonge kwa thamani ndogo kutokana na uwezo wao wa chini. Huu ndiyo uadilifu wa rais wetu mwema, na ndiyo siasa ya nchi yetu. Vinginevyo, Rais Magufuli asingefanya hivyo, ingekuwa ni Gentrification ya kuwanyanyasa wanyonge na ni kinyume na msimamo wa CCM na ni kinyume na siasa ya nchi yetu. Tanzania inaweza ikafanya maboresho ya sehemu za watu maskini kwa kuwasaidia maskini kwa kuwatoa watu maskini kutoka kwenye umaskini, na si kinyume chake.

Nashauri itumwe tume huru ichunguze kwa kina kama kuna ushawishi wowote wa watu wachache kule wanaotumia vyombo vya dola kujifaidisha kibinafsi badala ya kufaidisha wananchi wanyonge; na kusikiliza kero za hawa wakazi wa Mkuranga, Kibiti na Rufiji, ili waboreshewe maeneo yao na wasiendelee kunyanyaswa na Polisi. Haiihitaji nguvu huko. Siyo bure!

AMANI! AMANI! AMANI!

Samahani kama nimekosea.

Ndugu yenu,

Saleh Jaber

30/05/2017

 

MAREJEO:

Glass, R. (1964). Aspects of Change. 1st ed. London: MacGibbon & Kee Ltd.

TV, G. (2017). Walichokisema Wananchi wa Mkuranga. [Online] YouTube. Available at:

[Accessed 30 May 2017].

SHERIA ZA NDOA ZA UTOTONI NA MIMBA ZA MASHULENI

Ningependa kuandika machache juu ya mada ya mimba inayoitwa mimba ya utotoni na ndoa za utotoni.

Kwanza kabisa, anayechukua mimba huyo hana utoto. Halafu pili, nawapongeza waheshimiwa Salma Kikwete, Mwigulu Nchemba na Ali Kesi (2017) kwa kuweka mguu chini kwa msimamo wao na ni msimamo wa Watanzani wengi wa kutetea mila na utamaduni wa taifa kwa mustakbal wa watoto wetu wote wa kike na wa kiume na kuwa mfano bora katika familia zao, taifa lao na kwa vizazi vijavyo vya taifa letu. Utamaduni ambao misingi yake siyo ya kuonekana kwa baadhi ya watu wachache na mienendo yao, bali ni misingi ya maandishi matakatifu ambayo yamechukua kina kipana katika sehemu kubwa ya maisha ya kila siku ya Watanzania, ambayo yanatokana na utamaduni, mila na desturi, na dini zetu mbili, Uislamu na Ukristo.

Utamaduni wa watu wa Tanzania na dini za watu wa Tanzania haubadilishwi na matangazo ya TV au picha za mitandaoni zenye ajenda za siri za baadhi ya watu wachache ambazo ni kinyume na maadili ya Tanzania. Mara nyingi, miti ya jana ya asili haikatwi, bali mbegu zilizopandwa leo zinaweza kufukuliwa na zikateketezwa kama ni mbovu na kama hazifai. Ni kazi ya idara ya Utamaduni na TCRA kupiga vita mitandao na matangazo yenye kuathiri tamaduni zetu.

Vilevile, nampongeza Waziri wa sheria, Mheshimiwa Palamagamba Kabudi na Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Mheshimiwa George Masaju kwa kutambua kwamba hoja za kitamaduni, kidini na za kimila ni hoja ambazo ‘very sensitive’  katika taifa letu.

Bila ya shaka, sheria hizi za ndoa za utotoni zilizowekwa kwenye katiba yetu na wazee wetu wakati ule, wazee walio na hekima akiwamo baba wa taifa Mwalimu Nyerere, ni sheria zenye hekima pana sana ambazo zimetulinda na kutuweka kwenye hali ya amani kwa muda mrefu na ni sheria za kuheshimiwa sana na zina maana kubwa sana. Nawashangaa sana kusikia watu wanaosema kwa vishawishi kwamba sheria hizo zimepitwa na wakati. Jibu ni kwamba, binadamu kama ‘binadamu’ yule wa miaka ya 60 na binadamu wa karne ya 21 na hata karne zijazo hawana tofauti, kilichobadilika ni nyakati na mazingira tu yaliyotuzunguka kutokana na teknolojia na utandawazi, lakini binadamu na roho yake na athari zinazotarajiwa kuathiri roho ya mwanadamu kwa yale ya siri au yaliyodhahiri hazijabadilika katika maumbile ya mwanadamu. Tutaathirika tu.

Kwahivyo basi, kwa kuwa misingi ya watu wetu imesimama kwenye dini, utamaduni, mila na desturi, waheshimiwa wanaotuwakilisha sisi masikini, wana dhamana kubwa sana kwa kulinda maslahi ya nchi ya hapa duniani na hata kwenye maisha ya milele kesho akhera. Hawa Watanzania wanawategemea nyinyi kulinda nchi yao, rasilimali zao, utamaduni wao na dini zao. Mkitetereka nyinyi na viongozi wengine wa jamii kwa vishawishi vya nje ya mipaka ya nchi yetu, utamaduni wa taifa utapotea na mtakuwa hamjawafanyia uadilifu vizazi vijavyo ambavyo ndiyo watakao kuwa watoto wetu sote na wajukuu wetu sote. Hatima yake ni mbaya sana.

Twende moja kwa moja kwenye mada. Sheria inazuia watoto wasiolewe mpaka miaka 18 au zaidi. Wakati huo huo, watoto wanapewa mimba wakiwa mashuleni kwa vishawishi vilivyowazunguka na ushawishi wa ubaleghe wao na matakwa yao ya kimwili, halafu baada ya kupata mimba tunamtaka tena aendelee kusoma. Ni nini athari yake? Hapa kuna athari kubwa mbili na pengine zaidi ya mbili:

 1. Baada ya mtoto kupata mimba halafu tukamtaka (au tukamlazimisha) tena aendelee kusoma, wanafunzi wengine wa kike na wa kiume wataliona hili ni jambo la kawaida kwa mtoto wa kike, ambavyo sivyo na wala si jambo la kawaida katika jamii wala katika dini.
 2. Halafu baada ya mtoto wa kike kupata mimba, mtoto wa kiume anaenda jela miaka 30, ambaye kwa dini ya Kiislamu, kwa mfano, mwanamme ndiye anayeruhusiwa kuowa mpaka wanawake wanne (kwa sheria maalum ya Kiislamu) kusitiriana kwa hali zote za kibinadamu. Lakini badala yake, mwanamme ndiye anayepewa adhabu kubwa wakati ashki ni ya wote. Naunga mkono maneno ya Mheshimiwa Nchemba (2017) alivyosema, “Hatuwezi tukaipa dhambi jina zuri na baadaye tukaitukuza. Dhambi ni dhambi, itabakia kuwa dhambi.”

Nataraji tumepata picha ya jinsi ya mustakbali wa taifa utakavyokuwa kijamii ukiangalia na changamoto za utandawazi. Nashauri sheria zinazogusa mambo ya kijamii zisiguswe kwenye katiba yetu kwa faida yetu sote. Leo upo afuweni, mjukuu wako anaweza kuja kuwa gengeni.

Nawapongeza waheshimiwa wabunge wote kwa kazi kubwa wanayoifanya katika jamii na michango yao ya kuleta changamoto kwenye bunge tukufu. Tofauti zenu siyo uadui, bali ni kheri kwenu.

Samahani kama nimekosea.

Ndugu yenu,

Saleh Jaber

30/05/2017

 

MAREJEO:

Kabudi, P. (2017) Dodoma, Tanzania:

https://www.youtube.com/watch?v=YLSU-Xt8W04&feature=youtu.be

Kikwete, S. (2017) Dodoma, Tanzania:

https://www.youtube.com/watch?v=Nk5_D3LDdhE

Masaju, G. (2017) Dodoma, Tanzania:

https://www.youtube.com/watch?v=fa1u5av-FVE&t=4s

Nchemba, M. (2017) Dodoma, Tanzania:

https://www.youtube.com/watch?v=PpWBUx_zDts