MHESHIMIWA RAIS JOHN POMBE MAGUFULI AMPOKEA RAIS WA AFRIKA KUSINI MHESHIMIWA JACOB ZUMA KATIKA ZIARA YA KUENDELEZA UHUSIANO WA KIMAENDELEO NA WA KIHISTORIA BAINA YA NCHI MBILI

 • Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa John Pombe Magufuli, amempokea mgeni wake Rais wa Afrika Kusini, Mheshimiwa Jacob Zuma, jijini Dar es Salaam ambaye yupo katika ziara yake ya kikazi ya siku moja

 • Tanzania na Afrika Kusini wametiliana saini katika mikataba mbalimbali ya maendeleo. Mheshimiwa John Pombe Magufuli amemshukuru Rais Jacob Zuma katika ujio wake nchini na ametanguliza shukran za msaada wa madawati yaliyotolewa na Afrika Kusini mwaka jana katika kampeni aliyoianzisha Rais Magufuli ya kutokomeza uhaba wa madawati mashuleni ili kwenda sambamba na ilani ya chama tawala ya kutoa elimu bure mashuleni kuanzia shule ya msingi mpaka shule za sekondari

 • Mheshimiwa Rais Magufuli amegusia baadhi ya mambo ambayo wamekubaliana na Rais Jacob Zuma katika maendeleo ya nchi ikiwemo biashara na uwekezaji, kukuza sekta ya viwanda, miundombinu ya usafiri, nishati, na mengineyo. Pamoja na hayo, Mheshimiwa Magufuli alifarijika kumjulisha Rais Zuma miradi mbalimbali mikubwa ya kimaendeleo inayoendelea hapa nchini kwa kipindi cha muda mfupi tangu achukue urais, ukiwemo mradi wa umeme na mradi wa ujenzi wa reli ya ‘Standard Gauge’ wa kilomita 1,200 ambao mradi wake katika vipande vilivyobakia, Mheshimiwa Magufuli amemzungumzia Mheshimiwa Zuma kumtafutia njia ya kuupatia mkopo nafuu kwa kupitia jumuiya ya BRICS ili mradi huo ukamilike kwa manufaa ya Watanzania

 • Vilevile, Mheshimiwa Rais Magufuli amehimiza kukuza utalii kwa kuwaunganisha watalii wa Afrika Kusini na wawekezaji wa sekta ya utalii kuwekeza nchini Tanzania bara na visiwani katika maeneo ya vivutio vya kitalii. Mheshimiwa Rais amesisitiza pia kwenye uwekezaji wa madini, madawa, elimu ya mafunzo ya kidaktari, elimu ya sayansi na teknolojia, kupeleka walimu kufundisha lugha ya Kiswahili nchini Afrika Kusini, ulinzi na usalama

 • Mwisho, Mheshimiwa Magufuli amekumbushia ukongwe wa vyama vya CCM na ANC na akasisitiza kuendelea kushirikiana na Afrika Kusini katika kulinda amani na usalama barani Afrika; na kamshukuru Rais Jacob Zuma kwa ujio wake

 • Mheshimiwa Zuma naye amshukuru rais Magufuli kwa mualiko wake nchini Tanzania nchi ambayo ameielezea kuwa nchi nzuri, ya kuheshimika na ni nchi ya kihistoria kwa mchango wake mkubwa katika kuzikomboa nchi nyingi za Afrika kutoka utawala wa kikoloni, ikiwemo Afrika Kusini. Vilevile akazidisha salamu zake kwa waheshimiwa viongozi wa serikali za nchi zote mbili waliohudhuria kwenye hafla hiyo na akaendelea kwa kutoa rambirambi za vifo vya wanafunzi waliopata ajali Arusha

 • Mheshimiwa Zuma amechukua fursa ya ujio wake kusheherekea mwaka huu na Watanzania, urithi wa Mheshimiwa Oliver Reginald Tambo (miaka 100 tangu kuzaliwa kwake, 27 Oktoba 1917), kwa kuwa Tanzania ilikuwa ni nchi ambayo imechukua nafasi muhimu katika maisha yake na maisha ya chama cha ANC walipokutana na akina Mandela mjini Dar es Salaam mwaka 1962 katika kuunganisha urafiki na kujadili uhuru wa Afrika Kusini

 • Mheshimiwa Zuma ameeleza, maamuzi ya makutano hayo ndiyo yaliyobadilisha dira ya chama tawala cha ANC katika kuikomboa Afrika Kusini, na tangu wakati huo, Tanzania imekuwa ndiyo nchi pekee iliyotarajiwa kuikomboa Afrika Kusini kutoka kwa makaburu, watu ambao hawakuthamini utu wa mtu wala roho za watu

 • Kutokana na hivyo, Tanzania imekuwa ni nchi muhimu sana katika historia ya Afrika Kusini, ameeleza Zuma

 • Mheshimiwa Zuma ameunga mkono mazungumzo yao na Mheshimiwa Magufuli ya kuwa Tanzania na Afrika Kusini ni nchi ndugu na ni nchi zenye uhusiano mkubwa wa kihistoria. Vilevile, ameridhia ushirikiano baina ya nchi mbili kwenye maeneo ya ulinzi na usalama wa taifa, sayansi na teknolojia, sanaa na utamaduni, mazingira, biashara na uwekezaji, usafiri, maliasili, na kadhalika

 • Katika maridhiano ya kiuchumi, Mheshimiwa Zuma amesema wataangaza zaidi kwenye uwekezaji binafsi, miundombinu, usindikaji wa mazao, uchakataji wa makanikia, na miradi ya pamoja ambayo mikakati yake yameandaliwa jioni hiyo kwa wafanyabiashara wa nchi zote mbili kuangalia fursa hizo za kibiashara na wakati huo huo zikisimamiwa na vyombo maalum vya serikali za nchi zote mbili na mpaka kufikia kusaini makubaliano ya mwisho na kuyatekeleza makubaliano yote ambayo yaliyokuwa tayari yashapitishwa

 • Pamoja na hayo, kutakuwa na mikutano ya hapa na pale ya kuzidisha uhusiano wa kibiashara na vilevile kuzidisha uhusiano baina ya watu wa Tanzania na Afrika Kusini kwa programu maalum inayoitwa African Liberation Route ambayo inasimamia kuonesha historia kubwa ya jitihada ya Afrika Kusini katika ukombozi wake

 • Tanzania chini ya uongozi wa Mwalimu Nyerere, ilikuwa ndiyo nchi kiongozi katika kuunda na kuendesha kamati ya ukombozi na vilevile katika kuunda na kuendesha jumuiya ya umoja wa Afrika (OAU). Tanzania, bila ya shaka ndiyo nyumba ya historia ya ukombozi wa Afrika Kusini, amesema Mheshimiwa Zuma

 • Ameendelea kusema, hivi karibuni Afrika Kusini imefarijika kumpatia hayati Jenerali Hashim Mbita, kwa heshima na taadhima, tuzo yenye heshima kubwa nchini Afrika Kusini, The Order of the Companions of O. R. Tambo, kuashiria heshima kubwa na mchango mkubwa wa hayati Jenerali Hashim Mbita (Mtanzania) aliyekuwa katibu mkuu wa kujitolea kwa dhati katika kamati ya ukombozi ya Jumuiya ya Umoja wa Afrika (OAU)

 • Pamoja na hayo, Afrika Kusini na Tanzania imekuwa ikibadilishana mitazamo ya kiusalama na ya kisiasa ya kikanda na Afrika nzima. Tanzania ni nchi inayoendelea kupigania usalama na amani barani Afrika na imetoa mchango mkubwa katika kupigana na ukoloni na ubaguzi wa rangi nchini Afrika Kusini. Mbali na hayo, Mheshimiwa Zuma amejitolea kufanya kazi pamoja na Tanzania katika kutatua changamoto za hali ya kisiasa ya baadhi ya nchi za Afrika ikiwemo Kongo ili kuleta hali ya usalama na amani

 • Mheshimiwa Zuma amekana vikali, ugaidi wa aina yoyote ule na unapotokea popote pale. Ni vigumu kutekeleza na kufikia malengo ya Agenda 2063 iwapo hatutapata usuluhisho wa changamoto za usalama na amani zinazokabili bara la Afrika, amesema Zuma

 • Mheshimiwa Jacob Zuma amemalizia kwa kusema, amefarijika kwa ujio wake na kukutana na kufanya mazungumzo na Mheshimiwa Rais Magufuli katika mambo muhimu; na vilevile makutano haya, ni njia moja wapo ya ukumbusho wa mchango wa Tanzania kwa nchi mbalimbali za Afrika, hususan Afrika Kusini, na amesema kuna sehemu nyingine za kihistoria nchini Tanzania ambazo Afrika Kusini haitozisahau katika maisha yake, kwa mfano, Mazimbu na Dakawa, mkoani Morogoro

 • Ingawa hajui Kiswahili, lakini Mheshimiwa Zuma amesema anapenda maneno ya Kiswahili kama ‘Ndugu’, ‘Ndugu zetu’. Amempongeza Rais Magufuli kwa kumpokea kwa ukarimu mkubwa yeye na jopo lake na kujisikia kama yupo nyumbani. Amempa shukran nyingi na amemualika Rais Magufuli kutembelea Afrika Kusini katika wakati muwafaka ili kuendeleza uhusiano wa nchi mbili

Advertisements