ALIYEKUWA MEYA WA DAR ES SALAAM NA MAKAMU WA MWENYEKITI WA YANGA (MIAKA YA 60 NA 70) MHESHIMIWA KITWANA KONDO AZIKWA LEO

Na Eliphace Marwa – Maelezo:

RAIS Mstaafu Ali Hassan Mwinyi ameongoza mamia ya wakazi wa jiji la Dar es Salaam katika maziko ya mwanasiasa mkongwe na aliyekuwa Mstahiki Meya wa Jiji la Dar es Salaam, Kitwana Kondo.

Mbali na Mwinyi wengine waliohudhuria maziko hayo yaliyofanyika katika makaburi ya Tambaza ni Makamu wa Rais Mstaafu, Mohammed Gharib Bilal, Mawaziri Wakuu Wastaafu, Salim Ahmed Salim na Edward Lowassa, Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Abdulrahman Kinana, Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba pamoja na wengine.

Akizungumza nyumbani kwa marehemu, Mzee Mwinyi alisema, marehemu Kondo alikuwa  ni mtu ambaye alijitoa katika kulitumikia taifa kwa moyo wake, hivyo mchango wake ni mkubwa katika kulitumikia taifa na hasa wakazi wa jiji la Dar es Salaam.

“Alikuwa ni rafiki yangu ambaye tumefahamiana kwa muda mrefu sana, tumepoteza mtu muhimu sana, lakini kazi ya Mungu haina makosa, tumuombee kwa Mwenyezi Mungu amlaze mahali pema peponi,” alisema Mzee Mwinyi.

Kwa upande wake, Kinana alisema, taifa na hasa wakazi wa Dar es Salaam wamepata pigo kubwa kwa kumpoteza mzee huyo ambaye bado busara zake zilikuwa zikihitajika.

“Alikuwa ni kiongozi wa jamii, alikuwa ni mwalimu wa watu wengi katika mambo mbalimbali, ni msiba mkubwa lakini ni kazi ya Mungu, tuendelee kumuombea apumzike kwa amani,” alisema Kinana.

Naye, Waziri Mkuu wa Zamani, Edward Lowassa alisema, kutokana na kazi kubwa iliyofanywa na Mzee Kondo ni vema uongozi wa jiji kuangalia namna ambavyo barabara moja ya jiji hilo likapewa jina la KK ikiwa ni kuheshimu na kutambua mchango wake.

“Namuomba Mstahiki Meya, barabara moja uiite KK, itakuwa ni heshima kumuenzi Mzee Kitwana Kondo kwa kazi kubwa aliyofanya wakati wa uhai wake,” alisema Lowassa.

Naye Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba alisema, mchango wa Mzee katika taifa ni mkubwa lakini kwa bahati mbaya ni kama umeshindwa kutambuliwa.

“Ni mtu ambaye bahati mbaya sana historia ya nchi yetu haitambui mchango wake katika kuleta uhuru wa nchi na kudumisha uhuru wa nchi hii,” alisema Profesa Lipumba.

Akieleza chanzo cha kifo cha baba yake, mtoto wa kwanza wa marehemu Mzee Kondo, Stara Kondo alisema, Baba yake alilazwa katika hospitali ya Hindu Mandal Mei 18 kutokana na kuugua muda mrefu lakini alifariki juzi.

“Alikuwa anaumwa muda mrefu lakini hadi anafariki madaktari walisema alipata stroke (Kiharusi) na shinikizo la damu, tutamkumbuka kwa mambo mengi kwa sababu ni baba lakini alikuwa ni kichwa cha familia,” alisema Stara.

mwinyi

Rais Mstaafu wa awamu ya pili, Alhaj Ali Hassan Mwinyi akiweka udongo kwenye maziko leo makaburi ya Tambaza jijini Dar es Salaam.

bomani

Jaji Mstaafu, Mheshimiwa Mark Bomani akiweka udongo kwenye maziko leo makaburi ya Tambaza jijini Dar es Salaam.

kingunge

Mwanasiasa Mkongwe nchini, Mheshimiwa Kingunge Ngombare Mwiru akiweka udongo kwenye maziko leo makaburi ya Tambaza jijini Dar es Salaam.

gharib bilal

Makamu wa Rais Mstaafu, Mheshimiwa Gharib Bilal akiweka udongo kwenye maziko leo makaburi ya Tambaza jijini Dar es Salaam. Picha zote na Emmanuel Massaka, Globu ya Jamii.

Allah awape subra familia ya marehemu katika kipindi hiki kigumu na roho ya marehemu ailaze mahala pema peponi, Jannat Firdous. Amin.

Inna lillahi wa inna ilayhi raajio’un.

Advertisements

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out / Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out / Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out / Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out / Change )

Connecting to %s