WAKAZI WA MKURANGA WALONGA HALI HALISI YA UNYANYASAJI NA KERO KWA WAKAZI WA MKOA WA PWANI

Baadhi ya wakazi wa Mkuranga wahojiwa na kutoa muono wao wa hali halisi inayoendelea Mkoa wa Pwani na kila mmoja wao ameelezea kwamba Polisi wanawanyanyasa na wanawasumbuwa kufanya kazi zao kwa utulivu na kwa hivyo wamekosa amani. Haya ni maneno ya wakazi na raia wema wenyewe ambao hawafanyi uhalifu wowote. Kwa muda gani wamekuwa wakinyanyaswa, haijulikani.

Ushauri wangu kwa Mheshimiwa Rais ni kuliangalia hili suala kwa ukaribu zaidi kwa amani ya watu wa mkoa wa Pwani. Wakazi wazawa wa maeneo hayo wapewe uhuru wao wa kufanya kazi zao kwa utulivu na amani na bila ya kusumbuliwa kwa kuhamishwa hamishwa na mpaka kufikia hali ya kukosa amani na sehemu zao wenyewe.

Kwa hali hiyo iliyojitokeza kwenye hii video ya Global TV (2017), naishauri serikali kwanza isitumie nguvu ya dola na kusababisha hatari kubwa zaidi. Badala yake, Polisi na uongozi wa CCM wa maeneo hayo wawape amani wakazi wa maeneo hayo kwa kuwaacha na maeneo yao ya makazi na sehemu zao za kujitafutia riziki kwa amani na utulivu na kutafuta njia za kuzungumza na wakazi wa mitaa ya hapo na vijiji vya hapo kwa kuwatatulia changamoto zao na kuwawekea mazingira mazuri, bila ya vitisho; na nina imani kubwa na Rais Magufuli kuwa ni rais msikivu na mwenye kuwatakia watu wake umoja, upendo na amani.

Kuna kitu wazungu wanakiita ‘Gentrification’. Gentrification ni neno ambalo asili yake lilifafanuliwa na bibi mmoja nchini Uingereza anaitwa Ruth Glass (1964) alifafanua, Gentrification ni hali ya kuifanya sehemu moja ya hali ya watu wa chini kuigeuza kuwa ni sehemu ya hali ya juu kwa kuwatoa na kuwafukuza watu wa hali ya chini maskini na kuwapa watu matajiri kujenga nyumba za ghali, halafu kuwasukuma watu maskini mbali na maeneo yao waliyozaliwa nayo na waliyokulia nayo na kuwafanya washindwe kuishi maisha ya hapo walipozaliwa. Kwa lugha nyingine ya kigeni (Social cleansing). Hii ni hali ya hatari nchini kwetu.

Nchi yetu ni nchi ya kijamaa na ndiyo misingi aliyotuwekea baba wa taifa Mwalimu Nyerere. Badala ya kuwafukuza watu maeneo yao tulikuwa tunatakiwa wakazi wa maeneo fulani (popote nchini) waachwe kwa amani katika maeneo yao na badala yake kuwaboreshea maeneo yao ili waendelee kutunza utamaduni wao (ambao ni utamaduni wa Kitanzania) na unatakiwa kulindwa kama ilivyo tamaduni zingine nchini mwetu.

Bi Ruth Glass (1964) alisema, kawaida ya Gentrification inapoanza sehemu moja haiishii hapo itaenda sehemu nyingine ya karibu yake inayofuata, halafu itaendelea kuwa hivyo hivyo na hatimaye watu wa hali ya chini wataendelea kuwa na hali ya chini na watu wa hali ya juu wachache ndiyo watakaofaidika na utamaduni wa watu utapotea.

Mheshimiwa Rais Magufuli nampongeza kwa kuonesha mfano wa kusimamia msingi wa nchi yetu ya Kijamaa kama inavyoainishwa kwenye katiba yetu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na katiba ya chama tawala cha CCM, kwa kuonesha mfano hivi karibuni kwa kuwatetea Watanzania wanyonge wa Magomeni Kota kwa kuchukua sehemu yao ambayo ni ya ghali kwa thamani, na badala yake kuwarudishia sehemu hiyo hiyo wale masikini wanyonge kwa thamani ndogo kutokana na uwezo wao wa chini. Huu ndiyo uadilifu wa rais wetu mwema, na ndiyo siasa ya nchi yetu. Vinginevyo, Rais Magufuli asingefanya hivyo, ingekuwa ni Gentrification ya kuwanyanyasa wanyonge na ni kinyume na msimamo wa CCM na ni kinyume na siasa ya nchi yetu. Tanzania inaweza ikafanya maboresho ya sehemu za watu maskini kwa kuwasaidia maskini kwa kuwatoa watu maskini kutoka kwenye umaskini, na si kinyume chake.

Nashauri itumwe tume huru ichunguze kwa kina kama kuna ushawishi wowote wa watu wachache kule wanaotumia vyombo vya dola kujifaidisha kibinafsi badala ya kufaidisha wananchi wanyonge; na kusikiliza kero za hawa wakazi wa Mkuranga, Kibiti na Rufiji, ili waboreshewe maeneo yao na wasiendelee kunyanyaswa na Polisi. Haiihitaji nguvu huko. Siyo bure!

AMANI! AMANI! AMANI!

Samahani kama nimekosea.

Ndugu yenu,

Saleh Jaber

30/05/2017

 

MAREJEO:

Glass, R. (1964). Aspects of Change. 1st ed. London: MacGibbon & Kee Ltd.

TV, G. (2017). Walichokisema Wananchi wa Mkuranga. [Online] YouTube. Available at:

[Accessed 30 May 2017].

Advertisements

One thought on “WAKAZI WA MKURANGA WALONGA HALI HALISI YA UNYANYASAJI NA KERO KWA WAKAZI WA MKOA WA PWANI

  1. JAMII YA TANZANIA NA ATHARI ZA UTANDAWAZI WA KIUCHUMI NA KISIASA – SJ POST

Comments are closed.