ATHARI YA KUFUTA TOZO YA VIPULI NA ZANA ZA VIWANDA KWENYE BAJETI YA 2017/2018

Ningependa kutoa mchango wangu mdogo wa haraka haraka kenye bajeti ya mwaka 2017/2018 iliyopendekezwa mwezi wa sita na Waziri wa Wizara ya Fedha, Mheshimiwa Philip Mpango, kupitia TBC via BongoStars online TV (2017), ingawa mimi siyo mwanauchumi lakini nataraji mchango wangu utasaidia kwa njia moja au nyingine. Kwa kweli inaonesha jinsi gani serikali hii ya awamu ya tano ilivyokuwa sikivu kama zilivyokuwa awamu zilizopita na vilevile jinsi gani serikali hii ya awamu ya tano inavyojali maslahi ya watu wake kwa kuwanyanyua kiuwezo katika maisha yao. Wengi wamechangia maeneo mbalimbali kwenye bajeti hii ya mwaka 2017/2018 ambayo michango yao ina muelekeo mzuri na ina tija nzuri, lakini mimi ningependa kuchangia sehemu moja tu, kwenye tozo iliyofutwa ya kuingiza vipuli vya kuchochea viwanda (kama sijakosea).

Kwasababu tumeshaanza mbio za uchumi wa viwanda, pendekezo la kufuta tozo kwenye vipuli vya kuchochea viwanda ni pendekezo zuri sana lakini tuangalie pia athari zake kwa upande mwingine.

Nchi yetu ni nchi ambayo siyo ‘Surplus country’ kwa maana ya kwamba hivi sasa tunanunua bidhaa zaidi kutoka nchi za nje kuliko sisi tunavyouza kupeleka nchi za nje; matokeo yake ni kwamba serikali hatupati pesa zinazotoka nje ya nchi na kuingia ndani ya nchi zikiwa kama ni mapato ya serikali.

Kinachotokea hivi sasa nchini kwetu, zile nchi tajiri zenye uwezo ‘surplus countries’ zinakuja kuwekeza nchini kwetu. Uwekezaji huu siyo wa serikali ya Tanzania na siyo ya Watanzania bali ni ya wawekezaji wageni wa nje ambao wanatumia ardhi ya Tanzania, wafanyakazi wa hali ya chini wa Tanzania na maliasili ya Tanzania. Lakini bidhaa zote na pesa yote inayovunwa inarudi nchini kwao na Tanzania inabakishiwa na kodi tu ambayo haitoshelezi kutukwamua kiuchumi mpaka kufikia kuwa ‘surplus country’.

Kivutio kilichowekwa cha kuondoa kodi za vipuli na zana za viwanda ili kuchochea viwanda watakaofaidika wengi wao ni wageni na si wazawa. Na matokeo yake ndiyo niliyoyaelezea hapo juu ya kwamba mavuno yote yataenda nje na Tanzania itabaki na kodi tu na ajira ndogondogo za watu wa hali ya chini. Isieleweke vibaya, uwekezaji unakaribishwa lakini lazima tuangalie athari zake kwa pande zote.

Kuna mambo mawili yatatokea na serikali iyaangalie haya kwa makini:

  1. Baadhi ya Watanzania wataweza kufaidika ikiwa wataingia ubia katika uwekezaji na wageni kwa kujipatia mapato ya mauzo yao ya nje ya nchi ambayo yatakadiriwa na serikali kwa ujumla wa uzalishaji wake ili serikali ijue hasa nini mapato ya kila kilichochumwa ndani ya nchi.
  2. Muwekezaji mgeni ataondoka na faida yote na kuacha kodi ya serikali tu kama nilivyoielezea hapo juu ambayo haitotosheleza kujikwamua kiuchumi kufikia kuwa ‘surplus country’.

Naishauri serikali, suluhu ya fursa hii ya kufuta tozo ya vipuli na zana za viwanda kwa hapa tulipo ni kuweka balance ya uwekezaji kwa baadhi ya mambo niliyoyapendekeza hapo chini kwa sasa baina ya utandawazi wa ndani na utandawazi wa kidunia.

Hatua hizi chache zitatusaidia kwa sasa kwasababu nchi yetu na wananchi wake wengi hawana uwezo wa kuwekeza na kufikia matakwa ya wananchi wote kihali, kimali, kiafya, maisha bora na ustawi wa jamii. Vilevile, ikiwa tutafungulia mlango huu wa kuingizwa bure vipuli na zana za viwanda, hatari yake ni kwamba nchi za nje zenye uwezo na wenye watu wenye uwezo kuliko nchi yetu watakuja kutanda kwenye ardhi yetu na mpaka kupelekea wazawa kukosa ardhi ya kuwekeza au kufanyia mambo yao ya kujiendeleza na kujikwamua kiuchumi hapo watakapo kuwa tayari kufanya hivyo. Na hasa ukizingatia kwamba ardhi inatolewa kwa mikataba ya miaka mingi. Kwahivyo tufanye haya mambo kwa mbinu strategic kama ifuatavyo:

  1. Serikali kuweka kikomo (cap) cha wawekezaji wa nje ambao wanazalisha ndani lakini wanauza bidhaa zao nje ya nchi ambayo mapato yake hayarudi nchini. Hii itasaidia kuzuia bidhaa ya aina moja kuzalishwa nchini na viwanda visivyo na idadi ndani ya nchi bila ya faida ya serikali na watu wake.
  2. Kuwafanyia wepesi na kuwashawishi wawekezaji wa nje kuwekeza kwenye maeneo ya mazao na bidhaa mbalimbali ambazo zitauzwa ndani ya nchi tu, bidhaa ambazo wananchi Watanzania wanazihitaji zaidi katika maisha yao ya kila siku, kwa mfano matunda, unga, mchele, dawa ya meno, sabuni, viatu, nguo, na kadhalika. Kwa kufanya hivyo siyo kwasababu nyingine, ila bidhaa za ndani ziwe rahisi kwa wananchi wa hali ya chini na waweze kuishi maisha mazuri ya kibinadamu na waweze kupata mahitaji yao ya kila siku kwa bei ya chini na bei nafuu.
  3. Serikali iweke bei elekezi kwa wawekezaji wa nje kwenye maeneo hayo yaliyotajwa hapo juu kwa kumlenga mwananchi wa hali ya chini, lakini wakati huo huo muwekezaji naye apate faida.
  4. Serikali iweke masharti kwa wawekezaji kuzalisha kwa viwango tofauti kwa maana ya kwamba, mfano wawekezaji wa nguo wanaweza kuzalisha nguo kwenye viwango viwili au hata viwango vitatu tofauti (kwa kushirikisha TBS na TFDA) ili hata yule asiyejiweza kabisa wa hali ya chini aweze kununua shati jipya la kuvaa lenye kiwango cha chini badala ya kununua mtumba. Hali kadhalika viwango tofauti kwenye matunda, vyakula, na kadhalika.
  5. Ajira kwa wafanyakazi wazawa iwe asilimia 85 mpaka asilimia 90 kwa viwanda vya wawekezaji wa nje na wa ndani.
  6. Serikali iimarishe ukusanyaji wa mapato kwa njia ya elektroniki.

Ingawa nchi rafiki zinaweza zikawa na maelewano mazuri ya kidiplomasia kwa maslahi ya pande zote mbili, haimaanishi kwamba nchi rafiki itaweka maslahi ya kiuchumi ya Tanzania kwanza kabla ya nchi yake au kabla ya maslahi binafsi.

Huu ndiyo ushauri wangu na mchango wangu wa bajeti ya fedha kuelekea uchumi wa viwanda na kuwakwamua Watanzania kuelekea kwenye uchumi wa kati 2025. Tutafika tu.

Samahani kama nimekosea popote.

Ndugu yenu,

Saleh Jaber

14/06/2017

 

MAREJEO:

Mpango, P. (2017). Bajeti Kuu Ya Serikali Ya 2017/2018. [Online] YouTube. Available at:

[Accessed 14 June 2017].

Advertisements