MHESHIMIWA RAIS JOHN POMBE MAGUFULI AONGOZA MAELFU YA WATANZANIA KATIKA SIKU YA KIHISTORIA YA SHEREHE YA MUUNGANO WA TANGANYIKA NA ZANZIBAR ILIYOFANYIKA JIJINI DODOMA

 • Mheshimiwa Rais John Pombe Magufuli aongoza maelfu ya Watanzania na wageni kutoka nchi mbalimbali katika siku ya kihistoria ya sherehe za Muungano wa Tanganyika na Zanzibar iliyofanyika jijini Dodoma

 • Katika hotuba yake, Mheshimiwa Rais John Pombe Magufuli atambua uwepo wa Rais wa Zanzibar, Ali Mohammed Shein, Makamu wa Rais, Mheshimiwa Mama Samia Suluhu Hassan, Rais wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB), Akinwumi Adesina, Waziri Mkuu, Mheshimiwa Kassim Majaliwa, Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Mheshimiwa Balozi Seif Ali Idd, Spika wa Bunge la Afrika Mashariki, Mheshimiwa Martin Ngoga, Jaji Mkuu wa Tanzania, Mheshimiwa Ibrahim Juma, Jaji Mkuu wa Zanzibar, Mheshimiwa Omar Makungu, Rais Mstaafu wa awamu ya tatu, Mheshimiwa Benjamin Mkapa na mkewe, Mheshimiwa Mama Fatma Karume, Waheshimiwa Wake wa Viongozi, Waheshimiwa Mawaziri Wakuu Wastaafu, Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Waheshimiwa Wabunge, Waheshimiwa Mabalozi, Waheshimiwa Viongozi wa Vyama vya Siasa, Viongozi mbalimbali, wageni waalikwa na wananchi wote

 • Mheshimiwa Rais John Pombe Magufuli aliielezea tarehe hii ya leo mwaka 1964, Jamhuri ya watu wa Tanganyika na Zanzibar ziliungana na kuwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kama taifa jipya baada ya Hayati Sheikh Abeid Karume na Mwalimu Nyerere kutia saini ya kuunganisha nchi mbili katika siku ya kihistoria ya tarehe 26 Aprili 1964 na kuridhiwa na mabunge ya nchi zote mbili

 • Mheshimiwa Rais Magufuli alisema, maono ya Mzee Abeid Karume na Mwalimu Nyerere ndiyo yameunda Muungano huu na kuamua kuunganisha vyama viwili vya TANU (Tanganyika African National Union) na ASP (Afro Shirazi Party)

 • Amshukuru Mwenyezi Mungu kwa siku ya leo ya kihistoria na amshukuru Mungu kwa kuendelea kuulinda muungano na kulilinda taifa letu kwa ujumla. Awapongeza Watanzania wote wa dini zote, wa makabila yote, wa vyama vyote, na wa rangi zote waliopo ndani na nje ya Tanzania kwa kuadhimisha sherehe za miaka 54 ya muungano wa kuzaliwa taifa letu (Tanzania) “Happy birthday Tanzania, Happy birthday Watanzania, Happy birthday Muungano wetu ambao umetengeneza taifa la Tanzania”, alisema Mheshimiwa Rais Magufuli

 • Awashukuru mabalozi na wawakilishi wa taasisi mbalimbali za kimataifa ambao wamekuja kushiriki katika sherehe za muungano wa Tanzania, na amkaribisha na amtambulisha Rais wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB), Mheshimiwa Akinwumi Adesina pamoja na wajumbe wake

 • Aielezea umuhimu wa benki ya maendeleo ya Afrika (AfDB) ambayo inatoa mchango mkubwa kwa maendeleo ya bara la Afrika ikiwemo misaada ya kifedha, lakini pia inatoa ushauri na utaalamu. Na kwa bahati nzuri, Tanzania ni nchi moja wapo iliyoshiriki kuasisiwa kwa benki hiyo na pia ni mnufaika mkubwa wa benki hiyo. Akaendelea kuelezea, mathalan tangu imeanza kufanya kazi yake melini Tanzania mwaka 1971, Tanzania imenufaika na mkopo wa kifedha wenye thamani ya dola za Kimarekani, bilioni 3.457 na tangu mwezi Novemba mwaka 2017, benki hiyo inatekeleza miradi 25 yenye thamani ya dola za Kimarekani, bilioni 1.986

 • Mheshimiwa Rais aliainisha kwamba anatarajia kwenda Kondoa na Mheshimiwa Adesina kuzindua barabara ya Dodoma-Babati yenye urefu wa kilomita 251 ambayo Tanzania inashirikiana na Benki ya Afrika ya Maendeleo kuijenga barabara hiyo. Pia benki hiyo imefadhili barabara ya Dodoma-Iringa yenye urefu wa kilomita 260, na pia barabara ya Bububu-Mkokotoni yenye urefu wa kilomita 31, pia barabara za vijijini, Zanzibar, zenye urefu wa kilomita 21

 • Atoa shukran kwa Benki ya Maendeleo ya Afrika kwa niaba ya Watanzania kwa misaada mbalimbali wanayoitoa kwa maendeleo ya Tanzania na anatarajia kufanya mazungumzo naye kwa maendeleo ya barabara za Dodoma, hususan, barabara ya mzunguko (ring road)

 • Aelezea mafanikioa yaliyopatika ndani ya miaka 54 ya Muungano wa Tanzania, hususan kudumisha muungano wenywe ambao wapo wenzetu wengi walijaribu kuunda muungano kama wetu lakini hawakufanikiwa. Mheshimiwa Rais alielezea kuongezeka kwa maeneo ya mashirikiano kwa bara na visiwani kwa kutolea mfano mwaka 1964 maeneo ya mashirikiano yalikuwa 11 tu, lakini mpaka sasa tuna maeneo ya ushirikiano 22 ambayo yote yameongezwa kwa mujibu wa sheria kwa maridhiano ya pande zote mbili za muungano

 • Akaendelea kuelezea kwamba Muungano umefanya nchi yetu iwe yenye sauti, kuwa na nguvu zaidi, kuheshimika zaidi, na kujiamini kimataifa. Tumeweza kulinda uhuru na mipaka yetu na kujiamulia mambo yetu sisi wenyewe na kuwa na uwezo wa kutoa michango mbalimbali ya kimataifa katika kusaidia harakati za ukombozi, kutetea haki za wanyonge, pamoja na kusuluhisha sehemu mbalimbali za migogoro duniani

 • Halikadhalika, Muungano umewezesha mafanikio makubwa katika nyanja za kiuchumi, kisiasa, na kijamii. Tanzania ya leo siyo Tanzania ya mwaka 1964, hongera sana Watanzania, alisema Mheshimiwa Rais Magufuli

 • Aainisha maendeleo mbalimbali ya taifa ikiwemo umeme, usafiri wa nchi kavu, anga, na majini. Kuboresha huduma za jamii kama elimu, afya, na taasisi mbalimbali zinazosimamia. Awashukuru Mwalimu Nyerere na Mzee Karume kwa mchango wao mkubwa uliosaidia kupatikana kwa mafanikio haya

 • Afurahishwa kwenye sherehe hiyo kwa uwepo wa Mama Fatma Karume na amshukuru Mama Maria Nyerere kwa wote kuendelea kuunga mkono na kuhakikisha kwamba muungano wetu unadumu. Pia ashukuru na atambua mchango wa Rais wastaafu, Alhajj Ali Hassan Mwinyi, Mheshimiwa Benjamin Mkapa, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete, Mheshimiwa Salmin Amour, Mheshimiwa Amani Karume, Mheshimiwa Ali Mohammed Shein, na viongozi wote wastaafu na wazee ambao wamelitumikia taifa hili kwa uaminifu na kwa uadilifu “Ahsanteni sana wazee” alisema Rais Magufuli. Akaendelea kuwashukuru Watanzania wote kwa michango yao mbalimbali yaliyowezesha kwa kupatikana kwa mafanikio haya na atambua michango yao

 • Pamoja na hayo, Mheshimiwa Rais Magufuli aainisha kuwepo kwa changamoto za muungano ambazo amezielezea kwamba hakuna jambo zuri, lenye kukosa kasoro. Ameeleza kwamba kwa bahati nzuri, pande zote mbili za muungano wameweka utaratibu mzuri wa kuzishughulikia changamoto zilizopo

 • Ampongeza Makamu wa Rais, Mheshimiwa Mama Samia Suluhu Hassan, Mwenyekiti wa Kamati ya Muungano ambaye amefanya kazi kubwa na nzuri sana ya kushughulikia masuala ya muungano na changamoto zake. Pia ampongeza Mheshimiwa Kassim Majaliwa, Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Idd, Mawaziri, na Makatibu Wakuu wa Serikali zote mbili ambao ni wajumbe wa kamati hiyo. Mheshimiwa Rais John Pombe Magufuli aainisha kwamba ana matumaini makubwa kwa kupitia kamati na kwa ushirikiano wa wananchi wote, hatimaye changamoto hizo zilizobaki zitamalizwa

 • Afurahishwa na kauli mbiyu ya sherehe ya muungano ya mwaka huu ambayo inasema miaka 54 ya muungano wetu ni mfano wa kuigwa duniani. Tuuenzi, tuulinde, tuuimarishe, na kuudumisha kwa maendeleo ya taifa letu. Mheshimiwa Rais amesisitiza iwapo kauli mbiyu hiyo itatekelezwa kwa vitendo, tutaweza kutimiza dhamira ya waasisi wa muungano, baba wa taifa Mwalimu Nyerere na Mzee Karume, na asitokee mtu wa kuuvunja muungano na tusikubali kwa mtu, kundi, au chama chochote kuchezea muungano wetu. Mheshimiwa Rais Magufuli aahidi na Dokta Shein kuulinda muungano kwa gharama zote kwasababu ndiyo nguvu yetu na ndiyo silaha yetu kwa taifa

 • Mheshimiwa Rais Magufuli akaendelea kusisitiza kwamba kila mmoja ana wajibu wa kuulinda muungano. Wananchi wana wajibu wao na serikali zipo imara katika kuulinda muungano wake na kamwe hatoonewa aibu mtu yeyote awe ndani au nje ya nchi atakayejaribu kuuvuruga muungano wetu

 • Asisitiza Watanzania kuendelea kuilinda amani ya nchi kwasababu ndiyo msingi wa maendeleo. Atoa wito kwa Watanzania wasikubali kutumika kuivunja amani ya nchi na amewaomba wananchi kushirikiana na vyombo vya ulinzi katika kulinda amani. Asisitiza kwamba serikali ipo imara katika kuilinda na kuitunza amani

 • Awahakikishia Watanzania kwamba azma ya serikali kuhamia Dodoma ipo pale pale, na kama alivyoahidi mwaka huu anahamia Dodoma ikiwa sasa kama ndiyo makao makuu ya nchi. Mheshimiwa Rais Magufuli aliainisha kwamba alifurahishwa kumuona Mzee Kidumile aliyeimba wimbo wa Dodoma kama ndiyo makao makuu, vilevile amefurahishwa na Marin Hassan, mtangazaji wa TBC, anavyoiwakilisha safari ya Dodoma

 • Mheshimiwa Rais alieleza kwamba, makao makuu ya nchi kama ilivyokuwa Dar es Salaam miaka iliyopita na kuitwa jiji, akaangalia Tanzania ina majiji mangapi? manispaa ngapi? halmashauri ngapi? na kisha akaangalia mamlaka aliyokuwa nayo katika kutengeneza majiji, au manispaa, na kadhalika. Alichobaini ni kwamba Dar es Salaam ni jiji, Tanga ni jiji, Arusha ni jiji, Mwanza ni jiji, Mbeya ni jiji, na alipouliza kuhusu Dodoma akabaini kwamba Dodoma ni manispaa

 • Mheshimiwa Rais Magufuli akaelezea kwamba kaona haiwezekani Dodoma kuwa makao makuu ya nchi lakini bado haijawa jiji, na kwa mamlaka aliyokuwa nayo, Mheshimiwa Rais akawatangazia wananchi kwa mamlaka waliyompa kisheria, kuanzia leo, “Dodoma ni Jiji”, alisema Mheshimiwa Rais Magufuli. Shangwe na vifijo vilitoka kwa wananchi kwa furaha kubwa ya kutangazwa rasmi Dodoma kuwa jiji

 • Atoa wito kwa viongozi wahusika kwamba kuanzia leo tarehe 26 Aprili 2018 taratibu zote za kisheria zianze kutumika kama alivyoagiza, na amtangaza rasmi Mkurugenzi wa Manispaa ya Dodoma kuwa Mkurugenzi wa jiji la Dodoma kuanzia tarehe ya leo 26 Aprili 2018. Awaahidi Watanzania kwamba Dodoma itakuwa jiji la kipekee, na miradi mbalimbali itakayoombwa ikiwemo ya AfDB kwa jiji la Dodoma ili mambo yote mazuri yanayopatikana kwenye jiji yaweze kupatikana Dodoma kwasababu Dodoma ndiyo makao makuu ya nchi. Awapongeza wakazi wa Dodoma kwa upendo wao, mshikamano wao, na umoja wao wanaoutoa kwa wageni wanaokuja kwenye jiji la Dodoma na awapongeza kwa ukarimu wao

 • Aliponge jeshi kwa kazi nzuri wanazozifanya na akapongeza maonyesho ya sherehe za muungano ambayo yametoa mafunzo na elimu kupitia halaiki na jeshi la ulinzi na usalama. Atoa wito kwa Watanzania kuwa wamoja kwa ajili ya kulijenga taifa na uchumi wa taifa. Aelezea mambo mbalimbali ya maendeleo na awahakikishia Watanzania kwamba uchumi unaenda vizuri na akasisitiza kuutunza muungano na amani bila ya kujali vyama vyetu, dini zetu, makabila yetu, umri wetu, na hata maeneo yetu. Awausia wananchi kwamba nchi yoyote iliyotulia na kupendeza, wenye wivu huwa hawakosekani

 • Amalizia hotuba yake kwa kuvishukuru vyombo vyote vya ulinzi, waandishi wa habari, wananchi, na washereheshaji katika siku hii ya kihistoria ya Muungano wa Tanzania. Akamalizia kwa kuutukuza muungano, na jiji la Dodoma, na amani ya nchi, Tanzania, na Dokta Shein. Awashukuru wananchi kwa kumsikiliza na akaliombea baraka taifa na watu wake