MHESHIMIWA RAIS JOHN POMBE MAGUFULI AFUNGUA RASMI MAKTABA MPYA YA CHUO KIKUU CHA DAR ES SALAAM

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli tarehe 27 Novemba, 2018 amefungua maktaba mpya, kubwa na ya kisasa ya Kikuu cha Dar es Salaam iliyojengwa katika Kampasi Mlimani (Mwl. Julius K. Nyerere) Jijini Dar es Salaam.
Maktaba hiyo kubwa Afrika Mashariki na Kati imejengwa kwa gharama ya shilingi Bilioni 93.6 ikiwa ni msaada kutoka Serikali ya China na inakuwa maktaba kubwa kuliko maktaba zote ambazo China imezijenga barani Afrika.
Katika taarifa yake Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam Prof. William Anangisye amesema majengo ya maktaba hiyo yenye ghorofa mbili yamechukua eneo lenye ukubwa wa meta za mraba 20,000 yakiwa na uwezo wa kuhifadhi vitabu 800,000, kukalisha watumiaji 2,100 kwa wakati mmoja, yana kompyuta 160 zilizounganishwa na mtandao kwa ajili ya kusoma vitabu kwa njia ya kielektroniki, ofisi za wafanyakazi, eneo la wanafunzi wenye mahitaji maalum na ukumbi wa kisasa wa mihadhara wenye uwezo wa kuchukua watu 600.
Prof. Anangisye ameishukuru Serikali kwa mchango mkubwa uliosaidia kufanikisha ujenzi wa maktaba hiyo, ameishukuru Serikali ya China kwa kutoa msaada wa fedha za ujenzi huo na kampuni ya ujenzi ya Jiangsu Jiangdu ya China kwa kujenga majengo yenye ubora na hadhi ya hali ya juu.
Ameahidi kuwa Jumuiya ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam itahakikisha majengo ya maktaba hiyo yanatunzwa vizuri na maktaba inatumika kuwanufaisha wanafunzi wa chuo hicho pamoja na wanafunzi wa taasisi zingine za vyuo na wananchi wa kawaida.
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako amemshukuru Mhe. Rais Magufuli kwa namna anavyotoa kipaumbele kwa sekta ya elimu na ameahidi kuwa wizara yake itaendelea kuhakikisha taasisi zote zilizo chini ya wizara hiyo zinaendeshwa kwa kuzingatia maadili na matumizi bora ya rasilimali, pia amemshukuru Balozi wa China hapa nchini Mhe. Wang Ke kwa kusimamia na kufuatilia kwa ukaribu ujenzi wa maktaba hiyo na kwa Serikali ya China kutoa shilingi Bilioni 50.8 kwa ajili ya ujenzi wa chuo cha elimu ya mafunzo ya ufundi stadi (VETA) Mkoani Kagera.
Akizungumza katika sherehe hizo Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli amemshukuru Balozi wa China hapa nchini Mhe. Wang Ke na kumuomba apeleke shukrani za Tanzania kwa Rais wa China Mhe. Xi Jinping kwa misaada ambayo China imekuwa ikiitoa kwa Tanzania, ikiwemo ujenzi wa Maktaba hiyo na Chuo cha VETA kitakachojengwa Mkoani Kagera.
Mhe. Rais Magufuli amesema urafiki wa China na Tanzania ulioasisiwa na Baba wa Taifa Hayati Mwl. Julius Kambarage Nyerere na Mwenyekiti Mao Zedong umeendelea kuleta manufaa makubwa na kwamba Serikali ya Awamu ya Tano na itauendeleza na kuukuza uhusiano na ushirikiano huu mzuri.
“Jambo la kufurahisha ni kwamba misaada yao haiambatani na masharti. Wenyewe wakiamua kukupa wanakupa, walitujengea TAZARA, URAFIKI na pia wametusaidia katika maeneo mengine ya maendeleo” amesema Mhe. Rais Magufuli na kumhakikishia Mhe. Balozi Wang Ke kuwa Serikali itahakikisha kila msaada unaotolewa unatumiwa vizuri.
Aidha, Mhe. Rais Magufuli amempongeza Rais Mstaafu wa Awamu ya Nne Mhe. Jakaya Mrisho Kikwete na Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam Mstaafu Prof. Rwekaza Mukandala kwa kuandaa mpango wa ujenzi wa maktaba hiyo, na pia amewapongeza Jumuiya ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kwa kupata maktaba ambayo itawasaidia kuongeza kiwango cha ubora wa elimu.
Amewataka wana Jumuiya ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kuhakikisha maktaba hiyo inatunzwa vizuri na ametoa wito kwa Watanzania kujifunza lugha ya Kichina katika jengo mojawapo la maktaba hiyo litakalokuwa likifundisha lugha hiyo kwa kuwa kuna manufaa makubwa kwa Watanzania kujifunza lugha hiyo.
Sherehe hizo zimehudhuriwa na viongozi mbalimbali wakiwemo Balozi wa China hapa nchini Mhe. Wang Ke, Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma, Mawaziri Wakuu Wastaafu Mhe. Jaji Mstaafu Joseph Sinde Warioba na Mhe. Edward Ngoyai Lowassa, Mawaziri, Mabalozi wa nchi mbalimbali na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Mhe. Paul Makonda.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
27 Novemba, 2018

MHESHIMIWA RAIS JOHN POMBE MAGUFULI NA MAMA JANETH MAGUFULI WAMESALI IBADA YA MISA TAKATIFU DOMINIKA 34 KATIKA KANISA LA MTAKATIFU PETRO PAROKIA YA OYSTERBAY, JIJINI DAR ES SALAAM, NOVEMBA 25, 2018

magufuli 1

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli na Mkewe Mama Janeth Magufuli wakiwa katika Ibada ya Misa Takatifu Dominika ya 34 ya mwisho wa mwaka katika Kanisa la Mtakatifu Petro Parokia ya Oysterbay, Jijini Dar es Salaam. Ibada hiyo ni mwisho wa mwaka ya sherehe ya Kristo Mfalme iliyoongozwa na Padre Projestus Marko Kahitwa.

magufuli 2

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akikomunika Ibada ya Misa Takatifu Dominika ya 34 ya mwisho wa mwaka katika Kanisa la Mtakatifu Petro Parokia ya Oysterbay, Jijini Dar es Salaam. Ibada hiyo ni mwisho wa mwaka ya sherehe ya Kristo Mfalme iliyoongozwa na Padre Projestus Marko Kahitwa.

magufuli 3

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli na Mkewe Mama Janeth Magufuli wakitoka kanisani mara baada ya kumalizika kwa Ibada ya Misa Takatifu Dominika ya 34 ya mwisho wa mwaka katika Kanisa la Mtakatifu Petro Parokia ya Oysterbay, jijini Dar es Salaam. Ibada hiyo ni mwisho wa mwaka ya sherehe ya Kristo Mfalme iliyoongozwa na Padre Projestus Marko Kahitwa. PICHA NA IKULU.

MHESHIMIWA RAIS JOHN POMBE MAGUFULI AWAAPISHA VIONGOZI SABA (7), IKULU, JIJINI DAR ES SALAAM, AZUNGUMZIA MSIMAMO WA MAUZO YA KOROSHO

 • Mheshimiwa Rais John Pombe Magufuli awaapisha viongozi saba mbalimbali ikulu, jijini Dar es Salaam, na azungumza na Watanzania juu ya msimamo wa mauzo ya zao la korosho

 • Katika hotuba yake, Mheshimiwa Rais aelezea jinsi alivyoumizwa na bei elekezi iliyotolewa na bodi ya korosho ambayo inawakandamiza wakulima wa korosho

 • Kwa maslahi ya wakulima, aamua kufunga mnada na mauzo ya korosho kwa kulinda maslahi ya wakulima

 • Afanya maamuzi ya mwisho kwa kununua korosho zote kwa kupiku bei zote zilizojitokeza kwenye manunuzi

 • Atimiza ahadi yake ya kulinda maslahi ya wakulima kwa kununua korosho kwa shilingi elfu tatu na mia tatu kwa kilo kabla hazijabanguliwa

 • Atoa maagizo kwa Mkuu wa Majeshi kulinda maghala yote yaliyo na korosho nchini na kuhakiki tani zote zilizomo ndani ya maghala hayo kabla ya korosho kuhamishwa

 • Aagiza wakulima wote wenye korosho zilizo hesabiwa ambazo zimo ndani ya maghala kulipwa pesa zao mara moja

 • Aagiza wakulima wakati wakiwa wanalipwa walipwe pesa zao zote kamili na wasikatwe pesa zao kwa deni lolote walilonalo liwe ni la pembejeo au madeni mengineyo

 • Aagiza pesa zitolewe kwa mfumo maalum wa kuwalinda wakulima ili wapate pesa zao zote, na baada ya malipo yao wakulima wenyewe watalipa madeni yao

 • Aagiza jeshi kusomba korosho zote zilizopo kwenye maghala husika baada ya uhakiki wa korosho maghalani na baada ya kukamilika kwa malipo yote ya wakulima

 • Aagiza korosho zote kupelekwa kwenye maghala maalum yaliyotengwa na jeshi kuhifadhia korosho hizo, na korosho nyingine kwa kiwango maalum kupelekwa kwenye kiwanda cha ubanguaji korosho kilichopo Lindi ambacho hivi karibuni kimerudi kwenye mikono ya serikali

 • Aagiza kuanzia leo kiwanda hicho cha ubanguaji korosho kuwa kwenye mikono ya Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) mpaka yatakapofanyika maamuzi mingine

 • Ahimiza wateule wote kuanza kazi zao za usimamizi leo

 • Azikemea vikali bodi za kilimo ambazo zisizo na usimamizi wa maslahi ya wakulima

 • Aendelea kusisitiza viongozi juu ya utekelezaji wa utumishi wa umma

 • Awapa nasaha Mheshimiwa Tizeba na Mheshimiwa Mwijage kwamba wasije watu wakawaambia sababu zingine za kutenguliwa uwaziri wao mbali na sababu alizozielezea yeye kwa Watanzania. Atoa shukran kwa Mheshimiwa Tizeba na Mheshimiwa Mwijage kwa kazi waliojituma katika kipindi chao

 • Aendelea kuweka msisitizo mkubwa juu ya viwanda vya ndani

 • Awapongeza na awashukuru viongozi mbalimbali waliohudhuria katika hadhara hiyo, na awaombea baraka wananchi wote kwa kusikiliza hotuba yake

magufuli 1magufuli 2