MHESHIMIWA RAIS JOHN POMBE MAGUFULI MGENI RASMI KWENYE SHEREHE ZA KILELE CHA MBIO ZA MWENGE, KUMBUKUMBU YA HAYATI MWALIMU JULIUS KAMBARAGE NYERERE NA MAADHIMISHO YA WIKI YA VIJANA KITAIFA

 • Mheshimiwa Rais John Pombe Magufuli mgeni rasmi kwenye sherehe za kilele cha mbio za mwenge, kumbukumbu ya hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na maadhimisho ya wiki ya vijana kitaifa

 • Katika sherehe hizo, Mheshimiwa Rais aliwasabahi viongozi wote waliofika kwenye sherehe hizo akiwemo mtoto wa Mwalimu, Mheshimiwa Makongoro

 • Mheshimiwa Rais awashukuru wakazi wa Zanzibar kwa mapokezi mazuri na awapongeza kwa maandalizi ya kupendeza

 • Awakumbusha wananchi malengo ya sherehe hizo ambayo ni kumbukumbu ya baba wa taifa na hivyo Tanzania itaendelea kumkumbuka baba wa taifa katika miaka mingi ijayo kama siyo miaka yote ya uhai wa taifa

 • Awakumbusha wananchi kujiuliza kama sherehe hizi zina akisi matendo ya baba wa taifa iwapo matendo yake hayafanyiwi kazi

 • Kwa umuhimu wa siku hii ya leo, Mheshimiwa rais aona ni muhimu kumzungumzia Mwalimu Julius Kambarage Nyerere kwa mchango wake mkubwa katika taifa, ili vijana na watoto wetu wapate kumjua na kuijua misingi ya taifa letu na wafuate nyendo zake; alikuwa ni mtu ambaye msomi lakini hana pesa kwasababu alisimama kwa maslahi ya Watanzania walio wengi

 • Leo si viongozi wengi wenye kufuata nyendo zake, alihoji Mheshimiwa Magufuli kwa kutupia masuali:

 • Leo ni viongozi wangapi waliajiriwa na taasisi za nje na kulipwa mshahara na kusaliti nchi yao?

 • Viongozi wangapi waliosaini mikataba isiyo na tija ya maslahi ya taifa?

 • Viongozi wangapi ambao wameweka pesa kwanza badala ya Tanzania kwanza?

 • Kwa busara kabisa alitupia maswali hayo kwa wananchi wayatafakari na wayajibu wenyewe

 • Aliendelea kumpamba Mwalimu kwa sifa ya ‘ukinai wa mali’ kwa kutolea mfano wa miaka 23 ya urais wa baba wa taifa kama angetaka kuchukua eneo la ufukwe wote wa bahari ya maeneo ya Msasani ili liwe lake, angefanya hivyo, lakini aliishi maisha ya kawaida na kusimamia maslahi ya Watanzania wote

 • Aliendelea na kutaja sifa za Mwalimu. Mwanzoni tu mwa gurudumu la maendeleo ya taifa katika uongozi wa Mwalimu, baadhi ya viongozi wasomi walitaka kuongezewa mishahara. Mwalimu alikemea matakwa hayo kifalsafa ya hali ya kuwa wakati Watanzania wengi walikuwa na hali ya chini na hawana uwezo wowote

 • Atupa suali lingine kwa kuakisi uzalendo wa baadhi ya viongozi kama wapo tayari kufuata nyayo hizo kwa manufaa ya Watanzania wote

 • Asema suali hili haimaanishi kwamba mishahara isiongezwe, la hasha! lakini uwezo wa serikali bado haujafikia kuwafikia Watanzania walio wengi katika jamii (kwa mantiki ya usawa)

 • Pamoja na hayo, alisema mfano mzuri visiwani Zanzibar ambapo wameongeza mishahara kutoka laki moja na nusu mpaka laki tatu kima cha chini kwa mwezi; na bara baada ya kazi kubwa iliyofanywa ya wafanyakazi hewa, kuanzia mwezi ujao mishahara itaongezwa na hii ni kutokana na uchambuzi wa kina na baada ya serikali kujiridhisha vya kutosha

 • Aliendelea kuelezea sifa za Mwalimu kuwa alikuwa ni mwenye kuhimiza umoja, amani na mshikamano. Pamoja na kuwa na makabila 121 na dini mbalimbali lakini aliwasihi watu kushikamana na kujenga umoja wa kitaifa

 • Mheshimiwa Magufuli alimuelezea Mwalimu kuwa ni mtu aliyependa muungano, amani na mshikamano. Pamoja ya kuwa alishapata uhuru wa Tanganyika, bila ya ubinafsi alisubiri nchi nyingine kama Kenya, Uganda na Zanzibar zipate uhuru ili ziwe nchi moja. Lakini (kutokana na tofauti za kisiasa), Mwalimu aliamua kuungana na Zanzibar kwa hekima zake na hekima za hayati Amani Abeid Karume na kuunganisha vyama vya ASP na TANU na kuzaliwa kwa Chama Cha Mapinduzi

 • Atupia tena suali kwa wananchi, je, ni wangapi wanaochochea uvunjifu wa amani nchini?

 • Wangapi wanaochochea muungano uvunjike?

 • Mheshimiwa rais akaendelea kuelezea maono ya baba wa taifa ya maendeleo ya nchi ambayo mikakati yake ilianza mwaka 1967 ya serikali kusimamia na kushikilia vyanzo vikuu vya uchumi kwa kuamini kwamba mafanikio ya uchumi wa taifa lazima vilevile yatokane na rasilimali za taifa kwa mfano viwanda ambavyo vilisaidia kupunguza kuagiza bidhaa kutoka nje, na mengineyo mengi aliyoyafanya wakati ule ili kuleta maendeleo nchini Tanzania

 • Atoa mfano baada ya taifa kuipa mgongo Azimio la Arusha, viwanda vingi vikabinafsishwa kutoka mikononi mwa serikali na matokeo yake viwanda na mashirika yote yakafa. Kwa mfano kiwanda cha Mwatex, Sunguratex, Tanganyika Packers, na kadhalika. Jumla ya viwanda 197 vimekufa

 • Ahoji kwanini tuliliacha Azimio la Arusha? wakati mbadala wake ndiyo ukapelekea mpaka wananchi wa hali ya chini kukosa nyumba nzuri ya kukaa

 • Aliendelea kumwagia sifa nyingi za kisiasa ndani na nje ya Tanzania katika jukwaa la kimataifa. Amwita mpigania uhuru, mwana jumuiya ya Afrika, mpenda amani, haki, umoja na usawa, rais wa TANU, waziri mkuu wa kwanza wa Tanganyika, rais wa jamhuri ya Tanganyika, rais wa kwanza wa jamhuri ya muungano wa Tanzania, mwenyekiti wa kwanza wa CCM, baba wa taifa letu

 • Asema Mwalimu alikuwa ni miongoni mwa viongozi bora kuwahi kutokea si nchini Tanzania tu, bali kwa bara la Afrika na duniani kwa ujumla. Kwa hivyo, ni muhimu watoto wetu wakajua fikra za Mwalimu na kuzifanyia kazi katika ujenzi wa taifa, “Nyerere oyee! Nyerere oyee! Tanzania oyee!” alisema Mheshimiwa Magufuli

 • Afafanua kwamba masuali aliyoyauliza na sifa alizozitoa za Mwalimu, siyo kwa makusudi ya kumtuhumu mtu yeyote, bali ni kuwapa taswira Watanzania wote popote pale walipo watafakari wapi tulijikwaa katika kuleta maendeleo ya taifa letu na watu wake

 • Asisitiza kwa kufuata nyayo za baba wa taifa, nchi yetu itapata maendeleo mazuri tena ya haraka

 • Asema siyo rahisi kuvaa viatu vya baba wa taifa, lakini angalau tuzitimize ndoto zake. Kwa mfano kuhamia kwa makao makuu Dodoma ambapo tayari waziri mkuu kishahamia, makamu wa rais anahamia mwaka huu na mheshimiwa rais kuhamia mwakani, na huku ndivyo kumuenzi baba wa taifa kwa matendo siyo kwa maneno

 • Kwa kufuata nyayo za waasisi wa serikali mbili, Mheshimiwa rais amesisitiza kuendeleza umoja, mshikamano na muungano na kudumisha amani

 • Atoa onyo kwa yeyote atakayejaribu kuvunja amani, muungano na mshkamano wa Watanzania, asema tutapambana naye kwa nguvu zote

 • Aelezea jinsi serikali mbili chini yake na chini ya Mheshimiwa Ali Mohammed Shein, zinavyoongeza bajeti ya maendeleo katika kufikisha huduma kwa wananchi wote

 • Aelezea maendeleo ya kasi yaliyofanywa na serikali yake na aelezea jinsi hatua zilizochukuliwa kupigana na vita vya kiuchumi na kulinda rasilimali za Watanzania, hatua ambazo zimepelekea kukuwa kwa uzalishaji wa madini kwa haraka

 • Ampongeza Mheshimiwa Shein kwa kukuwa kwa uchumi wa utalii Zanzibar na awapongeza Wazanzibar wote

 • Aelezea ukuwaji wa uchumi, ukuwaji wa ujenzi wa viwanda, kupigana vita vya rushwa na ubadhirifu wa mali ya umma

 • Awaomba Watanzania wote wavumilie katika kipindi hiki cha mpito na baadaye maisha yatakuwa mazuri

 • Asema, na hata kama maisha hayatakuwa mazuri kwa wakati wetu, watoto na wajukuu wetu ndiyo watakaofaidika na jitihada zinazofanywa sasa hivi na viongozi na awaomba Watanzania waunge mkono jitihada zinazofanywa na serikali

 • Akaendelea kuzungumzia historia fupi ya mwenge iliyoanzishwa na baba wa taifa alipokuja na fikra hiyo na kusimama kwenye bunge la wakoloni tarehe 22 Oktoba 1959 na kusema, “Sisi Watanganyika tunataka kuwasha mwenge, na kuuweka juu ya mlima wa Kilimanjaro, umulike hata nje ya mipaka yetu, ulete matumaini pale ambapo hakuna matumaini, upendo pale ambapo pana chuki, heshima ambapo pamejaa dharau.”

 • Mheshimiwa rais alisema, faida za mwenge wa uhuru ni:

 1. Kuchochea uhuru

 2. Kuunganisha Watanzania

 3. Alama ya uhuru na utaifa

 • Akaendelea kuzungumzia vijana na kuwaomba waipende nchi yao na wakae mbali na maasi mabaya

 • Atoa shukran kwa waandalizi wa sherehe, viongozi wa dini, usalama wa taifa, halaiki na vyombo vya habari

 • Akiwa kama Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi, awaomba viongozi kufuata maadili kwenye uchaguzi wa viongozi na awatakia uchaguzi mwema na awaomba kuchagua viongozi bora na wenye uwezo. Akaendelea kunukuu usia wa baba wa taifa (1985) ambaye alisema, “Bila ya CCM imara, nchi yetu itayumba.”

 • Mwisho akamalizia kwa kumnukuu tena baba wa taifa ambaye alisema, “Kizazi changu kiliongoza jitihada za kuleta uhuru wa kisiasa, kizazi cha sasa cha Waafrika, hakina budi kuchukua kijiti pale tulipoishia na kwa nguvu mpya kusukuma mbele maendeleo ya bara letu.”

 • Mheshimiwa Rais Magufuli akahimiza kizazi cha sasa kuyafanyia kazi maneno ya baba wa taifa ili kuleta mabadiliko ya kiuchumi

 • Aiombea Mungu familia ya baba wa taifa, familia ya Mzee Karume pamoja na waasisi wote na akamalizia kuuombea mwenge wa uhuru na vijana wa Tanzania na taifa la Tanzania

Advertisements