Ujumbe Wangu Kwa Watanzania Wenzangu – Uchaguzi 2015

UCHAGUZI 2015

Tarehe 25 Oktoba mwaka huu 2015, ndugu zangu Watanzania wenzangu wataenda kupiga kura kuchagua kiongozi wa kuongoza nchi na vilevile wataenda kuchagua chama tawala kitakachoendesha nchi katika awamu ya tano. Ningependa kuchukua fursa hii kwa ufupi na kwa maneno machache kutoa mchango wangu wa kinasaha na wa kifikra kwa wapendwa ndugu zangu na Watanzania wenzangu wote ambao watakaopata fursa ya kwenda kupiga kura ya mwaka huu 2015.

TUWE MAKINI – MAENDELEO HAYAJI USIKU MMOJA

Kiongonzi au Rais wa Tanzania wa kila awamu zilizopita wameleta maendeleo nchini katika nyanja walizojikita nazo katika nafasi zao na katika wasaa wao. Sote tunajua hakuna binaadamu aliyekamilika ila mwenyewe Mola muumba mbingu na ardhi. Na sote tunajua hakuna mtu anayependwa na watu wote, na ni sawasawa na kusema hakuna rais au kiongozi aliyepita katika hii dunia bila ya kuwa na wapinzani pamoja ya kuwa kiongozi au rais huyo ana mazuri anayoyafanya au aliyoyafanya kimaendeleo katika nchi yake ambayo pia mara nyingi hutokea hao hao wapinzani wake pia hufarijika na maendeleo hayo kwa njia moja au nyingine. Kiongozi yoyote au rais yoyote atakayekuja na listi au orodha kubwa ya mambo anayotaka kuyafanya yote peke yake katika kipindi chake, kiongozi huyo au rais huyo si muwazi na si mkweli kwa wananchi bali ana ajenda yake ya siri ili afike anapotaka, na pengine ni kwa faida yake binafsi. Na isitoshe, kiongozi yoyote au rais yoyote anayekuja kwa njia ya kulaghai wananchi kwa kuwaahidi kutenda orodha kubwa ya mambo, hajifanyii haki nafsi yake, haifanyii haki nchi yake na hata hafanyii haki wananchi wenzake, na badala yake kiongozi huyo mwishowe hujidhulumu nafsi yake, kwasababu kihali halisi maendeleo hayaji kwa msimu mmoja na hayaji kwa usiku mmoja. Mwanasayansi mmoja wa Uingereza bwana Isaac Newton alisema, “If I have seen further, it is by standing on the shoulders of giants”.

KIONGOZI, UPINZANI NA MAENDELEO

Kawaida wapinzani hutokea ndani na nje ya nchi pale kiongozi au chama tawala kinapowakilisha sera zake na kinapowakilisha maslahi ya nchi yake. Mfano wa marais au viongozi ambao walikuwa na mtazamo wa mbali wa maslahi ya nchi zao na kupata upinzani na changamoto za aina mbalimbali ni akiwemo baadhi yao baba wa taifa Julius Kambarage Nyerere, Abraham Lincoln, Fidel Castro, Winston Churchill, Mao Zedong na wengineo wengi waliopita. Waheshimiwa wote hawa niliowataja hapa kila mmoja wao alikuwa na mtazamo tofauti na mwengine kutokana na changamoto walizokuwa nazo katika wasaa wao na walipokuwa na nafasi zao, lakini pia haimaanishi kuwa hawakuwa na sera zenye maslahi yenye kunufaisha wapinzani wao waliogongana nao katika kipindi cha awamu zao. Waheshimiwa hawa na wengine baadhi yao walikuwa si watu wa kukurupuka kwenye maendeleo, bali walikuwa ni viongozi ambao wenye mipango, na mitazamo yao ilikuwa ni ya kuona mbali na ni yenye maslahi ya nchi zao ambazo nchi hizo ndio zinanufaika na kufaidika hivi sasa na nyingine nyingi zikiwepo njiani kunufaika kwa misingi iliyowekwa na viongozi hao, ndio maana nikasema ili twende mbele kimaendeleo lazima tukubali kuwa lazima wapinzani watakuwepo, na kuwa na wapinzani ni bishara nzuri, lakini kwa wapinzani wenye kutaka kheri kimaendeleo na si kwa upinzani wa kurudisha nyuma kimaendeleo au upinzani wa kuleta chuki katika jamii, kwani muhimu ni maendeleo kwa Watanzania wote na siyo kushikilia madaraka kinguvu au kuleta upinzani wa kinguvu ili muhimu tu mtu akae madarakani au ili muhimu mpinzani akae madarakani, hapa Watanzania wenzangu tuwe makini na tuwe waangalifu.

Hivi sasa tunaye kiongozi wa nchi yetu na rais wetu mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete ambaye karibu anamaliza muda wake. Katika hotuba zake mbalimbali zilizopita, nakumbuka alitaja moja ya malengo yake makuu ya maendeleo katika awamu yake, na katika wasaa wake na katika nafasi yake aliyokuwa nayo ni kuleta maendeleo katika sekta au nyanja ya Kilimo. Nakumbuka nilipokuwa shule ya msingi Bunge jijini Dar es Salaam tulikuwa tunafundishwa na kukumbushwa kuwa uchumi mkubwa wa nchi yetu Tanzania ni kilimo. Kila miaka ilivyokuwa ikipita nilipokuwa shule ya msingi, mara kwa mara nilikuwa nachungulia Atlasi ya dunia kuangalia ukurasa wa sehemu inayoonesha uchumi wa nchi mbalimbali za dunia, na hamu yangu kubwa ilikuwa ni kuangalia kama Tanzania uchumi wake umebadilika kuwa pengine kitu kingine badala ya kilimo. Lakini mwaka baada ya mwaka Atlasi nilizotumia zilikuwa zinaonesha Tanzania inategemea uchumi wake kwenye kilimo tu. Sekta hii ya kilimo, kwasababu mbalimbali ambazo wenye ujuzi wa kisiasa na kiuchumi wanazijua sababu hizo kwanini sekta hii haikuleta maendeleo yaliyotarajika, pengine kwa wakati ule kwa Watanzania. Lakini tunamshukuru Mungu, Alhamdulillah, Tanzania sasa Mwenyezi Mungu kaibariki kiuchumi, imekuwa na mali asilia mbalimbali kwa mfano madini ya kila aina, utalii unazidi kukuwa, wawekezaji wanazidi kuvutiwa na nchi yetu, na muda si mrefu uliopita, nchi yetu imepata barka nyingine ya kugunduliwa kwa gesi asilia, na vilevile baada ya ruhsa, njia nyingine nyingi za kiuchumi zilijitokeza ambazo zimenyanyua hali za watu wanaojituma kutafuta rizki zao za kila siku katika mfumo wetu wa kijamii ambao ni mbali na mali asilia, pia hali zao watu hao zimefungukiwa kwa kupitia mfumo wetu huo tuliokuwa nao wa kijamii. Isitoshe, siyo kama ilivyokuwa miaka ya themanini, hivi sasa wanafunzi wa shule ya msingi hawahitajii sana kutumia Atlasi ya kitabuni, ikiwa wataamua kufanya hivyo ili kujua hali ya uchumi wa nchi yao Tanzania, kwasababu profesa Google na profesa Bing wapo, na wanafunzi wanaweza kupata majibu ya mara moja kwenye tovuti zinazoaminika mtandaoni ikiwa watataka kujua uchumi wa nchi yao Tanzania ulivyokuwa, ulipo hivi sasa na nini mustakbali wa uchumi wa Tanzania ili waje kufaidika nao ufikapo wakati wao. Na hivi ndivyo hali inavyobadilika kiwasaa. Lakini kuna kazi kubwa bado inatakiwa kufanyika.

Hebu turudi tena kwenye Kilimo. Kama nilivyosema hapo awali katika makala hii kuwa rais Kikwete katika hotuba zake mbalimbali zilizopita alitaja moja ya malengo yake ya maendeleo katika wasaa wake, awamu yake na nafasi yake aliyokuwa nayo ni kuleta maendeleo katika sekta au nyanja ya kilimo ili kuimarisha kilimo na kufaidisha Wakulima na kuwa na hifadhi ya chakula ya kutosha kwa taifa. Sekta hii nina budi kusema ni sekta ambayo ilisahaulika lakini kama wazalendo wanavyosema ‘Mtoto wa mkombozi, ni mkombozi’, sasa ndio napata fahamu kujua kuwa ni kweli baba wa taifa aliona mbali kwenye sekta hii kuwa ni moja ya sekta yenye malengo makuu mawili, kuleta uchumi wa taifa kwa wakati ule mgumu na kwa wakati ujao, na pili ni kuondoa tatizo la chakula nchini. Bila ya shaka mheshimiwa Jakaya Kikwete katimiza ahadi yake na kwa wasaa wake katika sekta hii ya Kilimo, na hilo sisi Watanzania tumeliona na kushuhudia kuwa limefanyika na limepiga hatua kubwa kimaendeleo sambamba na wakati wake kama mheshimiwa rais alivyokusudia na mwishowe kugongelea msumari wa mwisho kabla ya kumaliza awamu yake kwa kufungua rasmi hivi majuzi benki maalum ya Maendeleo ya Kilimo na Wakulima Tanzania (bonyeza hapa) kwa maelezo zaidi. Na mafanikio yake katika sekta hii ya Kilimo imempelekea kupewa tuzo maalum kutoka kwa Baraza la Kilimo Tanzania juu ya maendeleo ya sekta hiyo nchini (bonyeza hapa) kwa maelezo zaidi.

Hakuna kiumbe aliyekuja duniani akamaliza kazi zake, hilo lazima tulikubali, ni sawasawa na kusema, hakuna kiongozi aliyekuja duniani akamaliza kazi zake (ingawa sera zake zinaweza kuwa zimekamilika au hazijakamilika, inategemea), lakini kawaida ya kiongozi huleta bishara ili watakaorithi na kufuata msimamo wa dira waendeleze maendeleo yaliyoanzishwa au yaliyokusudiwa kwa kupokea mwenge uliowashwa kuwa ndio kiangazo cha mustakbali wa walengwa au waliokusudiwa, na hapa namaanisha mustakbali wa Watanzania wa pembe zote nne za taifa hili adhim, kuanzia kaskazini mwake mpaka kusini mwake na kuanzia mashariki mwake mpaka magharibi mwake. Kwahivyo, tuweke maanani kwa kujua kuwa mheshimiwa rais wetu Jakaya Kikwete awamu yake ikiisha muda si mrefu kuanzia sasa ataondoka, na rais yoyote atakayemfuatia wa kutoka chama chochote Tanzania naye pia atakuja na ataondoka. Muhimu ni kufuata kiongozi mwenye msimamo ambaye wewe Mtanzania utakuwa na uhakika kuwa kiongozi huyu ni kiongozi mwenye msimamo mmoja, na ni kiongozi mwenye msimamo na dira ya sera zake, na ni kiongozi ambaye ni mchapa kazi na ni kiongozi ambaye ni mtekelezaji na si kiongozi mwenye kuyumbayumba kisha mbeleni akakuacha kwenye mataa.

Watanzania wenzangu, ningependa kuchukua fursa hii kuwaelezea umuhimu wa kumchagua rais atakayekuja kuongoza awamu ya tano. Sote pengine tunajua sifa gani zinazostahiki za kumchagua kiongozi au rais wa awamu ya tano sifa hizo kiongozi huyo awe nazo. Sifa zipo nyingi za kumchagua kiongozi au rais, lakini mfano mmoja wapo wa sifa hizo ni, Rais lazima awe ni mtu mwenye Maadili, vilevile awe ameonesha yale aliyoyafanya alipokuwepo katika uongozi wake uliopita au katika jamii, vilevile awe mtu asiye na Udini (lakini ni mtu mwenye kuheshimu dini zote) na awe mtu asiye na Ukabila (lakini ni mtu mwenye kuheshimu makabila yote) kwa kuzingatia kuwa wote Watanzania ni wamoja, vilevile awe mtu mwenye sera yenye dira na siyo sera hewa isiyo na mpangilio na isiyo na dira maalum, na sifa nyingine nyingi kadhaa wa kadhaa… kila mwananchi ana wajibu na ana haki yake mwenyewe kupekua na kuangalia kiongozi gani atakayefaa katika kuendeleza nchi hapa tulipofikia. Umuhimu wa uchaguzi wa mwaka huu 2015 ni muhimu sana! Umuhimu wa uchaguzi wa mwaka huu ni muhimu kuliko miaka 20 iliyopita ya uchaguzi wa vyama vingi nchini Tanzania. Niulize kwanini?

KURA YAKO 2015

Rais utakayempigia kura ya kumchagua kuongoza nchi yetu Tanzania miaka mitano ijayo ni muhimu kama ilivyo miaka kumi ijayo kuanzia sasa. Miaka kumi ijayo ni muhimu sana katika kuleta maendeleo ya kijamii kwa kuutokomeza umaskini kwa wananchi wa Tanzania, na vilevile miaka mitano na miaka kumi ijayo ni muhimu sana katika kujenga miundo mbinu ili Tanzania iende sambamba na nchi zinazokuwa kwa kasi kiuchumi duniani na kama vile yenyewe jinsi inavyokuwa kwa kasi kiuchumi ili miundombinu hiyo iendelee na izidi kuvutia wawekezaji nchini na kukuza hali za kimaisha za Watanzania kwa ujumla na kuielekeza nchi yetu kwenye ile dira inayojulikana kitaifa kama ni dira ya ‘Vision 2025’ ya kutokomeza umaskini nchini, ambayo imebaki miaka kumi ijayo kuanzia sasa. Mtanzania mpiga kura mwaka huu 2015 unajukumu kubwa la kutambua kuwa kila kura yako ina ‘nguvu’ ya kuchagua chama kitakachotawala, ambayo pia itakayopelekea kuchagua rais au kiongozi atakayetupeleka kufikia malengo yaliyowekwa ya mwaka 2025, kura hii siyo kura ya usanii, kura hii siyo kura ya vichekesho vya jukwaani, kura hii ya mwaka huu siyo ya kukurupuka kama inavyofuatwa ngoma ya mdundiko na vishindo vyake mitaani, kura hii ni kura ya ‘dira ya taifa’, kura hii ni kura ya mustakbali wa Watanzania wote, kura yako pigia chama chenye mustakbali. Ndugu zangu Watanzania tukumbushane kuwa mdundiko mwisho wake ngomani, usiku wake kila mtu mchagoni, ifikapo asubuhi badala ya kuona jua linachomoza machoni, badala yake utaliona jua linazama machweoni, ndipo utakapojua na kujiuliza kwani kunani? Kwa mara nyingine tena, tuwe makini!

UMOJA, UTULIVU NA AMANI

Ikiwa awamu ijayo (awamu ya tano) tunaona ni muhimu kwa Watanzania, basi tuijenge na tuipandikize nguzo hii ya tano kwenye msingi ule ule madhubuti uliyojengwa hapo awali, nao ni msingi wa ‘Amani.’ Watanzania wapiga kura wana khiyari siku hiyo ya kupiga kura ya tarehe 25 Oktoba 2015, na vilevile wana khiyari kwa siku zifuatazo baada ya siku ya kupiga kura ya tarehe 25 Oktoba 2015, khiyari yenyewe ni aidha tuijenge nchi yetu sote kwa pamoja kwa utulivu na amani, au tufuate wito wa ngoma itakayopigwa mitaani yenye kuvunja utulivu na amani. Hii ni khiyari yetu na kila khiyari ina natija yake na ina matokeo yake. Ikiwa kama ni Mtanzania, nikae chini nijiulize ikiwa kama simo kwenye kitabu cha kupiga kura (BVR) na umri na haki zote za kupiga kura zinaniruhusu, lakini sijajiandikisha na simo kwenye kitabu cha kupiga kura ambayo ndiyo silaha yangu ya kumchagua kiongozi ninayemtaka, Je? bado nina haki ya kuwavunjia utulivu na amani wananchi na Watanzania wengine wanaopenda utulivu na amani nchini? Ni kama kusema nimo lakini simo! Hivi nahisi ni kinyume, na kama nimekosea hapa nisawazisheni na nisameheni. Na hata kama Mtanzania upo kwenye kitabu cha kupiga kura (BVR) na ukaenda kupiga kura kwa kutarajia kwamba kura yako ndiyo haki yako, basi kwani kura ya mwenzako siyo haki yake? Nahisi kwenda kinyume na kupinga matokeo ya kura kwa kunadi zahma na fujo mitaani, ni kusababisha hatari kwa usalama wa taifa, basi ni bora kuliepuka hilo na kukubali matokeo na kufuata mkondo wa sheria. Kwani nafuata msemo wa wazee wetu waliosema, “Mjenga nchi ni mwananchi” basi vilevile itakuwa “Mvunja nchi…”

Ndugu zangu Watanzania wenzangu, ningependa kuuelezea umoja, amani na utulivu kwa njia ya kitamthilia kama ifuatavyo:

UMOJA

Umoja, utulivu na amani hauji bila ya watu kushirikiana na kuwa pamoja na kuwa na malengo yao pamoja. Ingawa watu wanaweza wakatofautiana kifikra na kiitikadi, lakini lazima kuwe kuna chombo chenye kuwakilisha na kuwa kama ndiyo nguzo za umoja wenye kukusanya fikra endelevu, fikra zilizokhitilafiana na fikra zenye kuleta mutafaruk, ili ziweze kusimamiwa na kutatuliwa na chombo cha umoja huo ili nyumba hii ya amani isiyumbeyumbe na mpaka kuwafikia mashabiki ambao mara nyingine huwa wanataka kuicheza ngoma hata kama ngoma sio yao. Umoja na ushirikiano juu ya utulivu na amani ni muhimu kwa watu wote hata kama wana mitazamo tofauti au itikadi zao zikiwa tofauti.

AMANI

Neno ‘Dar’ maana yake ni ‘Dari ya nyumba au nyumba yenyewe.’ Nyumba yoyote lazima iwe na dari au ‘ceiling’ kuwa ndiyo ngao ya kuwalinda wanaoishi kwenye nyumba hiyo kwa majira yote na kwa hali yoyote. Lakini ngao hiyo haisimami bila ya kuwa na nguzo imara na bila ya kuwa na msingi imara wenye kusimamisha dari hiyo. Na msingi wa Tanzania ndiyo ‘Amani.’

UTULIVU

Neno ‘Salaam’ maana yake ni ‘Usalama’ vilevile unaendana na neno ‘Utulivu.’ Nyumba ikiwa imeezekwa vizuri, nguzo zake ni imara na msingi wake ni mzuri na imara basi ndani ya nyumba hiyo hupatikana utulivu na usalama. Nyumba yoyote ikiwa kama msingi wake haupo imara, na nguzo zake haziko imara basi kuweni makini ya kwamba nyumba hiyo itayumba tu! Na kuyumba huko kunaashiria kwa Tanzania nzima.

MAMA TANZANIA

Ingawa niko mbali sana, maili elfu na mia

Mimi ndiyo wako mwana, moyoni mwangu umeenea

Kwa tabu na huruma, sisi na wazazi umetulea

Mpaka leo tumesimama, tunaweza kujitegemea

Tanzania wewe ndiyo mama, amani nakuombea

Yaliyojiri yamejiri na yaliyotokea yametokea

Hapa tulipo ni majaali, muhimu huko tunapoelekea

Si mbali nawe kwa khiyari, bali ni hali ya dunia

Leo ikinikuta hali, kwako ndiyo nakimbilia

Tanzania wewe ndiyo mama, amani nakuombea

Tangu chama kimoja, mpaka sasa demokrasia

Hongera baba wa taifa, busara kutuletea

Mwinyi, Mkapa na Kikwete hawa ndiyo wameshika njia

Nchi yetu imenawiri, nchi yetu imeendelea

Tanzania wewe ndiyo mama, amani nakuombea

Kiongozi mrithi wao, yoyote atakayewajia

Awe mwenye ufunguo, afungue ya wapita njia

Afuate muelekeo wao, maisha mema kutuletea

Atuletee mafao, na Mungu atajaalia

Tanzania wewe ndiyo mama, amani nakuombea

Mapinduzi na umoja, tangu sitini na moja

Nyerere na Karume, tangu sitini na nne

Dini, ukabila na rangi, isiwe ndiyo sababu

Watanzania wote ni wamoja, tangu enzi za mababu

Tanzania wewe ndiyo mama, amani nakuombea

Mwanza, Lindi na Mbeya, Arusha, Tanga na Songea

Amani tunakuombea, kwa nzuri yetu nia

Kigoma, Tabora, Dar Salama, Unguja na Pemba Chakechake

Ewe Mungu ibariki, Tanzania na watu wake

Tanzania wewe ndiyo mama, amani nakuombea (Amin)

MWISHO WA MWANZO

Kwa kumalizia ujumbe wangu huu, Watanzania tuna khiyari ya kidemokrasia kuchagua chama tawala na kiongozi atakayetuongoza katika awamu ya tano, kwa kutumia haki na mfumo maalum wa kupiga kura wa kisasa (BVR) uliowekwa na uliyokubalika na vyama vyote nchini ambao utakaosimamiwa na kamati iliyoundwa ya kupiga kura ifikapo siku hiyo ya kupiga kura ya tarehe 25 Oktoba 2015. Ujumbe ni kwamba, kura yako ya tarehe 25 Oktoba 2015 ni kura ambayo ina bashiria chama tawala na vilevile kura yako ndiyo ina bashiria kiongozi atakayeiongoza nchi yetu Tanzania kwa miaka mitano na miaka kumi ijayo, kumbuka kuwa kwa yoyote utakayembashiria wewe kwa kiganja chako ambaye unahisi kuwa atafikia malengo ya ‘Vision 2025’, kabla hujabashiria huko kwa kupigia kura chama gani kitatawala na kiongozi gani ataongoza miaka mitano ijayo, kwanza lazima ujiulize “Who will guard the guardian?”

Samahani kama nimekosea.

Ndugu yenu mpendwa.

Saleh Jaber

06 Septemba 2015