MHESHIMIWA RAIS JOHN POMBE MAGUFULI AONGOZA BARAZA LA BIASHARA TANZANIA, AWAHAKIKISHIA WAFANYABIASHARA TANZANIA SALAMA CHINI YA UONGOZI WAKE, WAFANYABIASHARA WAFURAHISHWA NA HALI YA USALAMA NCHINI, WAPONGEZA UONGOZI WA MHESHIMIWA RAIS MAGUFULI, WATOA CHANGAMOTO MBALIMBALI, MHESHIMIWA RAIS MAGUFULI AWEKA UZITO MKUBWA KWENYE KUSISITIZA VIWANDA VYA NDANI NA MATUMIZI YA BIDHAA ZA NDANI

Advertisements

MHESHIMIWA RAIS JOHN POMBE MAGUFULI AWEKA JIWE LA MSINGI LA AWAMU YA PILI YA MRADI WA RELI YA TRENI YA KISASA KUTOKA MOROGORO MPAKA DODOMA

 • Mheshimiwa Rais John Pombe Magufuli aweka rasmi jiwe la msingi la awamu ya pili ya ujenzi wa reli ya treni za kisasa kutoka Morogoro mpaka Dodoma
 • Katika hotuba yake, Mheshimiwa Rais atambua uwepo wa Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mheshimiwa Makame Mbarawa, Waziri Mkuu, Mheshimiwa Kassim Majaliwa, Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Waziri Mkuu mstaafu, Pinda Mizengo, Waheshimiwa Mawaziri, Mheshimiwa Mahenge, Makatibu Wakuu, Wakuu wa Mikoa, Waheshimiwa Wabunge, Mheshimiwa Balozi wa Uturuki, Eralp, Mheshimiwa Balozi wa Uingereza Sarah Cooke, Wakuu wa Jeshi la Ulinzi na Usalama, IGP, Mkurugenzi, Kamishna Jenerali wa Magereza, Kamishna Jenerali wa Uhamiaji, Mkuu wa Takukuru, Viongozi wa JKT, muwakilishi wa Benki ya Dunia, Viongozi wa Shirika la Reli Tanzania, John Kondoro na Masanja Kadogosa, Viongozi wa Serikali, Mheshimiwa Mangula, Viongozi wa Vyama vya Siasa, Viongozi wa Taasisi za Dini, Viongozi na Wafanyakazi wa kampuni ya ujenzi wa reli ya Yapi Merkezi ya Uturuki, Wafanyakazi wa Shirika la Reli, Wananchi, na Waandishi wa Habari
 • Amshukuru Mwenyezi Mungu na ashukuru uongozi wa ujenzi wa reli kwa kualikwa kwa mara ya pili kuweka jiwe la msingi la ujenzi wa reli wa kihistoria nchini Tanzania, kutoka Morogoro hadi Dodoma yenye urefu wa kilomita 426. Pia awashukuru wakazi wa Ihumwa kwa mapokezi mazuri na awaahidi kuwatengenezea barabara ya kiwango cha lami kutoka Ihumwa kuungana na barabara kuu
 • Amuagiza Waziri wa Ujenzi kuanza kazi hiyo mara moja ili wakazi wa Ihumwa wapate kunufaika na maendeleo ya nchi yao, na pia waitumie barabara hiyo kukuza uchumi wao. Mheshimiwa Rais aliwafurahisha wakazi wa Ihumwa baada ya kuwafanyia dhihaka ya kitani ambayo iliitikiwa kwa kishindo kikubwa cha furaha na wakazi wa Ihumwa, Dodoma
 • Aainisha umuhimu wa miundombinu katika maendeleo ya nchi, ambayo miundombinu hyo ndiyo changamoto kubwa katika bara la Afrika kwenye sekta ya usafiri kukosekana na uimara wa miundombinu na usafiri wa uhakika, na kusababisha gharama za usafiri kuwa juu ukilinganisha na nchi nyingine duniani
 • Asema kutokana na tafiti, gharama za usafirishaji kontena moja la futi 20 kwenye nchi za Afrika Mashariki kwenda umbali wa kilomita 1500 ni dola 5000 za Marekani. Bei hii ni sawa na kusafirisha kontena lenye ukubwa sawa na huo (futi 20), kutoka China hadi Tanzania ambao umbali wake ni kilomita 9000 ukilinganisha na kilomita 1500 inayosafirishwa ndani ya Afrika Mashariki kwa bei hiyo hiyo
 • Aelezea miundombinu dhaifu ya usafiri inachagia katika kushusha mapato ya nchi za Afrika kwa asilimia 1%-2% na kuongeza gharama za usafirishaji kwa asilimia 40% na kusababisha nchi za Afrika kushindwa kushindana kiuchumi na nchi za mabara mengine katika masuala ya biashara, uwekezaji, na viwanda, na hivyo, afurahishwa uongozi wake kuitatua changamoto hiyo kwa kujenga miundombinu kama hiyo ya reli ya kisasa kwa kutumia pesa za ndani
 • Aainisha kwamba kuna njia nne kuu za usafiri. Usafiri wa anga, maji, barabara, na reli ambayo utafiti unaonesha, usafiri wa reli ndiyo usafiri bora, wa haraka, na wa salama katika kusafirisha shehena kubwa za mizigo na abiria. Usafiri wa reli una faida kubwa
 • Aelezea kutokana na ripoti ya Benki ya Maendeleo ya Afrika (2015) usafiri wa reli ni muhimu, ni muhimili mkubwa kwa maendeleo ya kiuchumi. Na endapo Afrika haitaboresha na kuimarisha usafiri huu, haitaweza kutumia rasilimali na utajiri uliyo nao
 • Aelezea miundombnu ya reli iliyopo hivi sasa ya reli ya kati iliyojengwa na wakoloni kwenye miaka ya 1896 hadi 1929, na reli ya TAZARA iliyojengwa na Wachina kwenye miaka ya 1970. Aainisha utendaji wa kazi wa treni hizi si wa kuridhisha kutokana na uwekezaji mdogo, na miundombinu chakavu, na uchakavu wa vitendea kazi, na uongozi uliokuwepo. Aupongeza uongozi uliopo hivi sasa wa kuchukua hatua za kuimarisha na kuboresha usafiri wa treni hizo, hususan reli ya kati, ambazo hivi sasa mafanikio yake yanaanza kuonekana
 • Asema ujenzi wa reli hii ya kisasa ambayo itatumia umeme na mafuta ya dieselutaongeza tija na ufanisi katika usafiri wa reli nchini ambayo faida zake ikiwemo kurahisisha usafiri wa abiria na mizigo. Treni za kisasa zitakuwa zinakimbia kwa kilomita 120 kwa saa kwa treni za mizigo, na kilomita 160 kwa saa kwa treni za abiria. Kwa hivyo, mtu anayesafiri kutoka Dar es Salaam mpaka Dodoma atatumia masaa matatu tu ya safari yake, wakati hivi sasa hutumia wastani wa masaa 11 kwa reli na masaa matano mpaka 6 kwa kutumia gari. Pia, mtu atakayesafiri kwenda Mwanza, atatumia masaa 9 badala ya masaa thelathini na sita kwa kutumia usafiri wa reli iliyopo
 • Aelezea jinsi reli mpya ya kisasa itakavyo chochea uchumi wa Tanzania na uchumi wa nchi za jirani kwa kutumia bandari ya Dar es Salaam. Reli ya kisasa itaweza kusafirisha tani milioni 17 kwa mwaka badala ya tani milioni 5 ambazo zinasafirishwa sasa. Pia aelezea umuhimu wa reli utakavyoongeza uhai wa barabara za lami. Aainisha reli mpya itakuwa na uweza wa kubeba tani 10000 kwa mpigo ambayo ni sawa na magari makubwa 500 ya mizigo yenye kubeba tani 200 kila moja
 • Asema mbali na usafirishaji mizigo na abiria, maeneo ya sekta zingine pia zitakuwa kiuchumi ikiwemo kilimo, utalii, ufugaji, uvuvi, viwanda, madini, na kadhalika, ambayo ni vigumu kukuza sekta hizi kiuchumi bila ya kuwa na miundombinu ya uhakika. Aliongeza kwa kusema, ujenzi wa reli ya kisasa, utatoa ajira takriban 30000 za moja kwa moja na ajira 600000 zisizo za moja kwa moja
 • Aelezea jinsi Tanzania itakavyofaidika na ukubwa wa idadi ya watu wake kiuchumi katika kufanya kazi na kuleta maendeleo ya nchi yao. Atoa mifano mbalimbali ya nchi nyingine ambazo zimefaidika na rasilimali za watu wake na kuwezesha kuwa mataifa tajiri na yenye kutoa misaada nje ya nchi zao na awatoa hofu wananchi kuwa na idadi kubwa ya watu nchini, lakini awasihi kuchapa kazi au vyuma vitabana tu
 • Aelezea umuhimu wa nchi serikali kuhodhi njia kuu za uchumi kama njia za usafiri wa reli, bandari, nishati, barabara, mawasiliano, maji, na kadhalika. Atoa mfano reli ilipobinafsishwa na makampuni binafsi kutoka nchi za nje, hakuna chochote kilichofanyika cha kuleta maendeleo ya reli hiyo pamoja na kuitumia reli hiyo kwa miaka zaidi ya 5 kuwa kwenye kutoa huduma
 • Mheshimiwa Rais aweka wazi kwamba njia ya mnyonge ni yeye mwenyewe kuisimamia na kuijenga reli ya kisasa kwa pesa yake mwenyewe, akimaanisha pesa za ndani, pesa za serikali ya Tanzania anayoiongoza, pesa za walipa kodi. Ni hali ambayo nchi nyingi zimeshindwa kufanya hivyo kwa kutumia pesa zao wenyewe au kwa kukopa kwa masharti magumu. Atoa wito kwa Watanzania wote popote walipo wajisifu na kushangilia ukombozi huu wa reli mpya ya kisasa unaoongozwa na serikali yake ya awamu ya tano
 • Awapongeza Watanzania wote wa dini zote na wa vyama vyote kwa ushirikiano wao kufanikisha mradi huu kutokana na kodi zao ambazo zimekusanywa vyema na serikali. Aainisha mbali na mradi wa reli ya kisasa ambao utatoa ajira ya watu laki sita, pia kuna mradi mwingine ambao unasimamiwa na serikali wa bomba la mafuta kutoka Hoima, Uganda mpaka Tanga, Tanzania, ambazo ajira zake zitanufaisha Watanzania 15000 moja kwa moja mbali na wafaidika wengine ambao wataingiliana na mradi huo kwa njia moja au nyingine
 • Mbali na miradi hiyo, kuna mradi mkubwa utakoajiri zaidi ya watu 20000 utakaogharimu zaidi ya shilingi trilioni 6 za Tanzania, mradi wa umeme wa Steigler’s Gorge ambao upo njiani utakaotoa umeme wa zaidi yamegawatts 2100 ili uongeze nguvu ya umeme na kutoa umeme wa uhakika katika kutimiza ndoto ya baba wa taifa Mwalimu Nyerere na kutimiza dira ya serikali ya awamu ya tano ya uchumi wa viwanda ili iwe chachu kwa Tanzania iweze kushindana kiuchumi kimataifa
 • Mbali na miradi hiyo, kuna miradi mingine ambayo inaendelea ya mabarabara makubwa na barabara ndogo, viwanja vya ndege, barabara za juu (flyovers). Kutokana na takwimu, miradi hii peke yake imeajiri zaidi ya watu milioni moja, alisema Mheshimiwa Magufuli
 • Akaongezea kuainisha kuwa kuna miradi mingi ikiwemo miradi ya umeme ya vijijini ambayo ikifika mwaka 2021 vijiji vyote vitakuwa vishapata umeme, na miradi ya maji ambayo inatoa ajira kwa Watanzania na inaibadilisha sura ya nchi kuelekea Tanzania mpya kwa vitendo
 • Atoa wito kwa Watanzania kufanya kazi na kuchukua fursa ziliopo. Aahidi kila siku kuwaambia Watanzania ukweli na akasisitiza kwa msemo wake maarufu ‘asiyefanya kazi na asile’ na ‘asiyekula afe’ na hii ndiyo lugha ya ukweli. Awapongeza Watanzania kwa kuchapa kazi na kuleta mafanikio nchini na kuifanya Tanzania kuwa nchi ya mfano. Atoa wito kwa Watanzania kuvipenda vyao, alisema Mheshimiwa Rais Magufuli
 • Aelezea kwamba uongozi wake unaleta mabadiliko na maendeleo nchini ni kwa manufaa ya vizazi vijavyo ili waikute Tanzania yenye neema, yenye kupendeza, na yenye viwanda vingi
 • Asisitiza wanaosimamia ujenzi wa reli ya kisasa ya awamu ya pili kukamilisha ujenzi kwa wakati, na afurahishwa na maendeleo ya ujenzi wa awamu ya kwanza kwa kuendelea vizuri kutokana na kuwa na changamoto huko mwanzoni. Aelezea umuhimu wa reli ya kisasa ikikamilika itakavyorahisisha usafiri wa watu baina ya Dar es Salaam na Dodoma
 • Ahimiza Watanzania kuendelea kulipa kodi ili kuleta maendeleo ya nchi yao wenyewe. Awaasa wale ambao wanaotoa risiti ya bei tofauti na thamani ya bidhaa kuwacha mara moja. Pia awataka TRA kuangalia kodi wanazozitoza kwa watu kutokana na vipato vya biashara zao. Isiwe badala ya kuwasaidia kiuchumi ili waweze kulipa kodi stahiki, inakuwa kero kero kwa walipa kodi na badala yake kuwafanya kutafuta mbinu nyingine za kuzikwepa kodi. Awataka TRA kujipanga kwenye kutoza kodi na awataka viongozi wa TRA kusimamia hilo
 • Aainisha kwamba awamu tano za mradi wa reli ya kisasa utagharimu shilingi trilioni 15 za Tanzania. Mbali na mradi wa reli, kuna barabara zitatengenezwa mjini Dodoma, upanuzi wa bandari ya Dar es Salaam, Mtwara, na Tanga, ununuzi wa meli kubwa ya ziwa Victoria, ukarabati wa viwanja 11 nchini, na ujenzi wa uwanja wa ndege wa kimataifa wa Dodoma, ununuzi wa ndege sita kwa mpigo, mradi wa Stiegler’s Gorge, na utekelezaji wa awamu ya tatu ya kupeleka umeme vijiji vyote nchini, na miradi ya kupeleka maji vijijini, na elimu bure kwa shule za msingi mpaka za sekondari, na huduma za afya ikiwemo vituo vya afya na madawa
 • Atoa wito kwa taasisi kutoa na kupokea risiti kila panapofanyika miamala ya manunuzi na mauzaji, atoa wito kwa wakuu wa magereza kuhamasisha kilimo kwa wafungwa kwenye magereza ili waweze kujikidhi milo yao, na atoa wito kila kiongozi kwenye eneo lake kusimamia mantiki ya magereza. Asisitiza amani nchini Tanzania na avipongeza vyombo vya ulinzi na usalama kwa kuendelea kusimamia na kuimarisha amani nchini
 • Atoa wito kwa wakazi wa Dodoma kwa ujumla kuchangamkia fursa za kiuchumi. Agusia maendeleo ya uwanja mkubwa wa mpira utakaojengwa mjini Dodoma. Agusia mustakbali wa viwanda mbalimbali vitakavyowekezwa na taasisi za mifuko ya hifadhi ya jamii
 • Amshukuru Mheshimiwa Waziri kwa mualiko na asisitiza mradi kukamilika kwa wakati. Awashukuru wakazi wa Dodoma na wana Ihumwa, viongozi wote waliohudhuria katika hafla hiyo. Amshukuru Mheshimiwa Naibu Spika, na Waheshimiwa Wabunge kwa kupitisha bajeti ya ujenzi wa reli ya kisasa na awahakikishia Wabunge kwamba serikali ya awamu ya tano ipo pamoja nao na awasihi kuendelea kutoa ushauri mzuri na kuchapa kazi kwa ajili ya Tanzania
 • Mwisho, awahakikishia Watanzania wote atawasimamia maslahi yao bila ya kuwabagua vyama vyao, dini zao, makabila yao au maeneo yao, na asisitiza kuwa maendeleo hayana vyama. Akaendelea kuwashukuru wana Ihumwa na waimbaji wa Tanzania All Stars. Akaiombea Ihumwa, akauombea mradi wa reli ya kisasa na wafanyakazi wake, na akawaombea Mungu Watanzania wote baraka

https://youtu.be/SD3t21qCsaY