MHESHIMIWA RAIS JOHN POMBE MAGUFULI AENDELEA NA ZIARA YAKE YA KIKAZI JIJINI MWANZA, AZINDUA VIWANDA MBALIMBALI, ATOA WIKI MBILI KWA WASIOENDELEZA VIWANDA

  • Mheshimiwa Rais John Pombe Magufuli aendelea na ziara yake ya kikazi jijini Mwanza kwa kuzindua viwanda mbalimbali jijini humo. Atoa wiki mbili kwa wasioendeleza viwanda viwanda ambavyo vilitakiwa viwe vinazalisha bidhaa, vitoe ajira na kupatia serikali mapato

  • Katika hotuba yake alipokuwa mjini Igogo, Mwanza, Mheshimiwa Rais alifurahishwa kufanya ziara hapo kwasababu mjini hapo ana historia napo na aliwahi kuishi katika kipindi cha maisha yake

  • Asifia eneo la Igogo lilivyokuwa na viwanda vingi wakati huo ambavyo sasa hivi havipo

  • Akipongeza kiwanda cha Victoria Moulders na mkurugenzi wake kwa kuzalisha bidhaa za kuuza ndani na nje ya nchi, kutoa ajira na kulipa kodi kwa mapato ya taifa

  • Amshauri aangalie maslahi ya wafanyakazi wake, na kwa upande wake atashughulikia changamoto za umeme zilizojitokeza na kuhakikisha kuendelea kupata umeme wa uhakika

  • Awashukuru wakazi wa Mwanza na atoa mchango wa milioni tatu kama sadaka yake kwa shule mbili za sekondari za eneo hilo na aahidi atafanya ziara nyingine kuangalia jinsi pesa zilivyotumika katika shule hizo

  • Awashukuru viongozi wa dini, waandishi wa habari na asisitiza amani nchini

  • Atoa mchango mwingine wa milioni moja kama sadaka yake kwa ajili ya ofisi ya tawi la Chama Cha Mapinduzi, kata ya Igogo, na akaendelea kuhamasika kutoa mchango kwa vyama vingine vya kisiasa papo kwa papo, lakini baada ya kuuliza, kulikuwa hakuna muwakilishi wa kupokea sadaka hiyo kutoka kwenye vyama vingine vya kisiasa

  • Mwisho akawashukuru wananchi na kuwaombea Mungu

MHESHIMIWA RAIS JOHN POMBE MAGUFULI AFUNGUA DARAJA LA FURAHISHA NA VIWANDA MBALIMBALI KATIKA ZIARA YAKE YA KIKAZI, JIJINI MWANZA

  • Mheshimiwa Rais John Pombe Magufuli amefungua rasmi daraja la Furahisha na azindua viwanda mbalimbali vilivyopo jijini Mwanza katika ziara yake ya kikazi

  • Katika moja ya hotuba zake, Mheshimiwa Rais amemshukuru Mwenyezi Mungu na awashukuru wakazi wa Mwanza kwa kumuamini na kumchagua kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

  • Mara baada ya shukran hizo, baraka za mvua fupi zilipita katika hadhara hiyo na mheshimiwa rais akawauliza wananchi kuwataka ushauri kama aendelee na mkutano huo au aghairi kwa kutaka ridhaa zao kumsikiliza huku wakiwa mvuani; lakini kwa kishindo kikubwa wananchi waliitika aendelee na hotuba yake na kumpa baraka zote pamoja na mvua ikinyesha

  • Awahakikishia wana Mwanza na Watanzania kwamba ameyaona mabango yao na amezisikia kero zao vizuri, na ataelekea Bukoba na Uganda katika kuweka jiwe la msingi la bomba la mafuta la kutoka Hoima hadi Tanga

  • Awaelezea wana Mwanza jinsi Mwanza ilivyokuwa na utajiri wa viwanda, kwa mfano, kilipokuwa kiwanda cha Mwatex, kiwanda cha pamba, kiwanda cha ngozi na mambo mengineyo ya maendeleo yaliyokuwepo ambayo hivi sasa hayapo

  • Awasihi wananchi wa rika zote waangalie wanapotoka na wajiulize maswali ya maendeleo yao na ya nchi yao

  • Ahimiza kujengwa viwanda ili vitoe ajira kwa wananchi na serikali kukusanya kodi yake ya mapato

  • Ampongeza Mheshimiwa John Mongellah kwa kufuata dira ya rais ya ujenzi wa viwanda jijini Mwanza

  • Ahoji iweje Tanzania iweze kuzalisha pamba halafu wananchi wake wavae mitumba; afafanua kwamba isitafsiriwe vibaya na hamaanishi kuwa mitumba isiuzwe, lakini ataka viwanda vya ndani viweze kuzalisha nguo za bei ya chini ili wananchi wawe na uchaguzi wa nguo mpya badala ya nguo za mitumba

  • Awataka Watanzania waendelee kumuunga mkono katika ujenzi wa viwanda ili kila Mtanzania afaidike na mazao ya Tanzania ya viwanda na serikali ipate kodi yake

  • Aitaka Mwanza na Tanzania nzima iwe ya viwanda kutoa ajira. Akatoa mfano mkoa wa Pwani hivi sasa in viwanda 371 vikiwemo 89 viwanda vikubwa. Amtaka Mheshimiwa Mongellah kuendelea na juhudi za ujenzi wa viwanda jijini Mwanza

  • Ampongeza Mheshimiwa Charles Mwijage kwa kutekeleza maelekezo ya viwanda vilivyokuwa vimesuasua kuwapa watu wengine kuviendeleza badala ya kukaa bila ya kuzalisha. Akaongeza kwa kusema, amewataka wenye viwanda ambao wamehodhi  viwanda bila ya kuviendeleza, kuviachia ili vipate kuendelezwa na wawekezaji wengine kwa mustakbali wa taifa

  • Aendelea kusisitiza Tanzania ni nchi tajiri na haikutakiwa kuwepo hapa ilipo

  • Akana vikali ufisadi na awaomba Watanzania waendelee kumuombea katika kupigana kutoka kwenye umaskini na kuelekea kwenye uchumi wa kati

  • Aelezea faida za utoaji elimu bure kwa watoto wa Tanzania ili waje kuwa na elimu ya kuitetea na kuilinda nchi yao

  • Aelezea miundombinu na mipango ya serikali kuelekea Tanzania mpya, Tanzania ya viwanda kwa kuzalisha umeme wa uhakika nchi nzima kwa kutumia pesa za mapato ya ndani

  • Asema mikakati yote hii ni kwa manufaa ya Watanzania wote wa hali ya chini na matajiri

  • Aelezea vipaumbele vya serikali katika kuleta maendeleo na atangaza miundombinu mipya na upanuzi wa uwanja wa ndege wa Mwanza kuwa uwanja wa ndege wa kimataifa ili upate kuchochea utalii na maendeleo kwa ujumla na athibitisha ahadi yake ya ujenzi wa meli ya ziwa Victoria

  • Katika kuchukua hatua hizi, awaomba wananchi wa Tanzania wavumilie katika kipindi hichi cha mabidiliko ya Tanzania mpya

  • Aelimisha kwamba kuwa na vyama tofauti siyo ugomvi, bali ni kuleta maendeleo hasa kwa wale wanaotambua maendeleo ya nchi

  • Amtaka Mheshimiwa Charles Mwijage kutenga pesa za kuwapa vijana kuwawezesha kujikwamua kiuchumi

  • Awataka wakuu wa mikoa kuwatafutia wafanyabiashara wadogo wadogo maeneo yenye miundombinu mizuri ya kufanya kazi zao za kupata riziki zao. Ajielezea kuwa habagui wafanyabiashara wadogo au wafanyabiashara wakubwa muhimu walipe kodi

  • Awataka viongozi kushirikiana na kuwa na umoja na mshikamano katika kuleta maendeleo ya wananchi

  • Aendelea kusisitiza viongozi wote kwenye ngazi zote kusimamia na kutatua kero za wananchi

  • Afanya makubwa kwenye hadhara hiyo baada ya kusikiliza kilio cha mama mjane hadharani aliyekuwa na matatizo ya muda wa miaka 9 kwa madai ya kusumbuliwa na kiwanja chake. Mheshimiwa rais alimtaka Mkurugenzi, Mkuu wa Mkoa na Naibu Waziri wa Ardhi kusimamia tatizo la huyo mama mjane na kupelekewa matokeo yake, na mheshimiwa rais akajitolea sadaka ya pesa kumpatia mama huyo. “Ahsante rais wa wanyonge, ahsante rais wa wanyonge”, mama huyo aliondoka akiyasema hayo

  • Awasihi wavuvi waache kutumia uvuvi haramu

  • Awaambia wana Mwanza wa vyama vyote vya siasa bila ya ubaguzi kuwa anawapenda na akawaomba washikamane katika kujenga Tanzania mpya

  • Awaahidi Watanzania kuwa siku zote atasimama kwa maslahi ya taifa

  • Mwisho, akampa fursa Mama Janeth Magufuli kuwasalimia wana Mwanza, na rais akawashukuru wana Mwanza wote kwa ukaribisho mzuri na akamaliza kwa kuiombea Mwanza, Tanzania na watu wake

 

MHESHIMIWA RAIS JOHN POMBE MAGUFULI AWAAPISHA VIONGOZI WATEULE, IKULU, JIJINI DAR ES SALAAM

  • Mheshimiwa Rais John Pombe Magufuli awaapisha viongozi wateule na awasihi kuzingatia sheria katika utekelezaji na wabaki kuwa watumishi wa umma na kutatua kero za wananchi wanyonge ambao hawana sauti katika jamii

  • Katika maapisho hayo, Mheshimiwa Rais afanya mabadiliko madogo ya uteuzi huo kwa kumhamisha Mheshimiwa Christine Mndeme, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma kwenda Mkoa wa Ruvuma, na Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Mheshimiwa Bilinith Mahenge kwenda mkoa wa Dodoma

  • Awataka wakuu wa mikoa na wakuu wa wilaya wateule na wanaoendelea kuleta mabadiliko ya kiuchumi katika maeneo yao ili kuleta maendeleo kwa wananchi

  • Awataka pia makatibu wakuu na manaibu katibu wakuu kutatua matatizo katika wizara zao kwa kushirikiana na kuwasaidia mawaziri kufanya kazi zao kwa ufanisi zaidi

  • Aainisha kwamba serikali imeshatenga na ishapeleka shilingi bilioni 147 za wanafunzi wa chuo kikuu kwa mwaka 2017/2018, kwa ambao wanastahili na wanakidhi vigezo vya kupata mkopo huo

  • Kwa maana hiyo, amesema mheshimiwa rais, atashangaa sana kama ataona mwanafunzi ambaye yupo kwenye orodha anayestahili kupata mkopo akalalamika hajapata

  • Amezitaka Wizara ya Fedha na Wizara ya Elimu kuhakikisha mikopo hiyo haitopata kwikwi au badala ya kwenda kwa wanafunzi ikapelekwa kwenye akaunti ya kunufaisha maslahi ya baadhi ya watu binafsi. Mheshimiwa rais aliainisha kwamba huu ni mfano tu lakini alisisitiza pesa za wanafunzi ziwafikie wanafunzi kwa wakati

  • Vilevile, amewataka mabalozi wa nje wanaoiwakilisha Tanzania, muda baada ya muda, wawe na utaratibu wa kueleza mafanikio ya uwekezaji nchini Tanzania kutoka nchi wanazoiwakilisha bila ya kujisahau

  • Mheshimiwa rais pia ataka wafanyakazi wa umma wanaopelekwa nje wawe na weledi na sifa zinazostahili

  • Akaendelea kusema kumekuwa na idadi kubwa uwakilishwaji wa Tanzania katika balozi za nje na akatolea mfano ubalozi wa Brazil nchini Tanzania kuwa una wafanyakazi wanne kwenye ofisi zao, na wafanyakazi wengine ni wananchi waajiriwa ambao wanafanya kazi zingine

  • Amteua na amtaka Mheshimiwa Adolf Mkenda, ambaye sasa ni Katibu Mkuu Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji, kuhamia Wizara ya Mambo ya Nje, kumsaidia na kufanya kazi na Mheshimiwa Augustine Mahiga kwenye maudhui ya kiuchumi

  • Awataka wateule wote kujua yanayoendelea katika maeneo yao na kuyafanyia kazi kwa niaba ya wananchi

  • Apigilia msumari kauli ya Jaji Mkuu, Mheshimiwa Ibrahim Juma, kwamba kisheria, Wakuu wa Mikoa ndiyo wenyeviti wa kamati ya maadili na kamati ya usalama, na kusimamia hayo ni utendaji wao wa kazi

  • Awapongeza na kuwashukuru viongozi wote waliohudhuria hapo pamoja na vyombo vya usalama kwa kufanya kazi nzuri ya kuendelea kulinda amani na utulivu nchini

  • Mwisho, akamalizia kwa kuliombea taifa na watu wake na kuendelea kwenye ajenda zingine za hafla hiyo

MHESHIMIWA RAIS JOHN POMBE MAGUFULI ATUNUKU VYETI VYA SHUKRAN NA PONGEZI KWA KAMATI MAALUM ZA UCHUNGUZI NA MAJADILIANO KUHUSU RASILIMALI NA MALIASILI YA MADINI NCHINI

  • Mheshimiwa Rais John Pombe Magufuli kwa niaba ya Watanzania, amewatunuku vyeti vya shukran na pongezi kwa kamati maalum za uchunguzi na majadiliano alizoziteua kuhusu rasilimali na maliasili ya madini nchini

  • Katika hafla hiyo, Mheshimiwa Palamagamba Kabudi ampongeza Mheshimiwa Rais kwa kuzikingia kifua maliasili za Tanzania na kutoka kwenye unyonywaji

  • Mheshimiwa Rais awashukuru wote waliohusika kwenye kusimamia suala zima la uchunguzi na majadiliano ya madini kwa uzalendo wao, na awashukuru Watanzania kuwa wavumilivu katika kipindi hiki kigumu

  • Apigilia msumari ufafanuzi wa Mheshimiwa Kabudi ya kwamba, makubaliano ya faida itakayopatikana ya asilimia 50 kwa 50 baina ya serikali na Barrick Gold Corporation haijawahi kutokea Afrika, na mbali na hilo, kampuni ya Barrick Gold Corporation itabeba dhamana ya gharama zote za rasilimali watu pamoja na kodi za serikali, na mbali na hayo serikali itapata shilingi za Tanzania bilioni mia saba (Tsh. 700 bilioni)

  • Ahoji hoja za watu wanaohoji hali ya uchumi wa Tanzania kwa madai ya kuwa umeshuka, akauliza je:

Serikali ingeweza kujenga reli mpya na ya kisasa kwa pesa yake taslimu?

Serikali ingeweza kununua ndege mpya 6 kwa mpigo mmoja kwa pesa yake taslimu?

Serikali ingeweza kutangaza ‘tender’ (zabuni) kwa mradi uliokuwa ni ndoto ya baba wa taifa, mradi wa Stiegler’s Gorge ambao utakaotoa megawatts 2100 hali ya kuwa sasa hivi Tanzania nzima inatoa megawatts 1460? mradi ambao pia pesa zake taslimu zipo tayari. Kama serikali haina pesa utatangaza ‘tender’ ya aina hiyo?

Serikali ingeweza kuongeza pesa ya bajeti ya huduma za afya kwa wananchi kutoka shilingi bilioni 31 mpaka bilioni 269?

Kama serikali haina pesa ingewezaje kusambaza umeme vijijini na inaendelea kusambaza umeme vijijini nchi nzima?

Kama serikali haina pesa ingewezaje kutangaza ‘tender’ ya kutengeneza meli mpya ya ziwa Victoria baada ya ajali iliyotokea ya MV Bukoba, meli ambayo itatengenezwa na wakandarasi wa Korea Kusini na pesa hiyo pia ipo tayari

  • Unaweza ukatoa mifano mingi ikiwemo ya barabara na ya madaraja ya kiwango cha lami zinazojengwa kwa pesa za ndani, alisema Mheshimiwa Magufuli

  • Awaomba Watanzania wasifuate takwimu zinazotolewa kinyume na takwimu za kiuchumi za serikali

  • Asema kazi kubwa iliyofanywa na kamati ya madini ya Almasi na madini ya Tanzanite ni kazi ya kupongezwa na si kazi ya kubezwa, kwasababu matokeo yake mazuri yalionekana baada ya siku chache tu kwa kukamatwa kwa almasi iliyotaka kusafirishwa kwa vipimo vya ulaghai

  • Asema juhudi hizi zilizofanywa na kamati na tume zote kusimamia madini hazikufanywa kwa maslahi yake binafsi, bali mapato yote yanayopatikana ni mapato ya serikali na ni mafanikio ya Watanzania wote

  • Atilia tena mkazo kwamba nchi yetu ni ‘donor country’ na siku zote imekuwa hivyo bila ya kujua, lakini sasa kila ‘donation’ itakayotolewa tutaijua

  • Kwa mantiki hiyo hiyo, ameelezea jinsi Watanzania wazalendo wanavyorubuniwa kuwa hawana mtaji

  • Afurahisha ukumbi kwa kusema ‘ukizaliwa tu Tanzania ni mtaji’

  • Awahamasisha Watanzania kutoka na dhana ya kuwa hawawezi kuwa na mtaji wa kujiendeleza kwa kuaminishwa kuwa hawawezi wakati wanaweza

  • Kwa mantiki hiyo hiyo, akasema tume ya uchunguzi na majadiliano ya madini imeweza kuwakilisha Watanzania na kuonyesha kwamba tunaweza

  • Awashukuru viongozi wa dini na viongozi wa vyama vya upinzani waliopongeza juhudi za serikali kwa maslahi ya Watanzania wote

  • Ahoji Benki Kuu ya Tanzania kwanini haikuzuia ‘tax avoidance?’

  • Ampongeza Gavana wa Tanzania, Profesa Benno Ndulu, ambaye anamalizia muda wake na akamtangaza Profesa Luoga kuwa Gavana mpya mtarajiwa wa Benki Kuu ya Tanzania. Amtaka Profesa Ndulu kumkabidhi majukumu ya kazi Profesa Luoga katika kipindi hiki

  • Amuomba Mheshimiwa Azan Zungu kufikisha salamu zake kwa Mheshimiwa Job Ndugai na aahidi kwa wakati muwafaka atakuja kuzungumza na wabunge

  • Kwa wafanyabiashara, amesema yeye na serikali yake inawapenda lakini walipe kodi na awasihi huu ndiyo wakati wa kufanya biashara kila sehemu

  • Asema nchi zote duniani zinahamasisha wananchi wake kuchukua fursa za kibiashara za ndani na mafanikio yanayopatikana ni mafanikio ya ndani ya nchi

  • Aitaka TIC kuhamasisha na kuwapa kipaumbele Watanzania kwenye fursa za kibiashara

  • Asema mafanikio ya Watanzania wajao yatakumbuka kizazi cha sasa hivi kutokana na fikra za kiakili za maendeleo ya baadae

  • Asema angekuwa na haja ya mali angetumbua na kufanya ubadhirifu alipokuwa wizara ya ardhi, wizara ya uvuvi na mifugo na wizara ya ujenzi jumla ya miaka 20, lakini aamini alikuja duniani bila ya pesa na atarudi bila ya pesa; awataka Watanzania kuwa wazalendo

  • Aiomba kamati ya majadiliano irudi tena kwenye meza ya mazungumzo na makampuni ya Tanzanite kusimamia maslahi ya taifa

  • Ataka mapato yote yatakayopatikana kutokana na juhudi hizi, yaende kwenye elimu ya watoto, madawa, miradi ya barabara na viwango vya hali ya maisha ya Watanzania yawe hali ya juu na hiyo ndiyo dira ya serikali ya awamu ya tano

  • Aelezea athari ya waandishi wa habari pale wanapoandika takwimu bila ya kuzingatia msingi wake na bila ya kufanyia utafiti wa ziada

  • Awaomba waandishi wa habari waweke Utanzania mbele

  • Mwisho akatoa fursa kwa wawakilishi wa viongozi mbalimbali waliohudhuria kuja kuwasalimia Watanzania na akawashukuru wote na kuwaombea Mungu