MHESHIMIWA RAIS JOHN POMBE MAGUFULI AZINDUA MFUMO WA MTANDAO WA PASIPOTI MPYA ZA TANZANIA ZENYE MFUMO WA KIELEKTRONIKI

 • Mheshimiwa Rais John Pombe Magufuli azindua mfumo wa mtandao wa pasipoti mpya za Tanzania zenye mfumo wa kielektroniki, jijini Dar es Salaam leo

 • Katika hotuba yake, Mheshimiwa Rais atambua uwepo wa Alhajj Mzee Ali Hassan Mwinyi, na viongozi wengine wakubwa wa kutoka bara na visiwani akiwemo Jaji Mkuu, Mheshimiwa Ibrahim Juma, Mheshimiwa Karume, Mheshimiwa Makungu, Mheshimiwa Zubeir, Mheshimiwa Tulia Ackson, Mheshimiwa Kijazi, Mheshimiwa Nchemba, balozi wa Ireland, Mheshimiwa Sherlock, na mabalozi wengine wa kutoka nchi mbalimbali, Mheshimiwa Makonda, Waheshimiwa Wabunge, Mstahiki Meya wa Dar es Salaam, Kamishna Mkuu wa Uhamiaji, Mheshimiwa Anna Makakala, Waheshimiwa Wakuu wa Ulinzi na Usalama kwa ujumla, viongozi wa siasa, dini, na waalikwa wote waliohudhuria hafla hiyo, uwepo wao ulitambuliwa na Mheshimiwa Rais John Pombe Magufuli

 • Awapongeza wafanyakazi wa Uhamiaji kwa kazi nzuri wanayoifanya na aelezea jinsi ya umuhimu wa idara ya Uhamiaji kwa masuala ya usalama wa nchi, na maendeleo ya nchi

 • Aelezea jinsi Idara ya Uhamiaji ilivyokuwa ikichezewa na kugeuzwa kuwa uchochoro wa wahamiaji haramu, wahalifu, na wafanyabiashara wa madawa ya kulevya, ambayo imepelekea kuharibu taswira ya nchi na kupelekea Watanzania halisi kupata tabu kuingia baadhi ya nchi na kusumbuliwa. Mbali na hayo, wengine wamepewa pasipoti za Tanzania hali ya kuwa wanamiliki pasipoti ya nchi nyingine ambavyo ni kinyume na sheria za nchi, alisema Mheshimiwa Rais Magufuli

 • Akaendelea kusema, sambamba na hayo, vibali vya makazi na vibali vya uraia wa Tanzania pia vilitolewa bila ya kufuata utaratibu na kupelekea wageni wengi kupata uraia bila ya kuwa na sifa stahiki, na wengine wakafikia mpaka kupata vyeo vikubwa ndani ya serikali wakati siyo raia wa Tanzania, wengine walipewa vibali vya makazi kiujanja ujanja, vilevile makusanyo ya mapato ya vibali na viza yalikuwa hayaridhishi. Hayo ni baadhi ya mapungufu yaliyojitokeza katika Idara ya Uhamiaji ambayo ilionekana kuwa imeshindwa kutimiza majukumu yake ipasavyo

 • Mapungufu haya ndiyo yamepelekea Mheshimiwa Rais Magufuli kufanya mabadiliko kwa kumteua mwanamama Mheshimiwa Anna Makakala kwa imani kwamba wanamama ni waaminifu na alipongeza kwa kufanya vizuri ingawa bado kuna mambo mengine hayajakamilishwa kusimamiwa kisawasawa, lakini aamini kwamba Mheshimiwa Anna Makakala atayasimamia kikamilifu bila ya uoga wowote, alisema Mheshimiwa Rais Magufuli

 • Awasihi wafanyakazi wa Uhamiaji waendelee kumpa Mheshimiwa Anna Makakala ushirikiano wa kutosha na amedokezwa kwamba wafanyakazi wa Uhamiaji wametoa ushirikiano wa kutosha. Kisha Mheshimiwa Magufuli akaondoa kiwingu kwa kufurahisha baraza baada ya kusema hasa wafanyakazi wanaume ndiyo wanatoa ushirikiano mzuri zaidi kwake

 • Mheshimiwa Rais akazungumzia umuhimu wa uzinduzi wa pasipoti mpya za kielektroniki ambazo zinatumika kama kitambulisho cha uraia wa mtu ambazo zina usalama zaidi kuliko pasipoti za zamani na mfumo wake. Pasi za kielektroniki zitakuwa kwenye mfumo wa kielektroniki ambao utaweza kusomwa nchi zote duniani ambazo zimo kwenye mfumo wa pasipoti za kielektroniki na itasaidia kurahisisha kuombea viza kwa haraka, kupunguza gharama za usafirishaji, na itapunguza upoteaji wa pasipoti siyo kama ilivyokuwa hapo awali kwenye mfumo wa zamani

 • Mfumo wa kielektroniki (e-Immigration) utakuwa na hatua nne mpaka kukamilika kwake na azipongeza ofisi za Uhamiaji na ofisi zingine zilizoshiriki katika kutekeleza mradi huo

 • Mheshimiwa Rais akaelezea jinsi ilivyokuwa akifuatilia mradi huu kwa karibu sana na akiri kwamba ilikuwa siyo kazi ndogo. Mheshimiwa Rais aainisha kwamba gharama za mradi wa mfumo wa pasipoti za kielektroniki ni dola za Kimarekani, milioni 57.82 sawa na shilingi za Tanzania, bilioni 127.2 ambapo awali mradi huo ulipangwa kutekelezwa kwa dola za Kimarekani, milioni 226 sawa na shilingi za Tanzania, bilioni 400 na ndiyo maana siku za nyuma baadhi ya watu walipiga kelele juu ya mradi huu kwa ajili ya maslahi yao binafsi kwa makusudio ya kula pesa za Watanzania, alisema Mheshimiwa Rais Magufuli

 • Aelezea jinsi vyombo vya dola vilivyofanya kazi nzuri ya kugundua mikakati hiyo, na aishukuru serikali ya Ireland kwa kusimama imara katika kuidhamini Tanzania kwenye mradi huo na mpaka kupatikana kampuni nzuri ambayo ilichukua mradi huo kwa dola za Kimarekani, milioni 57.82 ambayo ni sawa na shilingi za Tanzania, bilioni 127.2 badala ya shilingi bilioni 400, na ampongeza Mheshimiwa Makakala na Wizara ya Mambo ya Ndani kwa kazi nzuri waliyoifanya

 • Mheshimiwa Rais akaendelea kusema kwamba kutokana na matokeo hayo, Kamishna wa Idara ya Uhamiaji alipoomba nyumba za wafanyakazi wa Uhamiaji kwa makazi mapya ya Makao Makuu, Dodoma, aliwapatia nyumba 103 mjini Dodoma, kwasababu ya uzalendo ambao wameuonesha. Vilevile, Mheshimiwa Rais akawaongeza shilingi za Tanzania, bilioni 10 za kutengenezea Makao Makuu yao mapya kutokana na kuonesha kazi nzuri walizozifanya

 • Awasisitiza kuendelea na kazi nzuri. Awatanabahisha kwamba kuna Wakongo takriban 1,500 ambao wameingia mpakani, lakini walioripoti kambini ni chini ya 1,000 na wengine wameshaingia mitaani. Awapa changamoto ya kuwatafuta, na wakamatwapo wahamiaji wowote haramu wahojiwe mikoa waliyopita ili wapate kujua wamepita vipi mkoa hadi mkoa

 • Aelezea umuhimu wa Idara ya Uhamiaji kwa nchi kwenye mambo ya kudhibiti uhalifu na ukusanyaji wa mapato. Amshukuru tena balozi wa Ireland na ampongeza kwa kuongea Kiswahili, na aishukuru kampuni ya HDI iliyofanya kazi ya kuunda mfumo huu wa pasipoti za kielektroniki, na awashukuru Watanzania wote

 • Aainisha mradi huu umelipwa na serikali kwa pesa taslimu za Watanzania wanaolipa kodi na anawapongeza Watanzania wote na awasihi kuendelea kulipa kodi ili serikali iwaboreshee miradi kama hii na huduma mbalimbali za kijamii

 • Aainisha gharama za pasipoti mpya zimezingatia ubora wake, na zina kurasa nyingi kuliko za zamani, ni za kielektroniki, na pia bei yake ni rahisi kuliko nchi nyingine zenye pasipoti za kielektroniki kama hizi. Awasihi Watanzania wapatapo pasipoti hizi wazilinde, wazitunze, na wasizifanyie harakati za kughushi

 • Awataka wafanyakazi wa Uhamiaji kuharakisha huduma za wananchi na huduma za wageni. Akaelezea kwa vile taasisi zote husika zimeshirikiana katika kufanikisha mfumo huu, atashangazwa kuona kama mteja atacheleweshewa viza, au kibali cha makazi kutolewa kiholela, au kama mapato hayatoongezeka. Awasihi kuzingatia masuala ya usalama wa nchi

 • Aipongeza Uhamiaji kwa kufanya operesheni ya kutambua watu wasio raia na wanaofanya kazi kinyume na sheria, na akawasihi kuipenda nchi yao. Akaendelea kusema Idara ya Uhamiaji inahitaji maadili makubwa na awaomba wafanyakazi kuendelea kuwa na maadili na kupiga vita rushwa

 • Mheshimiwa Rais atambua mahitaji ya Idara ya Uhamiaji na awahakikishia ikiwa wataenda na mwendo huo walioanza nao wa kubadilika, na changamoto zao zitabadilika, na aitaka iwe ni idara ya mfano kwa umuhimu wake

 • Awapongeza wakazi wa Dar es Salaam kwa kujitokeza kwa wingi kwenye hafla hiyo, na awahakikishia changamoto za msongamano wa magari utapungua kutokana na hatua zilizochukuliwa na serikali kwa kujenga barabara za juu kwenye makutano ya barabara za TAZARA, na barabara za juu kwenye makutano ya barabara za Ubungo, ambazo gharama zake ni shilingi za Tanzania, bilioni 300

 • Aelezea kuanza kwa ujenzi mwingine wa awamu ya pili ya mabasi ya mwendo kasi kutoka mjini hadi Mbagala, na kuanzia mwezi wa pili, barabara ya Morogoro itaanza kupanuliwa kuwa barabara ya njia sita kutoka Kimara hadi Kiluvya yenye urefu wa takriban Kilomita 16, vilevile kuanza kwa ujenzi wa reli ya kisasa kutoka Dar es Salaam hadi Dodoma, yenye umbali wa Kilomita 712 itakayogharimu trilioni 7.06 ambazo zitalipwa taslimu na serikali; na awamu ya pili, itaenda Mwanza na Kigoma, kuungana na reli itakayoenda Burundi na Rwanda; itakapokamilika, reli hii itarahisisha usafiri kati ya Dar es Salaam na Dodoma

 • Sambamba na hayo, miradi mingine inaendelea kuboreshwa ikiwemo miradi ya afya, elimu, usambazaji wa maji ya kutoka Ruvu. Na hivi sasa miradi mingine inaendelea ya kuchimba visima virefu huko Mpera na Kimbiji kwa malengo ya kusambaza maji kwenye maeneo ambayo kwa sasa hayana mtandao wa mabomba ya maji na miradi hii itawezesha kupanua huduma ya maji katika sehemu ambazo hazijafikiwa na maji katika jiji la Dar es Salaam

 • Kwenye afya, Mheshimiwa Rais Magufuli ameelezea jinsi serikali inavyoboresha hospitali za taifa, Muhimbili, taasisi ya saratani ya Ocean Road, na hivi majuzi hospitali kubwa ya kisasa ya Mloganzila ilizinduliwa ambayo inaipunguzia mzigo mkubwa hospitali ya Muhimbili ambapo hivi sasa hospitali ya Mloganzila imeshachukua wagonjwa 140

 • Mheshimiwa Magufuli aahidi kuendelea kuijengea uwezo hospitali ya Mloganzila na kuziboresha hospitali za wilaya kama hospitali ya Amana, Mwananyamala, na Temeke, pamoja na vituo vya afya vipatavyo vitano ndani ya jiji la Dar es Salaam vikiwemo viwili ndani ya Wilaya ya Temeke, Yombo Vituka na Maji Matitu, ili viweze kukidhi haja za kina mama waja wazito

 • Kwenye elimu, Mheshimiwa Rais aahidi elimu kuboreka na awaomba wananchi waendelee kuiunga mkono serikali na kukiunga mkono Chama Cha Mapinduzi, kudumisha amani, kuchapa kazi, na kulipa kodi

 • Mwisho amalizia hotuba yake kwa kuwashukuru viongozi wote waliohudhuria kwenye hafla hiyo, na amshukuru Rais wa Zanzibar, Mheshimiwa Ali Mohammed Shein, Mheshimiwa Tulia Ackson, viongozi wengine wakuu wa ulinzi na usalama, na mabalozi. Akahimiza wananchi wajitoe kwenye kuchukua pasipoti mpya, na akamalizia kuombea Mungu pasipoti mpya za kielektroniki, Idara ya Uhamiaji, Wana Dar es Salaam, na Tanzania yote