AIR TANZANIA BOEING 787-8 DREAMLINER IKIRUKA KWENYE MAJARIBIO YA MWANZO MJINI SEATTLE LEO

Advertisements

MHESHIMIWA ADELARDUS KILANGI AFAFANUA SINTOFAHAMU YA PESA ZA ‘EXPORT LEVY’ YA KOROSHO, AELEZEA UBADHIRIFU WA PESA ULIOFANYIKA KWENYE BODI YA KOROSHO YA ZAMANI, AELEZEA MAPUNGUFU YALIYOBAINIKA YA SHERIA YA BODI YA KOROSHO BAADA YA SHERIA YA MWAKA 2009 KUPITISHWA, AMBAYO BAADAYE BODI YA KOROSHO HAIKUKAMILISHA MCHAKATO WA MFUKO WA PESA ZA KOROSHO KWA KUPITISHA BUNGENI KAMA SHERIA ILIVYOTAKA, AELEZEA KUTOKANA NA MAPUNGUFU HAYO KUTOKAMILISHWA KISHERIA SERIKALI INATUMIA SHERIA ILIYOPO HIVI SASA KIFUNGU CHA 12(1) NA 12(2) CHA MWAKA 2001 YA MFUKO WA PESA ZA UMMA, KWAHIVYO, PESA HIVI SASA ZILIPO KISHERIA HAZIRUHUSIWI KUTOKA KWENYE MFUKO MKUU WA SERIKALI KUTOKANA NA KIFUNGU CHA 13(2) CHA MWAKA 2001 YA MFUKO WA PESA ZA UMMA, NA HATIMAYE PESA HIZO ZITAENDA KWENYE MATUMIZI YA KUWALETEA MAENDELEO WATANZANIA WOTE NCHINI CHINI YA UONGOZI MAHIRI WA AWAMU YA TANO YA MHESHIMIWA RAIS JOHN POMBE MAGUFULI

JAMII YA TANZANIA NA ATHARI ZA UTANDAWAZI WA KIUCHUMI NA KISIASA

Jana nilipata fursa ya kuangalia YouTube video clip iliyorushwa na Global TV juzi ikimuonesha Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Mheshimiwa Gaudensi Milanzi (2018) inayohusu kongamano lililofanyika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) linalohusu kuendeleza utalii kwenye fukwe yote ya bahari ya Tanzania inayosemekana kutoka Tanga mpaka Mtwara kwa kujenga mahoteli ya kitalii. Ifahamike kwamba simzungumzii Mheshiiwa Gaudensi Milanzi ambaye ni Katibu anayefanya kazi yake vizuri kabisa ila nazungumzia wazo na fikra ya mradi huu kama mradi mzima ambao nimeshindwa kuvumilia na kunifanya niandike makala hii fupi na kugusia mambo mbalimbali machache yanayogusa maendeleo yetu nchini.

Fikra hii ya kujengwa kwa mahoteli ya kitalii, ina athari kubwa sana katika jamii yote inayoishi kanda ya Pwani ambao hawatofaidika na miradi hiyo. Siyo tu kufaidika kiajira, bali hawatofaidika kiuchumi na hata kijamii hawana faida nao mradi huu. Na nitaelezea athari zake kama ifuatavyo.

Unapofanya fukwe yote ya bahari ya Tanzania nzima kama inavyosemekana kutoka Tanga mpaka Mtwara kuwa na mahoteli ya kitalii, athari yake ni kwamba, kwanza wakazi wengi wa Pwani ambao wengi wao ni maskini unawazuia njia yao (access) ya kwenda Pwani kufanya uchumi wao wa uvuvi wa kuwapatia vijisenti vya kusukuma maisha yao ya kila siku, na vilevile ni kuwazuia wakazi wa Pwani kwenda kujifurahisha maeneo ya baharini na familia zao katika ardhi yao wenyewe waliyopewa na Mungu wao. Hali hii siyo Pwani tu, tumeona hata wananchi wa mkoa wa Geita, Tabora na Kahama wakilalamika kuachiwa mashimo ya madini na hali ya kuwa wananchi kutofaidika na ardhi zao na kuwachwa na umaskini mpaka hii leo.

Pili, sehemu hizo za Pwani zitakapojengwa mahoteli ya kitalii, ardhi yake itapanda bei. Nilielezea hili siku za nyuma (Katundu, 2017) na nikafafanua hali ya Gentrification inavyokuwa na athari zake katika jamii ni kuwa majengo mapya ya hali ya juu yanapojengwa sehemu, wanaoumia ni watu maskini wa maeneo hayo. Inawapelekea wakazi wa maeneo hayo kutokana na umaskini wao waondoke maeneo hayo na kusambaratika na matokeo yake ni kuuwa mila zao na kuuwa utamaduni wao ambazo ni mila na ni tamaduni za Kitanzania za jamii ya Watanzania. Sawa, tunaweza kudai kuwa ardhi ya nchi ni ya serikali, lakini serikali ina dhima kubwa kuangalia maslahi ya wananchi wenye asili ya ardhi ya waliyopewa na Mungu kuliko kitu kingine chochote. Wakati mwingine huwa najiuliza hivi kweli hawa wanaofikiria kufanya vitu kama hivi ni hufanya kwasababu ya kutokujua au ni nini hasa malengo? Pia huwa najiuliza je hawa wanaofikiria kufanya vitu kama hivi ni Watanzania kweli wa asili au ndiyo tumefikia mahali ambapo tunatambuana usoni lakini hatujuani yaliyo moyoni nani ni nani? Huwa pia najiuliza je hawa wanaofikiria kufanya vitu kama hivi, kweli hawa ni wazalendo wa nchi yao? Ni dhambi kubwa kumuumiza ndugu yako wa taifa moja kwa faida ya mtu wa nje. Mwalimu Nyerere aliyajua haya, ndiyo maana alisema tuonapo maendeleo hayaendani na misingi yetu ya taifa tuchukue hatua moja nyuma kisha tutafakari.

Mfano kama huu wa kufanya fukwe za bahari kuwa na mahoteli si jambo geni na ni mfano unaotaka kujirudia tena nchini kwetu. Ni yale yale yaliyotokea miaka ya 80 na 90 ndani ya kisiwa cha Mafia maeneo ya Utende kujengwa hoteli za kitalii na wakazi wa maeneo hayo ambao ni maskini hawakuwa na fursa na wala kufaidika nazo hizo hoteli. Matokeo yake baadhi yao wakazi wa maeneo hayo walilazimika kuuza maeneo yao ya Pwani kwasababu ya hali ngumu ya kimaisha na pia uchumi wao mkuu wa kuuza nazi ukafa kutokana na sera za ubinafsishaji za watu wa Magharibi. Mbali na hayo, wakazi wa Mafia walilalamika sana na mpango huo wa kujengwa hoteli, siyo tu kwa kukosa njia ya kwenda pwani kufanya kazi zao za kiuchumi na kujifurahisha na familia zao, lakini pia kutokana na kukosa (sitaki kutumia neno kukoseshwa) kielimu, hoteli zote zilizojengwa wameshindwa kupata ajira za uongozi wa hoteli hizo angalau wafaidike nazo lakini wameishia baadhi yao kuwa ni wafagizi na wapiga deki kwenye mahoteli hayo na ajira za juu kwenye menejimenti kwenda kwa watu ambao siyo watu wa Mafia. Kwa kweli inauma sana. Halafu bila ya aibu baadhi ya watu wanasimama bungeni kutetea haki za binadamu za ndoa za utotoni na usawa wa kijinsia? Kweli? Kuna usawa gani hapa?

Isitoshe, imefikia leo mwana CCM anajiita kuwa yeye ni mwana CCM na anaiwakilisha CCM kisha anasimama hadharani na mishipa ya shingo inamtoka na kutangaza kuwa yeye siyo muumini wa Ujamaa. Hapa ndipo tulipofikia kama nchi. Ikiwa wewe ni mwana CCM na huna imani na Ujamaa ni bora uhamie chama kingine au anzisha chama chako mwenyewe. Kwani nani aliyesema katiba ya Chama cha Mapinduzi au katiba ya Tanzania imefutwa mpaka wewe mwana CCM unathubutu kusimama hadharani na kusema wewe siyo muumini wa Ujamaa. Kwa kweli tuna kazi kubwa hapa tulipo na huko tunapoenda. Lakini bila ya kuangalia tunapotoka na yepi yaliyotufikisha hapa tulipo kisha tukarudia makosa hayo hayo tena na tena, nchi yetu na watu haitopiga hatua ya maendeleo.

Nimekuwa nikifuatilia mkutano wa 11 wa bunge unaondelea kwenye vikao mbalimbali vinavyojadili kuhusu mambo mbalimbali nchini. Nimesikiliza hoja za msingi za baadhi ya wabunge kuhusu zao la korosho linalohusu wananchi wa mkoa wa Pwani na kushuka nyanda za Kusini mwa Tanzania ambalo lilileta faida kubwa nchini mwaka 2016/2017 lakini mpaka hii leo, kati ya shilingi bilioni 210 za wakulima maskini wa zao la korosho zilizopatikana, wakulima wamepata shilingi bilioni kumi tu (kama sijakosea) kutokana na maelezo ya baadhi ya waheshimiwa wabunge. Mbali na hilo, unaposikia mpaka hii leo hakuna pesa ya pembejeo za wakulima wa korosho ili wapate kunufaika tena mwaka huu kwa zao lao kwa mwaka 2017/2018 au 2018/2019, unaposikia mikorosho ya Pwani na nyanda za Kusini imepata ugonjwa mpya wa mnyauko na hatua zilizopendekezwa na Wizara ya Kilimo ni kukata mti kwa kutumia panga sehemu zilizoathirika na ugonjwa huo halafu usilitumie tena panga hilo hilo kukatia sehemu nyingine lililoathirika na ugonjwa huo, unakaa unajiuliza huyu maskini pesa yake hajalipwa ya mazao yake ya korosho, pili anahitaji mapanga mangapi kukatia mikorosho yake, na pia pembejeo za msimu mpya hana, wakati huo huo unasikia miradi ya mikorosho mipya inaanzishwa sehemu nyingine za Tanzania ambazo zingine zinadaiwa kuwa hazina ardhi madhubuti ya kukuza mikorosho, maana yake uchumi wa korosho umekufa Pwani na nyanda za Kusini. Hii ni nini maana yake? Kisha tunajiuliza ni nani aliyeturoga? Jibu lake ni sisi wenyewe kujipeleleza na kujiuliza kisha ndiyo tutamjua mbaya ni nani.

Mheshimiwa Mbaraka Dau (2018) juzi bungeni ameelezea kwamba, meli nyingi za kigeni zinakuja kwenye bahari yetu kwenye kina kikubwa na kuvua samaki na kuondoka bila ya taifa kupata mapato. Tunawaachia watu wa nje wavue samaki wetu bila ya kudhibiti maliasili yetu lakini wakati huo huo tunawakamata Watanzania maskini kwenye vikapu vyao na wengine kupimwa urefu wa samaki wao.

Ushauri wangu ni kwamba, unapoziwezesha sehemu ambazo zinafanya vizuri kiuchumi, kwa mfano Pwani na nyanda za Kusini kwenye mikorosho, na pia kuziwezesha na kuziongezea uchumi wa uvuvi na kuweka miundombinu bora na siyo kuhamisha zao hilo au uchumi huo kwenda sehemu nyingine, unapoziwezesha sehemu zenye mifugo mingi kukamua maziwa na kuuza nyama na ngozi, unapoziwezesha sehemu zenye madini, na sehemu zenye maziwa yanayozalisha samaki kuzijengea uwezo wa uvuvi kama sehemu za Pwani na kuimarisha udhibiti na kuwapa afuweni wavuvi wadogo na wakubwa wa ndani, unapoziwezesha sehemu za kitalii za Kaskazini na Kusini, na kadhalika, yote haya matokeo yake mkusanyiko wa mapato yote yatainua hali ya uchumi wa wananchi wa maeneo hayo na taifa kwa ujumla na siyo kudidimiza uchumi wa eneo fulani na kulijengea upya au kulazimisha uchumi wa aina fulani kufanyika sehemu nyingine. Na wakulima wa korosho warejeshewe haki yao ya pesa zao walizozichuma mwaka 2017/2018 ambazo zitaingia kwenye mzunguko wa matumizi ndani ya nchi. Ikiwa tutafanya hivi kuendeleza pale tulipopata matokeo mazuri kama yaliyofanyika mwaka 2017/2018 kwenye mikorosho maana yake faida haitokuja sehemu moja tu bali itafaidisha kunyanyua uchumi wa watu wa sehemu husika na kuwatoa kwenye umaskini kwa vile walivyopewa na Mungu wao na vilevile taifa zima litafaidika kwa kukusanya kodi ya mapato hayo na kuleta maendeleo sehemu nyingine za nchi.

Kama inavyosemekana, mwaka jana serikali ilikusanya mapato mengi sana kwenye zao la korosho, kwahiyo kwanini tusiliendeleze hilo kwa sehemu hizo hizo zilizoleta mafanikio hayo? Waswahili husema, kujaa kwa maji pwani, hunyanyua ngarawa zote zilizo mchangani. Na kinyume chake, kukupwa kwa maji pwani, ngarawa zote zinalala mchangani.

Nampongeza Mheshimiwa Rais John Pombe Magufuli kwa hatua zake alizochukua za mwaka 2017/2018 kuwasaidia watu wa Pwani na kanda ya Kusini kwa zao la korosho kimnada na kwa baadhi ya pembejeo. Pia nampongeza Mheshimiwa Rais John Pombe Magufuli, nakumbuka katika hotuba yake mwaka jana (2017) alipiga vita kusikia neno ‘mnyauko wa korosho’ lakini leo Wizara ya Kilimo imerudi kinyume kabisa na hakuna hatua madhubuti zinazochukuliwa kuokoa zao hili na wizara husika.

Mheshimiwa Rais wetu mpendwa John Pombe Magufuli anafanya kazi kubwa sana ya kutuletea maendeleo nchini kwa manufaa ya wananchi wote wa Tanzania, lakini kama nilivyowasikia wakisema baadhi ya Waheshimiwa Wabunge wa vyama vyote kwamba, Mheshimiwa Rais Magufuli ana nia njema na maendeleo ya nchi yake lakini kuna baadhi ya watu waliomzunguka hawamshauri vizuri kwenye sera za nchi ingawa yeye mwenyewe ana uzalendo na taifa lake. Haya ni maneno ya baadhi ya Wabunge wengi wamekuwa wakiyarudia mara kwa mara kwenye vikao vyao vya wabunge na hawakumtaja au kumuoneshea kidole mtu yeyote aliye karibu na Mheshimiwa Rais Magufuli. Matokeo yake, kazi zote nzuri anazozifanya Mheshimiwa Rais Magufuli zitakuwa kama kujenga ukuta katikati ya bahari.

Nikiangalia kutangazwa kwa miradi ya hizi hoteli na hali ya korosho inavyoenda, ni viashiria kwamba ipo haja ya watu wa chini wa serikali na watu wa chini wa chama ikiwa wana nguvu ya kujiamulia tu na kufanya maamuzi ya kutekeleza miradi na mambo mbalimbali ya maendeleo ya taifa ya kijamii bila ya kujali au kuijua misingi ya taifa, maendeleo ya kudumu nchini kwetu Tanzania yatakuwa ni ndoto. Makala hii fupi nitairudia tena kwenye muendelezo wa Makala yangu ya athari za maendeleo ya Tanzania na utandawazi wa kisiasa sehemu ya pili ili kuangaza zaidi wapi Tanzania inatoka, wapi ilipo, na wapi inaelekea.

Tusipobadilika kifikra sasa na kuendelea kulinda uhuru wetu wa kujitawala wenyewe kutokana na mazingira yetu ya ndani ya nchi, tujijue kuwa bado tumo kwenye ukoloni na tusifikirie kukinai dhahabu kwa muda mrefu sana kama siyo milele. Huu ndiyo ukweli.

Nayasema haya kwasababu naipenda nchi yangu na nampenda Rais wangu. Napongeza juhudi zote zinazofanywa na Mheshimiwa Rais John Pombe Magufuli kwani ni mmoja wa Watanzania atakayekumbukwa kulitoa taifa la Tanzania kwenye umaskini na kuleta maendeleo makubwa nchini kwa kufuata nyayo za baba wa taifa. Bila ya kumsahau baba wa taifa Mwalimu Nyerere, busara zako tutazikumbuka milele.

Ndugu yenu.

Saleh Jaber

23/06/2018
MAPYA:
Sehemu hii ya maelezo imehaririwa tarehe 26 Juni 2018 na Saleh Jaber:

Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Mheshimiwa Adelardus Kilangi leo tarehe 26 Juni 2018 amesimama mbele ya bunge tukufu kufafanua sintofahamu ya pesa za ‘Export Levy’ ya zao la korosho.

Mheshimiwa Kilangi aelezea ubadhirifu wa pesa uliokuwa ukifanyika na bodi ya korosho ya zamani na mpaka kupelekea kubadilishwa kwa mfumo wa upokezi wa pesa.

Aelezea mapungufu yaliyobainika ya sheria ya bodi ya korosho baada ya sheria ya mwaka 2009 kupitishwa, ambayo baadaye bodi ya korosho haikukamilisha mchakato wa mfuko wa pesa za korosho kwa kupitisha bungeni kama sheria ilivyotaka.

Aelezea kutokana na mapungufu hayo kutokamilishwa kisheria, inawalazimu serikali kutumia sheria iliyopo hivi sasa kifungu cha 12(1) na 12(2) ya mwaka 2001 ya mfuko wa pesa za umma.

Kwahivyo, pesa hivi sasa zilipo kisheria haziruhusiwi kutoka kwenye mfuko mkuu wa serikali kutokana na kifungu cha 13(2) cha mwaka 2001 ya mfuko wa pesa za umma, na hatimaye pesa hizo zitaenda kwenye matumizi ya kuwaletea maendeleo Watanzania wote nchini, chini ya uongozi mahiri wa awamu ya tano ya Mheshimiwa Rais John Pombe Magufuli.

MAREJEO:

Dau, M. (2018) BAKHRESA Ameipa Serikali Meli, Wizara Bado Inasua sua Tu. [Online] YouTube. Available at:

[Accessed 23 June 2018].

Katundu, S. (2017) Walichokisema Wananchi wa Mkuranga. [Online]. Available at: https://sjposters.wordpress.com/2017/05/30/wakazi-wa-mkuranga-walonga-hali-halisi-ya-unyanyasaji-na-kero-kwa-wakazi-wa-mkoa-wa-pwani/ [Accessed 23 June 2018].

Kilangi, A. (2018) Serikali Yatoa Ufafanuzi Sakata la Korosho. [Online] YouTube. Available at:

[Accessed 26 June 2018].

Milanzi, G. (2018) Tanzania Yanusa Utajiri Kupitia Fukwe. [Online] YouTube. Available at:

[Accessed 23 June 2018].

MHESHIMIWA RAIS JOHN POMBE MAGUFULI APOKEA GAWIO LA PATO LA SHIRIKA LA TAIFA LA MAWASILIANO TTCL, ATOA WITO KWA WANANCHI KUTUMIA HUDUMA ZA TTCL, ATOA WITO KWA TAASISI ZA SERIKALI KUTUMIA HUDUMA MPYA YA ‘VIDEO CONFERENCING’ YA TTCL AIPONGEZA TTCL NA WAFANYAKAZI WAKE KWA KUFIKIA MAFANIKIO, AMPONGEZA MHESHIMIWA WAZIRI MBARAWA NA JOPO LAKE, AMPONGEZA SPIKA NDUGAI NA JOPO LAKE, ALIPONGEZA JESHI LA ULINZI NA KUJENGA TAIFA, AWAHAKIKISHIA WATANZANIA PESA ZOTE ZITAENDA KWENYE MAENDELEO YA TAIFA, AZITAKA TAASISI NA MASHIRIKA YA SERIKALI KUFUATA MFANO WA TTCL WA KUTOA GAWIO ILI KULETA MAENDELEO NCHINI, ASISITIZA AMANI NCHINI NA AZINDUA RASMI HUDUMA ZA TTCL NCHI NZIMA

Kutoka Ikulu.