Mashindano Ya Qur’an Tanzania Yaliyofanyika Diamond Jubilee Hall Dar es Salaam


Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akimkabidhi mshindi wa kwanza kwa upande wa wanawake na mshindi wa jumla wa kuhifadhi Qur’an juzuu 30, Ashura Amani (16) mwanafunzi wa kidato cha tatu katika shule ya sekondari ya Benjamini Mkapa, ikishuhudiwa na mwanaharakati wa kidini na kijamii na muasisi wa Taasisi ya Aisha Sururu Foundation, Bi Aisha Sururu (katikati).

MAKAMU WA RAIS AHIMIZA WATOTO KUPEWA ELIMU KATIKA MASHINDANO YA KUHIFADHI QUR’AN

samia suluhu

Makamu wa Rais Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan amewataka wazazi nchini kuhakikisha wanawapa watoto wao elimu tangu wakiwa wadogo ili iwajengee misingi bora katika maisha yao.

Mheshimiwa Samia ameeleza hayo wakati akizungumza kwenye mashindano ya Qur’an yaliyofanyika leo katika ukumbi wa Diamond Jubilee Hall, jijini Dar es Salaam. Alisema wazazi wanapaswa kutambua kuwa hakuna zawadi kubwa kwa mtoto kama elimu kwa sababu itamjengea misingi ya kujua afanye nini katika kuendesha maisha yake kwa mafanikio.

“Vile vile, niwaombe wazazi tuwatengenezee watoto wetu fursa wapate muda wa kupata elimu. Ukimpa utajiri mtoto na kwa kuwa hana elimu anaweza asiutumie vizuri; lakini ukimpa elimu itamfaa katika kuendesha maisha yake,” alisema Makamu wa Rais.

Aidha, aliwataka washindi wote wa kuhifadhi Qur’an wasisite kutafuta elimu zaidi ya dini na ya dunia kama maandiko ya kitabu kitakatifu cha Qur’an yanavyousia ili iweze kuwasaidia ulimwenguni na huko akhera kwenye maisha ya milele.

Makamu wa Rais alielezea kufarijika kwake kuona kuwa idadi ya washindani inaongezeka kila mwaka bila ya kubagua jinsia zao na washiriki wa mashindano hayo wakiwa na umri mdogo.”Hii inaonyesha kwamba vijana wanayo fursa nzuri ya kuhifadhi Qur’an Tukufu tena juzuu nzima wakiwa wadogo endapo sisi kama wazazi tutalifanyia kazi na kuwahimiza vijana wetu,” alidokeza.

Mapema Katibu wa Taasisi ya Aisha Sururu Foundation iliyoandaa mashindano hayo Bi Jokha Lemky alimweleza Makamu wa Rais kuwa kwa mwaka huu mashindano hayo yameshirikisha mikoa 24 ya Tanzania Bara na Visiwani yakiwa na washiriki 653 ambapo 66 ndiyo wameingia fainali.


Alisema pamoja na mafanikio hayo lakini Taasisi hiyo inakabiliwa na changamoto za kukosekana kwa kompyuta, photocopy, usafiri, scholarship na zawadi kwa washindi jambo ambalo Makamu wa Rais alisema atajitahidi kufanya kazi bega kwa bega na Taasisi hiyo katika kutatua changamoto hizo.

Katika mashindano hayo ya kuhifadhi Qur’an Makamu wa Rais alikabidhi zawadi kwa washindi waliohifadhi juzuu tatu hadi 30 ambapo aliyehifadhi juzuu 30 alipata shilingi milioni tano. Mashindano hayo yalihudhuriwa na waumini mbalimbali wa dini ya kiislam wakiwemo Balozi wa Algeria nchini na wawakilishi wa mabalozi wa Misri, Sudan na Iran.


Sehemu ya Viongozi waliohudhuria mashindano hayo ya kuhifadhi Qur’an.


Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan (katikati) akizungumza na Mwenyekiti Mtendaji wa Taasisi ya Aisha Sururu Foundation, Bi. Aisha Sururu (kushoto) na Katibu wa Taasisi hiyo Bi. Joha Lemky (kulia) wakati wa mashishindano ya kuhifadhi Qur’an  yaliofanyika kwenye ukumbi wa Diamond Jubilee Hall.


Sheikh Muharami Mziwanda akitoa elimu juu ya umuhimu wa kuijua Qur’an  kwenye ukumbi wa Diamond Jubilee Hall.


Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan (katikati) akiwa kwenye picha ya pamoja na washiriki wa kike walioshiriki mashindano ya kuhifadhi Qur’an kwenye ukumbi wa Diamond Jubilee.


Majaji wa Mashindano ya kuhifadhi Qur’an  yalioandaliwa na Taasisi ya Aisha Sururu Foundation.

Mashindano Ya Qur’an 2016 Tanzania – Aisha Sururu Foundation

wpid-fb_img_1440929286581.jpg

Assalaam alaykum,

Aisha Sururu Foundation ina furaha kuwaalika kwenye fainali ya mashindano ya mwaka 2016 (1437 AH) ya kuhifadhi Qur’an tukufu itakayofanyika Jumapili ya tarehe 19/06/2016 katika ukumbi wa Diamond Jubilee Hall, ambapo vijana wanawake na wanaume watakaoshiriki katika mashindano haya watapigania nafasi zao za kwanza kwenye jukwaa la mashindano ya kuhifadhi Qur’an katika mwezi huu mtukufu wa Ramadhan.

Mashindano ya kuhifadhi Qur’an ya mwaka huu yatakuwa ni mashindano ya kumi na nne (14) tangu mashindano ya kuhifadhi Qur’an yanayoandaliwa na Aisha Sururu Foundation yaanzishwe, Alhamdulillah.

Mwaka huu Aisha Sururu Foundation imeshirikisha mikoa 24 ya Tanzania pamoja na visiwa vya Zanzibar, Unguja na Pemba, kwa nia ya kuwashajiisha watoto kuhifadhi Qur’an katika viwango vya juu vya kuisoma Qur’an tukufu.

Kauli Mbiyu ya Mwaka Huu: Tuwathamini Waalimu Wetu wa Qur’an Tukufu, Tupate Radhi za Mola Wetu Ra’ufu.

Tukio: Mashindano ya Kuhifadhi Qur’an Tukufu.

Tarehe: 19/06/2016.

Ukumbi: Diamond Jubilee Hall, Dar es Salaam, Tanzania.

Wakati: Saa 2 Asubuhi Mpaka Saa 8 Mchana (8am – 2pm).

Mgeni wa Heshma: Mheshimiwa Makamu wa Rais, Bi Samia Suluhu.

Shukran.

Wabillahi Tawfeeq,

AISHA SURURU FOUNDATION